Rais Mstaafu Jakaya Kikwete katika mahojiano na Ndugu Amarildo Da Conceiacao kutoka Taasisi ya DKt. Agostinho Neto, Mpigania Uhuru na Rais wa Kwanza wa Angola jijini Dar es Salaam jana |
Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete ametembelewa na ujumbe kutoka Taasisi ya Dkt. Agostinho Neto ya Angola jana jijini Dar es Salaam.
Ujumbe wa Taasisi hiyo unaoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Amarildo Da Conceicao uko nchini kwa lengo la kufanya mahojiano na viongozi wa Tanzania kwa lengo la kuhifadhi historia ya mpigania uhuru na muasisi wa Taifa la Angola Dkt. Agostinho Neto.
Akimuelezea Dkt. Agostinho Neto, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete amemzungumzia mpigania uhuru huyo kuwa mtu mwenye kuzungumza kwa sauti ya upole lakini kiongozi makini, shupavu na mwenye uwezo mkubwa wa kifalsafa na kifikra. Dkt. Kikwete amesema anakumbuka akiwa kiongozi wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, walimualika Dkt. Neto kuja kuzungumza na wanafunzi katika Darasa la Itikadi alipozuru nchini mwaka 1974.
Mpigania uhuru huyo aliyembatana na mkewe mwenye asili ya kireno aliulizwa swali na mwanafunzi mmoja, 'iweje yeye ni mpigania uhuru dhidi ya watu weupe ilihali ameoa mwanamke mweupe?'. Katika jibu lake, Dkt. Neto alisema, 'mapambano hayana rangi, hatupambani na watu weupe tunapambana na ukoloni, mtu mweupe anaweza kuungana nasi katika mapambano yetu hali kdhalika wapo wenzetu weusi wanaoungana na kusaidia wakolini dhidi yetu'.
Rais Mstaafu amewapongeza Taasisi ya Agostinho Neto kwa jitihada inazochukua za kuhifadhi historia ya mpigania uhuru na muasisi wa Taifa la Angola. Amewakumbusha umuhimu wa kuhakikisha kuwa historia hiyo inarithishwa kwa kizazi baada ya kizazi ili watambue tulipotoka, tulipo na tunapotakiwa kwenda.
Ujumbe wa Taasisi ya Neto pia umefanya mahojiano kama hayo na Mama Maria Nyerere, Mke wa Baba wa Taifa, Mheshimiwa Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu Mstaafu na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Nchi za Kiafrika (OAU) na viongozi na watanzania mashuhuri ambao walishiriki kwa namna moja au nyingine katika harakati za uhuru wa Angola.
Imetolewa na Ofisi ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne,
Dar es Salaam
2Aprili, 2016
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269