Breaking News

Your Ad Spot

Mar 1, 2016

'MZOZO BURUNDI UPEWE KIPAUMBELE MKUTANO WA EAC'

'Mzozo Burundi upewe kipaumbele mkutano wa EAC'
Huku marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC wakitazamiwa kukutana mjini Arusha Tanzania kesho Jumatano, mashirika ya kijamii na asasi za kiraia zipatazo 17 za kanda hiyo zimetoa wito wa kupewa kipaumbele mgogoro wa kisiasa wa Burundi katika mkutano huo.
Taarifa ya pamoja ya asasi hizo za kiraia iliyotolewa jana mjini Arusha Tanzania imesema kuwa: “Tumesikitishwa mno na habari kwamba kadhia ya Burundi haiko katika ajenda ya mkutano wa kawaida wa 17 wa jumuiya ya EAC huko Arusha, licha ya hali ya kisiasa na kiusalama katika nchi hiyo kuzidi kuwa mbaya.”
Makundi hayo ya kiraia ya kanda ya Afrika Mashariki yamewataka viongozi wa EAC kubuni mfumo mwafaka wa kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Burundi, kama ilivyopendekezwa na Bunge la Afrika Mashariki EALA mwezi Novemba mwaka jana. Kadhalika taarifa hiyo imetoa wito wa kujumuishwa pande zote katika mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mzozo huo, wakiwemo wanasiasa wa upinzani na wa chama tawala CNDD-FDD waliokimbia nchi; na kwamba mazungumzo yenyewe yafanyike kila siku hadi mwafaka upatikane.
Hii ni katika hali ambayo, ujumbe wa Umoja wa Afrika ulioitembelea Burundi hivi karibuni ulitangaza kuwa, utatuma nchini Burundi waangalizi 100 wa haki za kibinaadamu pamoja na waangalizi wengine 100 wa kijeshi. Burundi ilitumbikia katika machafuko ya ndani mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka jana baada ya kiongozi wa sasa wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kutangaza nia yake ya kugombea nafasi hiyo kwa mara ya tatu mfululizo.
Hadi sasa mamia ya watu wameuawa katika machafuko hayo na maelfu ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages