CHAMA cha
soka mkoa wa Dar es salaam, DRFA kwa kushirikiana na shirikisho la soka
nchini TFF,leo imezindua rasmi kozi ya ukocha wa leseni C’
inayotambuliwa na shirikisho la kandanda barani afrika CAF.
Kozi hiyo
ya wiki mbili inaendeshwa na mkufunzi, Salum Madadi ambaye ni
mkurugenzi wa ufundi wa TFF,ikiwa na jumla ya washiriki 31 wengi wao
wakiwemo makocha wa vilabu vya ligi daraja la pili,daraja la kwanza na
ligi kuu.
Miongoni
mwa washiriki hao ni pamoja na kocha msaidizi wa Simba,Suleiman
Matola,katibu mkuu wa zamani wa Simba Muhina Kaduguda,kocha wa Ruvu
shooting Tom Olaba,kocha wa makipa wa Yanga Juma Pondamali,nyota wa
zamani wa Taifa Stars, Ally Mayai na Peter Tino.
Mgeni
rasmi katika ufunguzi wa kozi hiyo ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya
TFF,Msafiri Mgoy,ambaye amewapongeza washiriki kwa uamuzi wao wa kutaka
kujiongezea maarifa ya ufundishaji wa soka ,kwa kuwa tanzania
inakabiliwa na upungufu mkubwa wa makocha ikilinganishwa na mataifa
mengine ya Afrika ambayo yamepiga hatua kisoka.
Aidha
amesema TFF imeweka mpango maalum wa kutunza kumbukumbu za makocha hao
na wengine watakaopatikana,pamoja na kufuatilia kazi zao kwenye vilabu
mbalimbali watakavyofundisha ili iwe rahisi kuwatengenezea mazingira
mazuri ya kufanya kazi zao.
Naye
mwenyekiti wa DRFA,Almasi Kasongo wakati akimkaribisha mgeni
rasmi,amesema chama chake kinataraji pia kuendesha kozi za madaktari
pamoja na kuendeleza mpango wake wa kuinua soka la vijana,ili taifa liwe
na wachezaji wenye uwezo wa kushindana na mataifa mengine.
Kasongo
amesema licha ya chama chake kuwa na mikakati ya kuhakikisha soka la
mkoa wa Dar es salaam na nchi kwa ujumla linanyanyuka,lakini bado nguvu
kumbwa inahitajika kutoka TFF pamoja na wadau wenye mapenzi mema na
mpira wa nchi hii.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI NA MAWASILIANO YA DRFA,
Omary Katanga,
Mkuu wa habari na mawasiliano DRFA.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269