………………………………………………..
Serikali iliandaa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana mnamo
mwaka 1996; Utekelezaji wa Sera hii umekabiliwa na changamoto mbalimbali
za kitaifa na za kidunia.
Katika milenia hii ya Sayansi na teknolojia, vijana wa kiume na
kike ni rasilimali kubwa zaidi kwa sasa na siku za baadaye; wanatoa
msukumo wa kuleta mageuzi ya kijamii, kiuchumi na kisiasa katika sayari
hii yenye mabadiliko ya haraka duniani.
Mazingira ya dunia, kijamii, kiuchumi na kisiasa yameathiri hali
ya vijana nchini Tanzania, Uhamiaji wa vijana kutoka maeneo ya vijijini
kwenda mijini umeongeza mzigo wa huduma za Umma mijini na miundombinu
ya kijamii hivyo kuleta ukuaji wa haraka wa sekta isiyo rasmi na
ongezeko la matukio ya ajira mbaya kwa vijana.
Vijana wengi nchini wanafanya kazi kwenye sekta za kilimo,
uvuvi, madini, ufugaji wa wanyama na viwanda vidogovidogo kama vya
useremala, sonara, biashara ndogondogo za kuuza nguo za mitumba, matunda
na vyakula vya aina mbalimbali.
Pamoja na ukweli kwamba vijana hawa wamejiajiri lakini bado
wanakumbana na matatizo mengi katika kutekeleza shughuli zao; matatizo
hayo ni pamoja na ukosefu wa mtaji wa kufanyia kazi, vifaa na ujuzi wa
kiufundi au stadi muhimu za maisha.
Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 1996 imewezesha
utekelezaji wa program mbalimbali za maendeleo ya vijana ambazo ni
pamoja na stadi za kujenga uzoefu kwa ajili ya uwezeshaji wa kiuchumi,
maadili mema, mwenendo na utendaji bora, ushiriki wa vijana na utoaji wa
huduma rafiki kwa vijana.
Hata hivyo Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007
inalenga masuala ya maendeleo ya vijana katika uwezeshaji wa kiuchumi,
mazingira, ukuzaji wa ajira, ushiriki wa vijana katika masuala
mbalimbali kwenye jamii, VVU na UKIMWI, jinsia, Sanaa na utamaduni,
michezo, afya ya uzazi kwa vijana na masuala ya maisha ya familia.
Katika kutekeleza Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka
2007 Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imejizatiti kutoa
elimu ya uhamasishaji, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, ujuzi, na stadi za
maisha kwa vijana wote nchini kwa kukutana na vijana katika kila
Halmashauri na kutoa elimu inayowasaidia vijana kujitambua hivyo kutumia
fursa mbalimbali walizonazo kujiendeleza.
Kwa kuanzia Vijana kutoka Halmashauri za Mkoa wa Mbeya,
Dodoma,Kilimanjaro, Singida, Kigoma, Manyara, Arusha na Mara wamefikiwa
na Wizara ya habari, Vijana, Utamaduni na Michezo katika harakati za
kuwakomboa vijana kifikra na kiuchumi ili kuondokana na kundi la vijana
lisilokuwa na mwelekeo katika jamii.
Wizara inaendelea kuhamasisha vijana kujiunga katika vikundi vya
uzalishajimali, kusajili vikundi hivyo na hatimaye vikundi hivyo
kujiunga katika SACCOS za vijana zilizoanzishwa, ikizingatiwa kuwa hii
ni mojawapo ya kigezo muhimu cha kikundi kuweza kupewa Mkopo kupitia
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Mfuko wa Maendeleo ya vijana una changamoto mbalimbali zikiwemo:
Fedha zinazotengwa kwa ajili ya Mfuko kuwa kidogo ukilinganisha na
mahitaji ya Vijana, Vijana wengi kutokuwa na mwamko wa kurejesha fedha
kwa wakati, Maandiko ya Miradi mingi inayowasilishwa kutokidhi vigezo
ili kuweza kukopesheka.
Fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ni kwa ajili ya Vijana
wote nchini, kila kijana anayo haki ya kunufaika na Mkopo kutoka katika
Mfuko huu. Vijana wanatakiwa kukopa na kurejesha na siyo kama wengine
wanavyohusisha fedha hizi na masuala ya kisiasa wakidhani ni takrima.
Pia, wanatakiwa kuzingatia masharti/ vigezo vilivyopo katika mwongozo wa
Mfuko pindi wanapoandaa Maandiko ya Miradi yao.
Serikali imelenga kuendelea kuboresha Mfuko huu ili kuwa na
fedha za kutosha na kuweza kuwafikia vijana wengi nchini, hii itasaidia
vijana wengi kujiajiri wao wenyewe na kutengeneza ajira kwa vijana
wengine.
Katika kutekeleza azma ya kusaidia Vijana, jumla ya shilingi
Bilioni 6 zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili
ya kusaidia mfuko wa Maendeleo ya Vijana, ambapo Vijana kutoka
Halmashauri mbalimbali nchini wamepatiwa mikopo yenye unafuu, riba
kidogo na upatikanaji wake ukiwa ni wa urahisi.
Mfuko huu ulianzishwa mwaka 1993,
chini ya kifungu namba 17(1) cha The Exchequer and Audit Ordinance (Cap
439) No 21 of 1961, lengo likiwa ni kuwasaidia vijana ili wapate mikopo
yenye masharti nafuu.
Katika ziara yake ya kukagua
miradi ya vikundi vya Vijana wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi hivi
karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Vijana, Utamaduni na Michezo
Bi. Sihaba Nkinga amewashauri vijana kuchangamkia fursa hiyo ambayo
haimuhitaji mkopaji kuwa na dhamana isiyo hamishika bali kuwa na
uaminifu wa kurejesha mkopo huo utakaotolewa kupitia vyama vya kuweka na
kukopa SACCOS.
“Vijana wanatakiwa kuhamasishwa
kuunda na kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali na kuunda SACCOS
za vijana ili waweze kupatiwa mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya
Vijana kwa ajili ya kuongeza mitaji na kupanua uzalishaji”. Anasema Bi.
Nkinga.
Afisa Maendeleo ya Vijana
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bibi. Subira Mfanga anabainisha kuwa
vijana nchini wanahitaji elimu ya ziada kubadilisha fikra zao kwani kwa
kufanya hivyo itawasaidia vijana kutambua kuwa fursa za ajira
zinasababishwa na wao wenyewe kwa kuwa waaminifu, kuchukua mkopo
unaotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na kurudisha mkopo huo kwa
wakati ili kuweza kutoa fursa kwa vijana wengine kufikiwa na mkopo huo.
Bibi Mfanga anaongezea kuwa zoezi
lililofanywa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuwafikia
vijana wa Halmashauri ya Mwanga ni lulu kwa vijana wa Wilaya hiyo kwani
limewasaidia vijana kujielewa hivyo kuacha kutumika vibaya katika
makundi yanayoleta uhasama ndani ya jamii bali wajikite zaidi katika
uwekezaji kwa kuanzisha miradi endelevu, yauhakika na inayotekelezeka.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Deogratius Yenza amesema
kuwa viongozi wa Mkoa wa Dodoma wako bega kwa bega na Vijana wa Mkoa huo
kwani vijana ndio sehemu kubwa ya nguvu kazi ya Taifa wanahitaji
kujengewa ujuzi, kushauriwa, na kufanyiwa tathmini ya miradi wanayoombea
mikopo ili iweze kuleta tija na hamasa kwa vijana wengine kuiga mfano
wa vijana wa Dodoma.
Aidha Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo Vijana Bi. Venerose
Mtenga amesema kuwa walengwa wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ni vijana
wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 watakaoruhusiwa kuomba mkopo na
kurejesha mikopo hiyo kwa kipindi cha miaka miwili ambapo muda wa
maandalizi utakuwa wa miezi mitatu tu na riba yake itakua asilimia kumi
(10%) kwa mwaka ambapo kikundi kitalazimika kulipa tozo ya asilimia 15
iwapo kitashindwa kurejesha mkopo katika muda uliopangwa.
Akifafanua jambo wakati wa semina ya kuhamasisha vijana wa Mkoa
wa Mbeya Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Mbeya Bw. George Mbijima
amewataka vijana kutambua yakua miradi itakayopewa mikopo kupitia Mfuko
wa Maendeleo ya Vijana itaibuliwa na vikundi vya vijana wenyewe na
andiko la miradi litawasilishwa kwa Afisa Maendeleo ya vijana wa
Halmashauri husika ambapo ataitembelea miradi hiyo iliyowasilishwa kwake
ili kuthibitisha uhai wake na uwezo wa miradi kurejesha mkopo na
kuwasilisha miradi hiyo kwa Afisa wa Mkoa ambaye baada ya kuipitia
ataituma Wizarani kwa hatua zaidi.
Hata hivyo, vijana waliopata
nafasi kushiriki semina mbalimbali zilizotolewa na Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo wameiomba Serikali kupitia Idara ya
Maendeleo ya Vijana kuhakikisha kuwa mafunzo hayo yanakuwa endelevu na
yanawafikia vijana nchini kote ili kuwawezesha vijana kufahamu umuhimu
wa Mfuko huo, upatikanaji wa fedha, pamoja na sifa za upatikanaji wa
fedha kutoka mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Jitihada zote hizo zinalenga
katika kufikia malengo na mikakati mbalimbali ya kukuza ajira kwa Vijana
nchini kama zilivyoainishwa kwenye Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka
2007, Sera ya Ajira ya mwaka 2008, Mpango Kazi wa Taifa wa Ajira kwa
Vijana wa mwaka 2007, MKUKUTA II na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka
2025.
Tanzania kama sehemu ya dunia
inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana walioko katika
mazingira hatarishi pamoja na umuhimu wa kuhakikisha kuwa vijana
wanahusishwa kikamilifu katika malengo ya maendeleo kama Taifa la kesho.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269