Breaking News

Your Ad Spot

Jun 12, 2015

KAMARA ACHUKUA KIJIJI YANGA

Baadhi ya mashabiki waliofika kwenye mazoezi ya Yanga Uwanja wa Karume jana wakimshangilia kiungo mpya wa timu raia wa Sierra Leone, Lansana Kamara.
KOCHA wa Yanga, Hans Pluijm, amevutiwa na ufiti wa mwili wa kiungo aliyeko kwenye majaribio, Msierra Leone Lansana Kamara, ingawa amesisitiza kwamba amebakiza hatua moja tu afuzu.
Lakini mchezaji huyo kwenye mazoezi ya jana Jumatano amefanya jambo ambalo mashabiki walilazimika kumzuia na kumjaza noti.
Kamara ambaye alianza mazoezi juzi Jumanne kwenye Uwanja wa Karume, ameteka akili za mashabiki wa Yanga kutokana na jitihada zake ambazo wamedai zimewazidi wachezaji wote ambao wapo mazoezini kwa sasa.

Katika mazoezi ya jana, mchezaji huyo alichukua kijiji baada ya kuwazidi kete wenzake kwenye mazoezi mengi kuanzia ya mbio, kupiga mashuti, mazoezi ya viungo mpaka pushapu. Pia alikusanya kijiji cha mashabiki mazoezini
Mwanaspoti lilishuhudia baadhi ya wachezaji maarufu wa Yanga wakimwambia apunguze mbio wakati wa mazoezi kwani alikuwa akiwaburuza jambo ambalo lingeweza kuwagombanisha na kocha kwa kudhani kwamba wanatega.
Ndipo mchezaji huyo akawa anafanya mdogomdogo ingawa bado alikuwa akiwaburuza na kufanya wengi wao waonekane hawako fiti.

Pluijm alivutiwa na jitihada za mchezaji huyo na kusisitiza kwamba mazoezini ameridhika naye lakini hawezi kufanya uamuzi wa mwisho mpaka ampe mechi moja kwani wachezaji walioko mazoezini Yanga kwa sasa ni wachache.

Mchezaji huyo amefanya uamuzi mgumu kwa taifa lake kwa kugoma kujiunga na timu ya taifa aliyoitwa kujiandaa na mechi dhidi ya Guinea ili amalizane kwanza na Yanga.

“Nimezungumza na kocha amenikubalia nimemwambia kama kutakuwa na mchezo mwingine nitajiunga na timu, lakini kwa sasa sitaweza kujiunga nao,” alisema.

Wachezaji ambao wameanza mazoezi Yanga ni mabeki Rajab Zahir, Pato Ngonyani, Kelvin Yondani, kipa Benedicto Tinocco, viungo Geofrey Mwashiuya, Said Makapu, Kamara na mshambuliaji Hussein Javu.

“Huwezi kupata kipimo kizuri hapa katika mazoezi, nafikiri tunatakiwa kuwa na subira kwanza nataka kumpa mechi moja ili nijue undani wa uwezo wake ndani ya kiwanja,”alisema Pluijm.

AJAZWA NOTI

Wakati Yanga wakimaliza mazoezi yao ya jana asubuhi kiliibuka kihoja kimoja kwa mashabiki wa timu hiyo ambao walilazimika kumzunguka kiungo huyo na kuanza kumchangishia fedha za kula bata baada ya kuridhishwa na kazi yake.

Mashabiki hao ambao walimshtua kiungo huyo

walilazimika kuchukua mfuko wa plastiki wa kuhifadhia maji ya kunywa na kuanza kujichangisha fedha ambapo kila kiungo huyo alipotaka kuondoka walimzuia wakitaka asubiri fedha hizo.

Baada ya kumaliza zoezi hilo mashabiki hao waliendelea kumsindikiza Kamara mpaka katika gari ndogo ya meneja wake Gibby Kalule alilolitumia kuondoka katika eneo hilo.

“Sikuwa nawaelewa kwanini wamenipa fedha huku pia wakinizuia kuondoka, nimefurahi sana kuona hili walilofanya watu wa hapa wanapenda sana mpira,”alisema Kamara.

SIMBA WASHTUKA

Katika mazoezi hayo ya Yanga, mashabiki wa Simba waliohudhuria walionekana kushtushwa na umbo la kipa Tinocco ambaye ni mrefu kuliko wachezaji wote wa Yanga na Simba.

Mashabiki hao wa Msimbazi walisikika wakidai kwamba kipa huyo huenda akaibua changamoto kubwa kwa makipa nchini na akawa bora kuliko hata waliopo sasa licha ya kwamba ni kijana.

Lakini habari za ndani ya Yanga ni kwamba mchezaji huyo ngongoti bado hajalivutia benchi la ufundi na linafikiria kumpa muda zaidi licha ya kwamba umbo lake linawachengua mpaka mashabiki wao ambao wamekuwa wakikejeli kwamba ni mrefu kuliko lango lenyewe.

Chanzo:Mwanspoti mtandaoni

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages