Breaking News

Your Ad Spot

Mar 19, 2016

JUMAMOSI 9 MFUNGUO TISA JAMADI THANI 1437 HIJRIA

Jumamosi 9 Mfunguo Tisa Jamadi Thani 1437 Hijria
Leo ni Jumamosi tarehe 9 Mfunguo Tisa Jamadi Thani 1437 Hijria sawa na tarehe 19 Machi 2016 Miladia.
Miaka 52 iliyopita katika siku kama ya leo, Imam Khomeini mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa hotuba na kuwataka wananchi wa Iran wasifanye sherehe za Nairuzi za mwaka mpya wa Kiirani wa 1342 ili kulalamikia hatua zisizo za kisheria za utawala wa kifalme wa Kipahlavi. Nairuzi ni sherehe za kitaifa za Wairani ambazo hufanywa kila mwanzoni mwa mwaka wa Kiirani. Katika kipindi chote cha mwaka 1341 Hijria Shamsia utawala wa kidikteta wa Shah ulichukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha misingi ya utawala wake na kwa ajili ya kuyaridhisha madola ya kigeni hususan Marekani. Imam Khomeini kwa uono mpana na kutazama mustakbali wa mambo akiwa pamoja na maulama wengine aliitangaza sikukuu ya Nairuzi kuwa mambolezo ya umma ili kubatilisha propaganda za utawala wa Kipahlavi za kuhalalisha hatua zake za hiana. Kwa muktadha huo, wananchi na viongozi wa kidini walifanya vikao vya maombolezo katika pembe mbalimbali za Iran. Ubunifu huu wa Imam Khomeini ulikuwa na taathira kubwa kiasi kwamba, katika siku ya pili ya sikukuu ya Nairuzi maafisa wa utawala wa Shah walishambulia mkusanyiko wa matalaba (wanafunzi wa masomo ya dini) katika mji wa Qum waliokuwa wakifanya maombolezo na kuwauwa shahidi na kuwajeruhi baadhi yao.
Siku kama ya leo miaka 133 iliyopita, alizaliwa Sir Norman Haworth, mtaalamu wa kemia wa Uingereza. Sir Haworth alifanya utafiti na uhakiki mwingi wa kisayansi kuhusu haidrokaboni na akafanikiwa kubuni mpango mpya kwa ajili ya muundo wa molekuli ya sukari. Vilevile Sir Haworth alifanya utafiti na majaribio kuhusu vitamini C ambayo muundo wa molekuli yake unashabihiana na sukari na akatayarisha aina yake ya kutengenezwa viwandani kwa jina la asidi askobiki. Mwaka 1937 Sir Norman Haworth alitunukiwa tuzo ya kemia ya Nobel kutokana na uhakiki na utafiti wake mkubwa. Sir Haworth alifariki dunia mwaka 1950.
Na siku kama ya leo miaka 29 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Machi 1987 alifariki dunia Louis de Broglie, ambaye alikuwa wa mwisho katika kizazi cha waasisi wa fizikia ya kisasa akiwa na umri wa miaka 95. Louis de Broglie alizaliwa mwaka 1892 na baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia alianza utafiti wa elimu ya fizikia. Mtaalamu huyo wa fizikia wa Ufaransa alitatua masuala mengi ya elimu hiyo kwa nadharia yake mashuhuri ya Wave Particle Duality. Mwaka 1929 alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages