Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
akisalimiana na mwakilishi wa VSO Tanzania Jean Van Wetter wakati
alipowasili katika viwanja vya Ukimbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini
Unguja leo katika hafla ya sherehe ya kukabidhi Vihori kwa wakulima wa
Mwani. (Picha zote na Ikulu)
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
akifuatana na Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na
Watoto Bi. Zainab Omar Mohamed (wa pili kushoto) na Katibu wa Wizara hiyo Bi. Asha Ali Abdalla (kulia)wakati alipowasili
katika viwanja vya Ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja leo
katika hafla ya sherehe ya kukabidhi Vihori kwa wakulima wa Mwani.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
akiangalia bidhaa mbali mbali zilizotengenezwa kwa kutumia zao la mwani
na kikundi
cha Ulezi ni Kazi cha shehia ya Fujoni Jimbo la Kitope, wakati wa
sherehe za kukabidhi Vihori kwa wakulima wa mwani hafla iliyofanyika leo
Ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja.
Baadhi ya Viongozi,Wananchi na wakulima wa mwani wakiwa katika sherehe za kukabidhi vihori kwa wakulima wa mwani zilizofanyika leo katika ukumbi wa Salama Bwawani Mjini Unguja ambapo mgeni rasmi akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Akinamama wakulima wa mwani kutoka sehemu tofauti za Unguja na Pemba wakiwa katika ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja katika sherehe za kukabidhi vihori kwa wakulima wa mwani kwa Mikoa ya Unguja na Pemba leo.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
akimkabidhi Kihori Bi. Zainab Daudi Haji mkulima wa mwani wa Uroa Wilya
ya Kati Mkoa wa Kusini wakati wa sherehe za kukabidhi vihori kwa
wakulima wa mwani zilizofanyika leo katika ukumbi wa Salama Bwawani Mjini Unguja.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
akimkabidhi Kihori Bw. Kombo Salim Hamadi mkulima wa mwani wa Tumbe
Magharibi Kaskazini Pemba wakati wa sherehe za kukabidhi vihori kwa
wakulima wa mwani zilizofanyika leo katika ukumbi wa Salama Bwawani Mjini Unguja.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
akitoa hutuba yake kwa wananchi wakati sherehe za kukabidhi Vihori kwa
wakulima wa mwani katika ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja
leo.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
akitoa hutuba yake kwa wananchi wakati sherehe za kukabidhi Vihori kwa
wakulima wa mwani katika ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja
leo.
Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
WIZARA ya Biashara Viwanda na Masoko, Wizara ya
Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na
Watoto zimeagizwa kufanya kazi kwa karibu na wakulima wa mwani ili kuhakikisha
kuwa bei wanayolipwa wakulima hao inalingana na nguvu na gharama wanazozitumia
sambamba na hali halisi ya bei ya bidhaa hiyo katika soko la nje.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa agizo hilo leo huko ukumbi wa Salama,
katika Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar mara baada ya kukabidhi vihori vya
kubebea mwani kwa wakulima wa mwani wa Unguja na Pemba.
Katika hotuba
yake Dk. Shein alisema kuwa ni wajibu wa Serikali kuwaunga mkono wananchi kwa
kuwajengea uwezo, ikiwemo kuwapatia masoko, mafunzo muhimu na fursa za mikopo
pamoja na kuongeza kasi katika kutafuta masoko mapya.
Dk. Shein alisema
kuwa dhamira ya Serikali ni kutaka kuona kuona kuwa wakulima wa zao la mwani
wanaongeza kiwango cha uzalishaji wa mwani na uwezo wao wa ubunifu katika
kutumia rasilimali zilizoizunguka Zanzibar, ili waweze kujikwamua kiuchumi na
kufikia malengo la Mpango wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupambana na Umasikini
Zanzibar awamu ya pili (MKUZA II).
Aidha, Dk. Shein
alieleza haja ya kufanywa utaalamu uliotumika hadi bei ya karafuu ikaongezeka
kufanywa pia, kwa upande wa bei ya zao la mwani huku akieleza kuwa Serikali
itaendeleza jitrihada zake za kuwanga mkono wakulima wa mazao mbali mbali na
kuhakikisha kuwa bei wanazolipwa kwa mazao yao inalingana na jitihada zao.
Dk. Shein
alihimiza kuwepo kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya
Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto na Taasisi ya Sayansi
na Teknolojia Tanzania (COSTECH) kwa ajili ya kufanya utafiti juu ya njia bora
za kuzalisha zao hilo ikiwa nji pamoja na kuwatafutia wakulima mbegu bora.
Pia, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kutoa nasaha zake kwa wale wote waliobahatika kupewa vihori
hivyo kuvifanyia kazi ipasavyo na kuvitunza huku akiahidi Serikali kuendelea
kutafuta njia zaidi za kuwasaidia wakulima wa mwani hapa nchini.
“ Vihori hivi vya
kisasa vitawapa nafuu wakulima wa mwani, hasa wanawake.. nafahamu jitihada za
kina mama katika uzalishjaji wa zao hili..matarajio yangu ni kuwa vihori hivi
vitasaidia kuondoa tatizo la ubebaji na vitatoa msukumo katika kuongeza kiwango
cha uzalishaji na hatimae muongeza kipato cha wakulima’,alisema Dk. Shein.
Kwa upande wa
utunzaji wa mazingira, Dk. Shein aliwataka wakulima wa mwani kukumbuka kuwa
wakidharau umuhimu wa kuyatunza mazingira wataweza kuathiri shughuli za uvuvi
na hata za utalii na kusisitiza kuwa kuweka safi mazingira ni jambo muhimu
sana.
Sambamba na hayo,
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza azma ya serikali katika kuimarisha sekta
ya uvuvi ambayo hapo siku za nyuma ilikuwa na mafanikio makubwa na hivi
karibuni kukabiliwa na changamoto na kusisitiza kuwa Serikali imeandaa Sera ya
Mkifugo na Uvuvi, ina mpango wa kuanzisha Kampuni ya uvuvi, kununua boti za maaluma
na za kisasa za uvuvi na kuanzisha kiwanda cha kusindika samaki hapa nchini.
Alisema kuwa
tayari Serikali imeshafanya mazungumzo na mwekezaji kutoka nje kwa ajili ya
kuwekeza kwenye sekta ya uvuvi kwa
kuanzia na rasilimali ziliopo nchini.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alieleza kuwa Serikali itasimamia ipasavyo mambo yote ya msingi
katika masuala yua uwezeshaji, ili kuona wakulima wa zao la mwani na mazao
mengine wanakua na kuondokana na changamoto zinazowakabili na kukuza kipato
chao.
Kabla ya hotuba
yake Dk. Shein alikabidhi vihori hivyo kwa vikundi vya Unguja na Pemba kwa
niaba ambapo mapema katika vuiwanja vya ukumbi huo alikagua maonyesho maalum
yaliohusisha bidhaa mbali mbali zilizotengenezwa kwa kutumia mwani zikiwemo
mafuta, sabubi za kukogea na kufulia pamoja na vyakula mbali mbali vinavyopikwa
kwa kutumia mwani na mazao mengine ya bahari.
Naye Waziri wa
Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bi Zainab
Omar Mohammed, alieleza mikakati iliyowekwa na Wizara yake katika kuhakikisha
zao hilo linapata mafanikio.
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bi Asha Ali Abdalla alisema kuwa moja ya
majukumu ya Wizara ni kusaidia uanzishwaji wa
makongano ya biashara, kama miongoni mwa mikakati ya kuwawezesha
wananchi kiuchumi.
Alisema kuwa wazo
la upatikanaji wa vihori hivyo linatokana na utafiti mdogo uliofanywa na
mfanyakazi wa kujitolea kutoka Shirika
la Kimataifa la Huduma za Kujitlea Bwana Hossein Chehrzade kwa kushirikiana na
wafanyakazi wa Idara ya Uratibu na Uendeshaji wa Programu za Uwezeshaji
Wananachi Kiuchumi, pamoja na Dk. Flower Msuya wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Bahari
Tanzania.
Katibu Asha
alisema kuwa jumla ya vihori 100 vimenunuliwa kwa kuazia na vitagawiwa Unguja
na Pemba kwa uwiano wa 30 kwa Unguja na 70 kwa Pemba ambapo jumla ya vikundi
vidogo vidogo 63 vya wakulima wa mwani na wakulima mmoja mmoja 14 watanufaika
na vihori hivyo.
Aidha, alisema
kuwa wanufaikaji wote wa mradi huo ni 448, kati ya hao 313 ni kutoka Pemba na
135 Unguja, wakiwemo wanawake 364 na wanaume 84 na kusisitiza kuwa vihori hivyo
vina uwezo wa kubeba kilo mia nne za
mwani mbichi kwa mara moja.
Alisema kuwa kwa
kutumia vihori hivi, uwezo wa wakulima wa kubeba mwani kupeleka ufukweni
utaongezeka kutoka kilo 50 hadi kilo 400, sawa na ongezeko la asilimia 87.5,
ongezeko ambalo linatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mwani hapa Zanzibar
sambamba na kuongeza kipato kwa wakulima wa zao hilo.
Nao wakulima wa
zao la mwani katika risala yao walieleza kuwa kutokana na upatikanaji wa vihori
hivyo wataweza kuongeza uzalishaji, kuokoa mwani mwingi ambao hubururwa na maji
na kukuza soko la mwani hapa Zanzibar.
Wakulima hao wa
mwani waliiomba Serikali kufanya kila liwezekanalo kuwapatia mambo yote ya
msingi yatakayopelekea kuimarika na kudumu kwa shughuli zao za mwani ikiwemo
kupandishiwa bei kwa zao hilo.
Sambamba na hayo
waliahidi kuvitunza vihori hivyo na kufuata masharti yote ambayo wamepewa ili
vihori hivyo viweze kudumu kwa muda mrefu na kuongeza uzalishaji wa mwani hapa
nchini.
Nao Wawakilishi
kutoka COSTECH pamoja na kutoka Shirika la Kimataifa la Huduma za Kujitolea
VSO, waliahidi kuendelea kuwaunga mkono wakulima wa zao hilo mwani hapa
Zanzibar ili liendelee kutoa ajira na kuongeza kipato cha wakulima na Taifa kwa
jumla.
Katika hafla hiyo
viongozi mbali mbali walihudhuria wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya,
viongozi wa Serikali na wananchi mbali mbali wakiwemo wakulima wa mwani kutoka
Unguja na Pemba ambapo pia, shughuli hiyo ilipmbwa kwa ngoma ya Kibatim utenzi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269