Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango akionyesha mkoba wenye bajeti ya serikali kwenye viwanja vya bunge mjini Dodoma, Juni 8, 2016. Jumla ya shilingi Trilioni 29.5 zimetengwa katika bajeti hiyo. (Picha na Ofisi a Waziri Mkuu)
Wabunge wa upinzani wakitoka bungeni
ikiwa ni muendelezo wa kupinga Naibu Spika kuongoza vikao vya bunge
mjini Dodoma leo Juni 8, 2016 wakati waziri wa fedha na mipango, Dkt.
Philip Mpango, alipowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti
ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Waziri Dkt. Mpango akisoma bajeti hiyo jioni hii.
1. Mheshpika, naomba
kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17. Pamoja na
hotuba hii, ninawasilisha vitabu vinne vinavyoelezekina makadirio ya Bajeti.
Kitabu cha Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu chaPili ni
Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea,
Taasisi na Wakala za Serikali; Kitabu chaTatu ni Makadirio ya Matumizi ya
Kawaida kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni
Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa Wizara, Idara za Serikali
zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka
2016 pamoja na Muswada wa Sheria ya kuidhinisha matumizi ya Serikali wa mwaka
2016 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.
2. Mheshimiwa
Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa baraka na
amani anayoendelea kuijalia nchi yetu na pia kwa kuniruhusu kusimama hapa mbele
ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa
mwaka 2016/17. Aidha, kwa namna ya pekee nachukua fursa hii kumpongeza
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais
na mwanamama wa kwanza kushika nafasi hiyo katika historia ya nchi yetu.
Nampongeza pia Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kuchaguliwa tena kuwa
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, nampongeza Mheshimiwa
Kassim M. Majaliwa kwa kuchaguliwa na wananchi wa jimbo la Ruangwa kuwa Mbunge
wao na kuteuliwa na Mhe. Rais na kuthibitishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda pia kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika
pamoja na Naibu Spika kwa kuchaguliwa kuongoza Bunge letu Tukufu.
Kadhalika, natumia fursa hii kumpongeza Mhe. Mohamed Othman Chande, Jaji Mkuu
wa Tanzania, kwa kuongoza mhimili wa Mahakama kwa weledi mkubwa.
3. Mheshimiwa
Spika, niruhusu pia niwashukuru sana waheshimiwa wenza wa viongozi wetu
wa kitaifa: Mama Janet Magufuli, Bwana Ameir Hafidh Ameir (mume wa Mhe. Makamu
wa Rais), Mama Mwanamwema Shein, Mama Mary Majaliwa, Mama Fatuma Ramadhani
Mganga (mke wa Mhe. Spika), Bwana James Andilile (mume wa Mhe. Naibu Spika) na
Mama Saada El-Maamry Othman (mke wa Mhe. Jaji Mkuu) kwa kuwasaidia na kuwatunza
viongozi wetu vizuri. Asante kwenu wote na Mungu awabariki.
4. Mheshimiwa
Spika, kwa mara nyingine natoa shukrani za pekee kwa Mhe. Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua
kuwa Mbunge na Waziri wa Fedha na Mipango. Ninatambua kwamba wananchi wa
Tanzania wananidai! Tarehe 29 Februari, 1968 Baba wa Taifa hayati Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere aliwasilisha hati ya madai kama ifuatavyo, nanukuu: “Tunadai
nini basi kwa wale wenzetu waliojaliwa kupata elimu? Tunadai huduma kwa
wananchi na huduma ambayo ukubwa wake utalingana na kiasi cha elimu waliyoipata”
mwisho wa kunukuu. Hivyo, napenda kumuahidi tena Mhe. Rais na Watanzania kwamba
nitaibeba dhamana hii kwa bidii na uadilifu ili kulipa deni langu kwa nchi
yangu. Vilevile, nawapongeza waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa kwenu na
kuwa sehemu ya Bunge hili. Napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri
wenzangu na Naibu Mawaziri kwa dhamana kubwa tuliyopewa na Mheshimiwa Rais
kuwatumikia Watanzania. Nampongeza pia Dkt. Thomas Kashililah, Katibu wa Bunge
na Bw. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama kwa kuratibu vyema shughuli
za Bunge na Mahakama kwa mtiririko huo. Napenda pia kumpongeza Prof. Mussa
Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kazi nzuri
anayoifanya ya kukagua na kutoa taarifa za matumizi ya fedha za umma kwa
wakati.
5. Mheshimiwa
Spika, ninaishukuru sana Kamati ya Bunge ya Bajeti chini ya
uenyekiti wake Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara vijijini na
Makamu Mwenyekiti Mhe. Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kwa
kuchambua kwa kina bajeti za Mafungu yote na kutoa mapendekezo na ushauri.
Aidha, napenda kuwashukuru wenyeviti wa kamati za kisekta kwa ushauri na
mapendekezo waliyotoa wakati wakichambua rasimu ya Bajeti hii. Ninamshukuru pia
Mhe. George Mcheche Masaju (Mb), Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha
kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016 na Muswada wa Sheria ya
Matumizi wa mwaka 2016 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.
6. Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mhe.
Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji, Mbunge wa Jimbo la Kondoa kwa kuteuliwa kuwa
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na pia ninamshukuru kwa ushirikiano
anaonipatia katika utekelezaji wa majukumu yangu. Aidha, napenda kumshukuru
Dkt. Servacius B. Likwelile, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango kwa
uratibu na usimamizi mzuri wa maandalizi ya Bajeti hii. Kadhalika, nawashukuru
Naibu Makatibu Wakuu; Gavana wa Benki Kuu; Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania; Msajili wa Hazina; Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu;
Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara; Wakuu wa idara, vitengo na Watumishi
wote wa Wizara na taasisi zake kwa kazi kubwa waliyoifanya kukamilisha Bajeti
hii.
7. Mheshimiwa Spika, Bajeti hii imezingatia mawazo na
mapendekezo ya wadau mbali mbali wakiwemo wenye viwanda, wafanyabiashara na
wengine wengi. Nawashukuru wote kwa mawazo na ushauri wao. Kipekee niwashukuru
wajumbe wa kamati ya wataalamu na ushauri wa masuala ya kodi (Task Force) na
kamati ya kitaifa ya ushauri wa kodi (Think Tank) kwa ushauri wao mzuri
walionipa.
8. Mheshimiwa Spika, kwa kukamilisha shukrani hizi,
napenda kutoa shukrani maalum kwanza kwa Prof. Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu
ya Tanzania, mwalimu wangu na mfano bora wa maisha yangu kikazi. Amenilea
kitaaluma na kikazi tangu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Benki ya Dunia, na
ameendelea kunishauri katika utumishi wangu Serikalini. Ninamshukuru sana kwa
uzalendo na unyenyekevu wake na ninamtakia kheri na afya njema yeye na familia
yake. Pia ninapenda kutoa shukrani maalum kwa rafiki yangu mpenzi, mke wangu
Mbonimpaye kwa kunitunza vizuri, lakini hasa kwa kuniombea msaada wa Mungu siku
zote akishirikiana na watoto wetu, wanafamilia wengine na marafiki zetu.
Asanteni na Amani iwe kwenu! Aidha nawashukuru viongozi wa dini mbalimbali na
watanzania wote ambao waliitikia rai ya Rais wetu Mhe. Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli kumuombea na wanatuombea sana na sisi wasaidizi wake ili
tujitoe na kuwatumikia watanzania, na hasa maskini, kwa bidii na
unyenyekevu. Mungu awabariki! Kadhalika, nawashukuru sana wananchi wa
kijiji cha Kasumo, wilaya ya Buhigwe nilikozaliwa, pamoja na wananchi wa Kasulu
na mkoa wa Kigoma kwa ujumla. Asanteni kwa kunilea na kwa mapenzi yenu mema.
9. Mheshimiwa
Spika, hotuba hii inawasilisha Bajeti ya kwanza ya Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yenye kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”.
Serikali inaleta Bajeti hii kwa dhamira ya kweli ya kutekeleza ahadi zake
zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 – 2020, Mpango wa Pili wa
Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025
ili kukidhi kiu na matarajio ya Watanzania. Malengo makuu ya kiuchumi ya Bajeti
hii ni mawili.Kwanza ni kutatua matatizo yanayowakabili wananchi ili
kuleta matumaini mapya ya maisha mazuri zaidi kwa wananchi wetu, hasa wa kipato
cha chini. Lengo hili litahusisha kufanya mabadiliko makubwa katika utendaji wa
Serikali, hususan kurejesha nidhamu ya kazi na uwajibikaji, na kuondokana na
ufanyaji kazi kwa mazoea, pia kuimarisha uadilifu na usimamizi wa matumizi ya
mali za umma na rasilimali za Taifa. Pili ni kujenga uchumi wa kipato
cha kati kiuhalisia kwa kusimamia kwa umakini utulivu wa uchumi na uendelezaji
wa viwanda vitakavyoongeza ajira hasa kwa vijana wetu nchini na kuongeza tija
kwenye kilimo ili kuongeza kipato katika sekta hii inayotegemewa na wananchi
wengi.
10. Mheshimiwa
Spika, wakati Mheshimiwa Rais akifungua Bunge hili tarehe 20 Novemba
2015, alibainisha maeneo yanayolalamikiwa sana na wananchi, na kuelekeza
Wizara, Ofisi na Taasisi husika zijipange ipasavyo kutatua malalamiko hayo kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali. Naomba niyarejee kwa kifupi. Kwanza ni rushwa
katika maeneo yote ya utoaji huduma kwa wananchi; Pili, ni upotevu wa mapato,
ujangili, wizi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha, uzembe na urasimu katika
maeneo mbalimbali; eneo la tatu ni huduma zisizoridhisha za upatikanaji wa
maji, elimu bora na afya; eneo la nne ni migogoro ya ardhi kati ya wakulima na
wafugaji, vijiji na hifadhi, wananchi na wawekezaji, wananchi na wamiliki wa
mashamba pori na uvunjaji wa sheria za ardhi.
11. Mheshimiwa
Spika, eneo la tano ni huduma zisizoridhisha za usafiri na usafirishaji
kutokana na uchakavu wa miundombinu ya reli, barabara, usafiri wa majini; na
udhaifu mkubwa wa shirika la ndege. Eneo la sita ni upungufu katika utoaji haki
ikiwa ni pamoja na mlundikano wa kesi mahakamani, wananchi kubambikiwa kesi na
polisi, makazi duni na ukosefu wa vitendea kazi kwa askari; eneo la saba ni
kodi na tozo za kero kwenye mazao, uhaba wa zana na pembejeo za kilimo, mifugo
na uvuvi, uhaba wa masoko ya uhakika, maghala, maafisa ugani na huduma za
ugani, na uvuvi haramu; na eneo la nane ni uwezeshaji mdogo kwa makundi maalum
hususan wazee, walemavu, wanawake, watoto, vijana, wafanyakazi, wasanii, wanamichezo,
wachimbaji wadogo na watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
12. Mheshimiwa
Spika, baada ya rejea hiyo, naomba niseme tena kwamba mkazo mkuu wa
Bajeti hii ni kutekeleza azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kutatua kero za
wananchi. Aidha, Serikali itatekeleza azma ya kuendeleza viwanda ambavyo ndiyo
msingi wa uchumi endelevu utakaowezesha Taifa letu kufikia hadhi ya kipato cha
kati na hali bora ya maisha ya wananchi walio wengi ifikapo mwaka 2025.
13. Mheshimiwa
Spika, Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17 inalenga kuimarisha
miundombinu ya msingi kama vile ya maji, umeme na usafirishaji kwa ajili ya
kuhakikisha maendeleo ya viwanda nchini na vile vile kuongeza uzalishaji wa
mazao ya kilimo yanayotumika kama malighafi viwandani. Ili kufanikisha hilo,
mkazo mkubwa utawekwa kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na ugawaji wa
rasilimali hizo katika maeneo muhimu ya kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya
viwanda. Jitihada kubwa zitaelekezwa katika kuziba mianya ya ukwepaji kodi, kuibua
vyanzo vipya vya mapato, na kuhimiza matumizi ya mashine za kielektroniki
- EFDs ili kuongeza makusanyo na vile vile kudhibiti matumizi
yasiyokuwa na tija. Hivyo, kauli mbiu ya Bajeti za nchi wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki kwa mwaka 2016/17 ni “kuongeza uzalishaji viwandani ili
kupanua fursa za ajira”(Industrial growth for job creation). Kwa msingi
huo, Bajeti ya maendeleo kwa mwaka 2016/17 imeongezwa kwa kiasi kikubwa na
kufikia asilimia 40 ya bajeti yote tofauti na miaka yote ya nyuma ambapo ilikuwa
wastani wa asilimia 25. Bajeti hii pia inalenga kujenga mazingira mazuri ya
kufanya biashara na kuwekeza ili kuvutia ushiriki wa wawekezaji wa ndani na nje
katika kuendeleza viwanda na kilimo.
II. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA
MWAKA 2015/16
14. Mheshimiwa
Spika, mpango na bajeti ya Serikali mwaka 2015/16 ililenga
kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 22.49 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na
nje. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 13.99 zilikuwa ni makadirio ya
mapato ya ndani zikijumuisha mapato ya Halmashauri; shilingi trilioni 2.32 ni
mikopo nafuu na misaada kutoka kwa Washirika wa Maendeleo; shilingi trilioni
4.03 ni mikopo ya kibiashara ya ndani; na shilingi trilioni 2.14 ni mikopo ya
kibiashara ya nje. Aidha, kiasi cha shilingi trilioni 16.57 kilipangwa kutumika
kwenye matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 5.92 kwenye matumizi ya
maendeleo.
Mapato
15. Mheshimiwa Spika,
katika kuhakikisha mapato ya ndani yanapatikana, sera za mapato za mwaka
2015/16 zililenga kupunguza misamaha ya kodi isiyokuwa na tija; kuongeza
matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato; na kuongeza
wigo wa mapato. Sera
hizo zililenga kukusanya mapato ya kodi ya shilingi trilioni 12.36, mapato
yasiyo ya kodi ya shilingi trilioni 1.11 na mapato yanayotokana na vyanzo vya
Halmashauri shilingi bilioni 521.9.
16. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2015
hadi Aprili 2016, jumla ya makusanyo ya ndani (ikijumuisha mapato ya
Halmashauri) yalikuwa shilingi trilioni 11.48 sawa na asilimia 99 ya makadirio
ya kukusanya shilingi trilioni 11.55 katika kipindi hicho. Mapato
ya kodi yalikuwa shilingi trilioni 10.17, sawa na asilimia 100 ya lengo, mapato
yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 967.2 sawa na asilimia 105 ya lengo na
mapato yaliyokusanywa na Halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 344.1, sawa na
asilimia 79 ya makadirio kwa kipindi hicho.
17. Mheshimiwa Spika, mwenendo huo mzuri wa mapato ya
kodi na yasiyo ya kodi umetokana na juhudi za Serikali ya awamu ya tano
katika ukusanyaji wa mapato na kupunguza mianya ya ukwepaji wa kodi, tozo na
ada mbalimbali. Hata hivyo, mapato ya Halmashauri
hayakufikia lengo kutokana na mifumo ya ukusanyaji mapato isiyoridhisha pamoja
na kodi ya majengo kutokusanywa kwa kiwango kilichotarajiwa kulingana na fursa
zilizopo.
Misaada
na Mikopo ya Nje yenye Masharti Nafuu
18. Mheshimiwa Spika, Serikali ilitarajia kupata shilingi
trilioni 2.32 kutokana na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa
Washirika wa Maendeleo. Hadi Aprili, 2016, misaada na mikopo nafuu
iliyopatikana ni shilingi trilioni 1.15, sawa na asilimia 65 ya lengo la
kipindi hicho. Kutofikiwa kwa lengo kumetokana na baadhi ya Washirika wa
Maendeleo kuweka masharti mapya na kubadilika kwa sera ndani ya nchi zao
zinazohusiana na misaada kwa nchi zinazoendelea.
Mikopo
yenye masharti ya Kibiashara
19. Mheshimiwa Spika, mwaka 2015/16, Serikali ilipanga
kukopa kiasi cha shilingi trilioni 6.18 ambapo shilingi trilioni 4.03 ni kutoka
vyanzo vya ndani na shilingi trilioni 2.15 kutoka vyanzo vya nje. Fedha
hizo zililenga kugharamia miradi ya maendeleo na kulipia dhamana za Serikali za
muda mfupi na hatifungani za Serikali zilizoiva. Hadi Aprili, 2016 Serikali
ilikopa kutoka vyanzo vya ndani shilingi trilioni 3.94 sawa na asilimia 97.8 ya
lengo. Kati ya hizo, shilingi trilioni 2.56 zilikuwa kwa ajili ya kulipia
dhamana za Serikali za muda mfupi na hatifungani zilizoiva na shilingi trilioni
1.39 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, kwa upande wa mikopo
ya nje, Serikali ilisaini
mikataba yenye jumla ya Dola za Kimarekani milioni 674.3 na Benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya usafirishaji, awamu ya
pili ya mradi wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam pamoja na mradi wa maji
safi na maji taka Arusha. Hata hivyo, hali ya soko la mitaji ulimwenguni
ilikuwa mbaya na kusababisha kuongezeka kwa gharama za mikopo mipya kwa
kiwango kikubwa na hivyo kuathiri upatikanaji wa mikopo ya nje.
Matumizi
20. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2015/16 pamoja na
mambo mengine ililenga kugharamia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015; kukamilisha
miradi iliyoanza kutekelezwa; na kulinda mafanikio yaliyopatikana katika sekta
za elimu, afya, maji pamoja na maendeleo ya jamii. Hadi Aprili, 2016
Serikali ilitoa mgao wa matumizi wa shilingi trilioni 16.86 kwenye mafungu mbalimbali
sawa na asilimia 89.9 ya lengo la kipindi hicho. Kati ya kiasi hicho, shilingi
trilioni 13.65 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na
shilingi trilioni 3.21 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Miradi
ya maendeleo iliyogharamiwa kwa kutumia fedha za ndani ni pamoja na: usambazaji
wa umeme vijijini, ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja, ukarabati wa
reli ya kati, ujenzi wa mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi I na II, na
usambazaji wa maji mijini na vijijini.
Ulipaji
wa Madai
21. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kulipa madai
mbalimbali yaliyohakikiwa ya makandarasi, wahandisi washauri, watumishi na
wazabuni wa huduma na bidhaa kulingana na upatikaji wa fedha. Hadi Aprili
2016, Serikali imelipa jumla ya shilingi trilioni 1.13, kati ya fedha hizo:
shilingi bilioni 689.5 ni kwa ajili ya makandarasi na wahandisi washauri;
shilingi bilioni 27.9 kwa ajili ya walimu na malimbikizo ya mishahara ya
watumishi; shilingi bilioni 10.0 kwa ajili ya Jeshi la Polisi; shilingi bilioni
211.0 kwa ajili ya mikataba ya kijeshi; na shilingi bilioni 194.0 kwa ajili ya
ankara za umeme kwa Wizara, Idara zinazojitegemea na Taasisi za Serikali.
Mafanikio
na Changamoto katika Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2015/16
22. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha miezi kumi ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2015/16, Serikali
imefanikiwa kutekeleza shughuli muhimu za Bajeti licha ya kukabiliwa na
changamoto kadhaa. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka
kwa makusanyo ya kodi kufikia wastani wa
shilingi trilioni 1.02 kwa mwezi mwaka 2015/16 ikilinganishwa na wastani wa
shilingi bilioni 904.0 kwa mwezi mwaka 2014/15; kufanikisha
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kutumia fedha za ndani bila ya kupata msaada
kutoka kwa wadau wa maendeleo kama ilivyozoeleka kwa chaguzi zilizopita; na
kuanza kwa utekelezaji wa elimu ya msingi bila malipo.
23. Mheshimiwa Spika,
mafanikio mengine ni kuongezeka kwa wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu
ya juu kutoka wanafunzi 99,069 mwaka 2014/15 hadi 123,798 mwaka 2015/16; kulipa
malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa ya makandarasi, wazabuni wa huduma na
bidhaa na watumishi.
24. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo,
zimejitokeza changamoto kadhaa
zikiwemo: ukwepaji wa kodiunaohusisha wafanyabiashara na watumishi
wasio waadilifu; uelewa mdogo wa Sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani;
mwitikio mdogo wa wafanyabiashara katika matumizi ya mashine za kielektroniki
yaani EFDs pamoja na wananchi kutodai stakabadhi zitokanazo na mashine hizo
katika ununuzi wa bidhaa na huduma; mazingira magumu ya ukusanyaji wa kodi
katika sekta isiyo rasmi; uwepo wa wafanyakazi na wanafunzi hewa; na kuwepo kwa
mahitaji makubwa yasiyowiana na uwezo wa mapato, yakiwemo mahitaji ya kuboresha
miundombinu hususan ya maji, reli, bandari, viwanja vya ndege na barabara.
Usimamizi wa Deni la Taifa
25. Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea kusimamia Deni la Taifa kwa kuzingatia
Sheria ya Mikopo, Dhamana, na Misaada SURA 134. Katika kuhakikisha kuwa
deni la taifa linasimamiwa kikamilifu, Serikali inakamilisha uaandaji wa Sera
ya Usimamizi wa Deni la Taifa na kufanya marekebisho ya Sheria ya Mikopo,
Dhamana na Misaada SURA 134 ili iendane na Sera hiyo. Sera hiyo itatoa dira ya
muda mrefu katika usimamizi wa deni la Taifa na hivyo kuiwezesha Serikali kuwa
na usimamizi madhubuti wa deni la Taifa. Aidha, Sera hiyo itatoa mwongozo wa
kukuza na kuongeza ufanisi wa soko la fedha la ndani pamoja na kusaidia
utekelezaji wa Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134 kwa ufanisi zaidi.
26. Mheshimiwa
Spika, hadi Machi, 2016 Deni la Taifa lilikuwa Dola za Kimarekani
bilioni 20.94 ikilinganishwa na Dola za Kimarekani bilioni 19.69 Juni, 2015 ikiwa
ni sawa na ongezeko la asilimia 6.34. Kati ya kiasi hicho, Deni la Serikali
lilikuwa Dola za Kimarekani bilioni 17.93 na Deni la nje la sekta binafsi
lilikuwa Dola za Kimarekani bilioni 3.01. Aidha, Deni la Serikali liliongezeka
kwa asilimia 6.01 ikilinganishwa na Dola za Kimarekani bilioni 16.92 Juni,
2015. Ongezeko hilo lilitokana na mikopo ya ndani na nje kwa ajili ya
kugharamia miradi ya maendeleo. Baadhi ya miradi iliyoendelea kutekelezwa
kutokana na mikopo hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara na madaraja nchini,
mradi wa kimkakati wa kuboresha majiji, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kV
400 kutoka Iringa mpaka Shinyanga, mabasi yaendayo haraka, ujenzi wa bomba la
gesi na mitambo ya kusafishia gesi, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam,
na mradi wa maji Ruvu chini na Ruvu juu.
27. Mheshimiwa
Spika, pamoja na kuendelea kuongezeka kwa Deni la Taifa, bado ni
himilivu. Hii inathibitishwa na Tathmini ya Uhimilivu wa Deni la Taifa (Debt
Sustainability Assessment) iliyofanyika Mwezi Septemba, 2015 ambayo ilionesha
kuwa deni hilo ni himilivu katika kipindi cha muda wa kati na mrefu.
Madeni
ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Serikali
28. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/16, Serikali
iliahidi kulipa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kutoa hatifungani
maalum. Hata hivyo, katika hatua za mwisho za kukamilisha mikataba ya
makubaliano kati ya Serikali na mifuko ili kutoa hatifungani maalum,
kulijitokeza masuala mbalimbali yakiwemo utofauti katika ukokotoaji wa deni
pamoja na michango ya watumishi hewa. Kutokana na tofauti hizo, Serikali
kupitia Mkaguzi wa Ndani Mkuu ilianza kufanya uhakiki kwenye mifuko yote ya
Hifadhi ya Jamii. Mkaguzi wa Ndani Mkuu amekamilisha uhakiki kwenye Mfuko wa
PSPF na mara zoezi litakapokamilika kwenye mifuko mingine, Serikali itatoa
hatifungani maalum kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii. Serikali itafanya pia
maboresho katika sekta hii ya hifadhi za jamii ili kuleta ufanisi na tija.
III. BAJETI YA MWAKA 2016/17
Shabaha na Misingi
ya Bajeti ya Mwaka 2016/17
29. Mheshimiwa Spika, kufuatia kukamilika kwa zoezi la uchambuzi wa mwenendo
wa viashiria vya uchumi jumla na maoteo katika kipindi cha muda wa kati - financial
programming, shabaha za uchumi jumla katika kipindi cha mwaka 2016/17 ni
kama ifuatavyo:-
(i) Pato Halisi la Taifa kukua kwa asilimia 7.2
mwaka 2016 kutoka 7.0 mwaka 2015;
(ii) Kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei katika
wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 5.0 na asilimia 8.0 mwaka 2016;
(iii) Mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya
Halmashauri kufikia asilimia 14.8 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16, na kuendelea
kuongezeka kufikia asilimia 16.9 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17;
(iv) Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.8 ya
Pato la Taifa mwaka 2016/17 kutoka asilimia 12.6 ya Pato la Taifa mwaka
2015/16;
(v) Matumizi ya Serikali yanatarajiwa
kuongezeka kutoka asilimia 23.2 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16 hadi asilimia
27.0 mwaka 2016/17;
(vi) Nakisi ya bajeti inakadiriwa kuwa asilimia
4.5 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17 kutoka makadirio ya bajeti ya asilimia 4.2
mwaka 2015/16;
(vii) Nakisi katika urari wa malipo ya kawaida
kuwa asilimia 7.9 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16 na kupungua hadi asilimia 7.5
mwaka 2016/17; na
(viii) Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa
kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa
kipindi kisichopungua miezi minne Juni 2017.
30. Mheshimiwa Spika, shabaha na malengo hayo yatafikiwa
kwa kutegemea misingi ya Bajeti ifuatayo:-
(i) Kuendelea kuwepo kwa amani, usalama,
utulivu na utengamano nchini, kikanda na duniani;
(ii) Utulivu wa bei za mafuta ya petroli katika
soko la dunia;
(iii) Kuwepo kwa hali nzuri ya hewa nchini na
katika nchi jirani;
(iv) Kuendelea kuimarika kwa viashiria vya
uchumi jumla na maendeleo ya jamii kama vile Pato la Taifa, biashara ya nje,
ujazi wa fedha, mapato, matumizi na huduma za jamii;
(v) Kuimarika kwa sera za fedha na za bajeti
zitakazosaidia kupunguza mfumuko wa bei na tofauti kati ya riba za amana na za
mikopo;
(vi) Kuendelea kuimarika na kutengemaa kwa
uchumi wa dunia; na
(vii) Ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi
utaongezeka hususan kwenye uwekezaji katika viwanda.
Sera
za Mapato kwa mwaka 2016/17
31. Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya tano imedhamiria
kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua hatua
mbalimbali. Katika
mwaka 2016/17, mapato ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kupunguza
utegemezi wa kibajeti kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Katika kufanikisha
azma hii, sera za mapato kwa mwaka 2016/17 zimejielekeza kwenye maeneo yafuatayo:
(i) Kusimamia kikamilifu matumizi ya vifaa na
mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza ufanisi na
kudhibiti upotevu wa mapato;
(ii) Kuendelea kupanua wigo wa walipa kodi ikiwa
ni pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iweze kuingia katika mfumo wa
kodi;
(iii) Kuimarisha ufuatiliaji wa mapato
yanayokusanywa na taasisi na mamlaka mbalimbali za serikali;
(iv) Kuendelea kuchukua hatua za kudhibiti na
kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija; na
(v) Kuendelea kuimarisha usimamizi na kufanya
ukaguzi wa mara kwa mara bandarini, kwenye viwanja vya ndege na maeneo ya
mipakani ili kuhakikisha kodi stahiki zinakusanywa.
Misamaha ya Kodi
32. Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kudhibiti utoaji wa
misamaha ya kodi kwa taasisi za kidini na wawekezaji ili kuhakikisha inakuwa na
tija kwa Taifa. Katika kutekeleza hili, Serikali itafanya marekebisho ya sheria
husika ili kuondoa matumizi mabaya ya misamaha ya kodi. Marekebisho hayo
yatawasilishwa katika muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016. Pamoja na mambo
mengine, marekebisho hayo yatalenga kuwataka wanufaikaji kulipa kodi kwa bidhaa
watakazoagiza na baadae kuwasilisha maombi ya kurejeshewa kodi hiyo baada ya
uhakiki kufanyika.
33. Mheshimiwa
Spika, Serikali itaendelea kutangaza na kutoa taarifa za wanufaika wa
misamaha ya kodi kila robo ya mwaka ili wadau waweze kufahamu sekta au taasisi
iliyonufaika na misamaha hiyo na maeneo ilikoelekezwa. Utaratibu huu utasaidia
kudhibiti wafanyabiashara, taasisi na makampuni yanayotumia vibaya misamaha
hiyo kwa kujinufaisha wao binafsi na watumishi wa umma wasio waadilifu.
Mapato yasiyo ya Kodi
34. Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2016/17, usimamizi wa
ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi ikiwa ni pamoja na kodi ya majengo utakuwa
chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania. Uamuzi wa kuipatia TRA jukumu hili
unatokana na uzoefu na mifumo ya ukusanyaji wa mapato waliyonayo nchi nzima
lakini pia mafanikio na uzoefu wa nchi nyingine kama Ethiopia na Rwanda. Aidha,
Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu matumizi ya vifaa na mifumo ya
kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi ili kuongeza ufanisi
na kudhibiti upotevu wa mapato. Miongoni mwa makusanyo yanayolengwa ni pamoja
na: tozo, faini kama vile za mahakama na usalama barabarani, ada, viingilio
kwenye hifadhi za Taifa na viwanja vya michezo pamoja na vibali vya kuvuna maliasili.
35. Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa na utaratibu wa
kuziruhusu baadhi ya taasisi za Serikali kutumia mfumo wa kubakiza maduhuli
– retention. Utaratibu huu umekuwa ukipunguza mapato kwenye
Mfuko Mkuu wa Serikali na kuzinufaisha taasisi chache. Hivyo, kuanzia mwaka
2016/17, Serikali itafuta utaratibu huo. Uamuzi huu ni kwa mujibu wa Sheria ya
Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 kifungu 58 (a) mpaka (c) ambayo inaelekeza mapato
yote ya Serikali yakusanywe na kuingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Sambamba na matakwa ya Sheria ya Bajeti, tathmini iliyofanyika kuhusu utaratibu
wa retention ilibaini kuwa:
(i) Taasisi zinazohusika na utaratibu wa
“retention” zimeacha majukumu yao ya msingi na kuegemea zaidi kwenye shughuli
za ukusanyaji mapato. Mifano ni pamoja na Wakala wa Misitu na Kitengo cha
Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi;
(ii) Baadhi ya taasisi zenye mfumo wa
“retention” zinapata fedha nyingi na kuonekana kujinufaisha zaidi wakati
Wizara, Idara na Taasisi zingine zinakabiliwa na uhaba wa fedha. Hali hii
imesababisha kuongezeka kwa maombi kutoka taasisi nyingine kutaka kujiunga na
utaratibu huu;
(iii) Taasisi zilizo kwenye mfumo wa “retention”
bado zinalipwa mishahara asilimia 100 kutoka kwenye mfuko mkuu wa Serikali; na
(iv) Utaratibu huu wa “retention” umesababisha
idara ambazo awali zilikuwa zikichangia Mfuko Mkuu wa Serikali kupitia maduhuli
kutochangia na hivyo kupunguza mapato ya Serikali.
36. Mheshimiwa Spika, kutokana na sababu hizo, kuanzia sasa
mapato yote yatakusanywa na kuwasilishwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na kila
fungu litapewa fedha kulingana na bajeti yake. Wizara ya Fedha na Mipango kwa
upande wake itahakikisha kwamba fedha kutoka Mfuko Mkuu zinagawiwa kwa Mafungu
mbalimbali bila kuchelewa kulingana na mapato yaliyokusanywa.
Sera
za Matumizi kwa Mwaka 2016/17
37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17, Serikali itaendelea kusimamia
nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
pamoja na miongozo mbalimbali. Lengo kuu ni kupunguza matumizi yasiyo ya
lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa
cha fedha kwenye miradi ya maendeleo. Katika kutimiza azma hii, Serikali
itachukua hatua mbalimbali kama ifuatavyo:
(i) Kuwianisha matumizi na mapato halisi
yatakayopatikana kwa kila mwezi ili kuepuka malimbikizo ya madai. Maafisa
Masuuli wanaagizwa kuzingatia maelekezo ikiwemo kuingia miadi baada ya kupokea
mgao wa fedha (exchequer) na siyo kabla;
(ii) Kuhakikisa malipo kwa wazabuni na watoa
huduma yanafanyika kwa kuwasilisha Hati za Ununuzi - LPOs zitokanazo na IFMS;
(iii) Kuwasilisha Bungeni marekebisho ya Sheria
ya Ununuzi wa Umma ili kuziba mianya ya upotevu wa fedha katika ununuzi wa umma
na kuhakikisha ununuzi unawiana na thamani ya fedha itakayotumika;
(iv) Kudhibiti matumizi ya taasisi za Serikali
yasiyo na tija na kufanya tathmini ya gharama za uendeshaji ili kuchukua hatua
stahiki kwa maendeleo ya nchi;
(v) Kuendelea na zoezi la kuunganisha
Halmashauri zote nchini kwenye mfumo wa malipo ya kibenki ili kuongeza udhibiti
wa matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha kwamba malipo yanafika kwa wakati;
(vi) Kuhakikisha kuwa mashirika ya umma
yaliyoundwa kwa lengo la kujiendesha kibiashara yanajiendesha kwa faida bila
kutegemea ruzuku ya Serikali; na
(vii) Kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya
matumizi ya fedha za umma hususan katika miradi ya maendeleo.
Maeneo
ya Vipaumbele
38. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye hotuba yangu ya
Hali ya Uchumi, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 una maeneo makuu
manne (4) ya vipaumbele:- (i) Viwanda vya Kukuza Uchumi na Ujenzi wa Msingi wa
Uchumi wa Viwanda; (ii) Kufungamanisha Maendeleo ya Uchumi na Rasilimali Watu;
(iii) Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji; na (iv)
Usimamizi wa Utekelezaji wa Mpango. Ili kufikia malengo hayo, mikakati
itakayotumika ni pamoja na: kuhamasisha wawekezaji na sekta binafsi kuwekeza
katika viwanda na maeneo mbalimbali nchini hususan kupitia mfumo wa ubia baina
ya serikali na sekta binafsi (PPP); kuondoa vikwazo kwa kuimarisha mazingira ya
uwekezaji na kufanya biashara; na kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na tathmini
ya utekelezaji wa Mpango.
Kuongeza
Uzalishaji Viwandani
39. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali,
kauli mbiu ya Bajeti ya mwaka 2016/17 ni “kuongeza uzalishaji viwandani
ili kupanua fursa za ajira”. Katika kufikia azma hii, Serikali imelenga
kutekeleza mikakati mbalimbali itakayochochea uwekezaji katika viwanda.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na: kufanya uthamini wa ardhi na mali na
kulipa fidia kwa maeneo maalum ya uwekezaji yaliyotengwa nchini; kugharamia
tafiti za viwanda kupitia taasisi za TIRDO, TEMDO, CAMARTEC na COSTECH;
kuendeleza miundombinu ya viwanda vidogo kupitia SIDO; kuanzisha kongane za
viwanda (industrial clusters); na kuwezesha upatikanaji wa teknolojia rahisi na
nafuu kwa ajili ya viwanda. Katika mwaka 2016/17, Serikali imetenga fedha za
maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 50.9 katika fungu 44 na fungu
46 ambazo pamoja na mambo mengine zitagharamia utekelezaji wa maeneo
niliyoainisha hapo juu.
40. Mheshimiwa
Spika, kama
alivyoelekeza Mhe. Rais wakati wa hotuba ya ufunguzi wa Bunge lako Tukufu,
Serikali itahakikisha viwanda vilivyopo vinafanya kazi. Katika mwaka 2016/17,
Serikali itakamilisha tathmini ya viwanda vilivyobinafsishwa ili kuweka
mikakati ya namna bora ya kuviendeleza. Baadhi ya viwanda hivyo ni viwanda vya
nguo, viwanda vya mazao ya mifugo, viwanda vya kusindika mazao yakiwemo mazao
ya mpira, korosho, tumbaku, miwa na mpunga. Katika kutekeleza jukumu hilo,
fedha za maendeleo zimetengwa katika Mafungu mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza
mashamba; na kuimarisha uzalishaji wa mazao ya kilimo, na ya mifugo. Pamoja na
kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi katika viwanda, Serikali itachukua hatua
stahiki dhidi ya wawekezaji waliokiuka masharti ya mikataba ya mauzo ya viwanda
walivyobinafsishiwa.
41. Mheshimiwa
Spika, katika
kuboresha mazingira ya uwekezaji wa viwanda, Serikali imetenga fedha za
kuboresha miundombinu ya uwekezaji hususan ya umeme, maji, barabara, bandari na
reli. Aidha, Serikali imedhamiria kuondoa urasimu usio wa lazima na kuharakisha
utoaji wa maamuzi ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi katika viwanda.
Vilevile, zipo hatua mahsusi za kodi zinazopendekezwa katika Bajeti hii ambazo
zina lengo la kushawishi na kuhimiza uwekezaji wa sekta binafsi katika viwanda.
Serikali pia itaimarisha upatikanaji wa mikopo ya uendelezaji wa viwanda
kupitia Benki ya Rasilimali pamoja na taasisi nyingine za fedha.
42. Mheshimiwa
Spika, Serikali
kupitia balozi zetu na Diaspora, itaimarisha diplomasia ya uchumi katika nchi
mbalimbali hasa zile zilizoendelea pamoja na nchi ambazo uchumi wake unakua kwa
kasi, ikiwemo Jamhuri ya Watu wa China, India, Korea Kusini, Afrika Kusini na
Brazil ili kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania na hivyo kufanikisha
azma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda. Vilevile, Serikali itaendelea kuimarisha
mazingira ya uwekezaji nchini ambayo yatahamasisha kampuni za kigeni zilizoko
hapa nchini kuwa mabalozi wetu na kuvutia kampuni nyingine za nje wanakotoka
kuja kuwekeza hapa nchini. Hivyo, kama nilivyoeleza awali, jukumu la kuboresha
mazingira ya uwekezaji litapewa kipaumbele katika Bajeti ya mwaka 2016/17.
HATUA ZA KUTATUA KERO ZA
WANANCHI
43. Mheshimiwa Spika; bajeti hii itajikita kutatua kero
katika maeneo yaliyolalamikiwa na wananchi kama nilivyoeleza hapo awali. Baadhi
ya hatua za kibajeti na kiutawala zitakazochukuliwa ni kama ifuatavyo:
Rushwa katika Utoaji wa Huduma
44. Mheshimiwa
Spika, katika kukabiliana na suala la rushwa na ufisadi,
Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.5 ili kuwezesha uanzishwaji wa
mahakama ya mafisadi. Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni
72.3 katika bajeti ya mwaka 2016/17 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kuiwezesha taasisi hii
kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Vile vile katika bajeti ya mwaka 2016/17,
Serikali imetenga shilingi bilioni 44.7 kwa ajili ya kuiwezesha Ofisi ya Taifa
ya Ukaguzi kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kukagua na kudhibiti matumizi ya
fedha za umma.
Hatua za Kuzuia Upotevu wa Mapato
45. Mheshimiwa
Spika, Serikali itadhibiti upotevu wa mapato kwa kuimarisha
ufuatiliaji wa mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya biashara, bandarini,
viwanja vya ndege na mipakani; kuwajengea uwezo watumishi ili waweze kufanya
kaguzi za kitaalam hasa katika sekta za madini, maliasili, ardhi, mafuta na
gesi asilia; kuhimiza matumizi ya mifumo ya kieletroniki katika kukusanya
mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, pamoja na kupunguza misamaha ya kodi.
46. Mheshimiwa Spika, Serikali inawapongeza wafanyabiashara
walioitikia matakwa ya Sheria Ya Usimamizi wa Kodi ambayo inamtaka kila
mfanyabiashara isipokuwa wale ambao wametangazwa rasmi na Kamishna wa Mamlaka
ya Mapato kutotumia mashine za EFD kutoa risiti kila anapouza bidhaa au huduma.
Hata hivyo, kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao bado wanakaidi matakwa haya ya
kutumia mashine hizo. Napenda kuwasihi wafanyabiashara hao kuanza mara moja
kutumia mashine hizo vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni
pamoja na kuwanyang’anya leseni zao za biashara na hawataruhusiwa kufanya
biashara hapa nchini kwa kipindi kisichopungua miaka miwili. Aidha, kwa
upande wa Serikali, ili kuwa na usimamizi mzuri wa fedha za Serikali na
kuhakikisha kwamba zinatumika kama ilivyokusudiwa, kwa mamlaka niliyopewa chini
ya Sheria ya Fedha za Umma pamoja na kanuni zake malipo yote lazima
yaambatanishwe na ankara za madai au stakabadhi (tax invoice) zilizotolewa na
mashine za EFD. Kwa sababu hiyo kuanzia tarehe 1 Julai 2016, ni marufuku kwa
Wizara, Taasisi, Wakala za Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa
kufanya biashara na wazabuni na wafanyabiashara wengine ambao hawatumii mashine
za kielektroniki - EFDs. Aidha, malipo yatakayofanywa bila stakabadhi au Ankara
zisizokuwa za mashine za EFD ni lazima ziambatanishwe na ushahidi kuwa
mfanyabishara husika ametangazwa rasmi na Kamishna wa Mapato kutotumia mashine
za EFD.
Hatua za Kudhibiti Matumizi
47. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea
kuchukua hatua za kupunguza na kudhibiti matumizi bila kuathiri ubora wa huduma zinazotolewa
na hivyo kuhakikisha uwepo wa ufanisi katika matumizi ya Serikali. Baadhi ya
hatua hizo zimeainishwa katika Mwongozo wa kutayarisha Mpango na Bajeti ya
mwaka 2016/17 niliouwasilisha hapa Bungeni Februari, 2016. Miongoni mwa hatua
hizo ni pamoja na:
(i) Kuhakikisha
mikutano yote ikiwa ni pamoja na mikutano ya bodi, mafunzo na semina inatumia
kumbi za Serikali na Taasisi za Umma;
(ii) Kutoa
kipaumbele kwa Taasisi za Umma katika kutoa huduma kwa Serikali kama vile bima,
usafirishaji wa barua, mizigo na vifurushi, matangazo na usafiri;
(iii) Kudhibiti
matumizi ya umeme, simu na maji ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa
mara;
(iv) Kudhibiti
ulipaji wa mishahara kwa watumishi ili kuepuka malipo yasiyostahili. Aidha,
Serikali itaendelea kufanya sensa ya watumishi wote;
(v) Kudhibiti
utoaji wa mikopo ya elimu ya juu ili kuepuka utoaji wa mikopo kwa wanafunzi
wasio stahili;
(vi) Kuendelea
kufanya ununuzi wa magari kwa pamoja na bidhaa moja kwa moja kutoka kwa
wazalishaji ili kupata unafuu
wa bei;
(vii) Kuendelea kudhibiti gharama za uendeshaji
wa magari ikiwa ni pamoja na matengenezo, mafuta na vilainishi;
(viii) Kupunguza na kuondoa matumizi yasiyo na
tija katika maeneo mbalimbali ikiwemo maadhimisho na sherehe za kitaifa,
matamasha, machapisho na safari za ndani na nje ya nchi zisizo na tija;
(ix) Kuhimiza matumizi ya nakala laini (soft
copy) za machapisho mbalimbali hususan yanayozidi kurasa 50 ili kupunguza
gharama za uchapishaji na kutunza mazingira; na
(x) Kudhibiti matumizi ya Taasisi na Mashirika ya
Umma yasiyowiana na majukumu yao ya msingi na yasiyo na tija.
Kero katika Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
48. Mheshimiwa Spika, azma kuu ya Serikali ni kuimarisha sekta ya kilimo,
mifugo na uvuvi kwa mtazamo wa kibiashara, kukuza viwanda na kuongeza thamani
ya mazao yatokanayo na sekta hii. Hata hivyo, bado sekta hii inakabiliwa na
changamoto kadhaa zikiwemo kodi na tozo za mazao zisizo na tija, uhaba wa
pembejeo, vifaa duni, masoko, na uhaba wa maafisa ugani.
49. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo,
Serikali imetenga jumla ya shilingi trilioni 1.56 sawa na asilimia 4.9 ya
bajeti yote ukiondoa deni la Taifa kwa ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali
katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji zikiwemo ununuzi wa pembejeo;
kuboresha upatikanaji wa masoko; kuongeza upatikanaji wa zana bora na za kisasa
za kilimo, ufugaji na uvuvi; na kuongeza maafisa ugani.
50. Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kupunguza ama
kuondoa kabisa ushuru na kodi mbalimbali za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi
zisizo na tija. Nitaeleza hatua mahsusi muda mfupi ujao. Aidha, Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania itaendelea kutoa mikopo ya riba nafuu na masharti
yanayozingatia hali halisi ya sekta ya kilimo ili kusaidia kuleta mapinduzi ya
kilimo kutoka kilimo cha kijungujiko (subsistence farming) kwenda
kilimo cha kibiashara. Katika mwaka 2016/17, Benki ya Kilimo itaendelea
kutangaza na kupanua huduma zake kwa wananchi mikoani.
Migogoro ya Ardhi
51. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na juhudi za
kutatua migogoro katika Sekta ya ardhi ikiwemo migogoro
kati ya wakulima na wafugaji, vijiji na hifadhi, wananchi na wawekezaji,
uvunjaji wa sheria za ardhi na umiliki wa mashamba pori. Katika kukabiliana na migogoro hiyo,
Serikali imetenga shilingi bilionibilioni
5.0 kwa ajili ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi; shilingi bilioni 13.0 kwa ajili ya
utekelezaji wa mradi wa umilikishwaji wa ardhi; na shilingi bilioni 8.8 kwa
ajili ya ununuzi wa vifaa vya upimaji wa ardhi. Aidha, Serikali imetenga
shilingi bilioni 33.4 kwa ajili ya programu ya kuwezesha umilikishaji wa ardhi
na uwekaji wa kumbukumbu utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu.
Vilevile, Serikali itaendelea kusajili migogoro ya ardhi katika maeneo
mbalimbali nchini na kutafuta ufumbuzi kulingana na mazingira ya eneo husika
ili kupunguza migogoro baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi.
Huduma zisizoridhisha za Usafiri na Usafirishaji
52. Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kukabiliana na kero
zinazotokana na uchakavu wa miundombinu ya reli, barabara, bandari na viwanja
vya ndege. Katika mwaka 2016/17, Serikali imetenga shilingi trilioni 5.47 sawa
na asilimia 25.4 ya bajeti yote ukiondoa Deni la Taifa, kwa ajili ya miradi ya
ujenzi na uchukuzi. Baadhi ya maeneo yanayohusika ni;
(i) Ujenzi wa miundombinu ya barabara – kiasi
cha shilingi trilioni 2.18 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hasa
zenye kufungua fursa za kiuchumi na kukarabati barabara zilizopo
(ii) Uchukuzi – kiasi cha shilingi trilioni 2.49
kimetengwa kwa ajili ya kuanza kujenga reli ya kati kwa kiwango cha standard
gauge; ununuzi wa ndege mpya tatu za abiria; ununuzi wa meli mpya ziwa
Viktoria; ukarabati wa meli katika ziwa Viktoria na ziwa Tanganyika; uboreshaji
wa miundombinu ya bandari; na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege. Aidha,
Kiasi cha shilingi bilioni 161.4 kimetengwa katika Mfuko wa Reli kwa ajili ya
ununuzi wa mabehewa na vichwa vya treni pamoja na ukarabati wa na Reli.
Umeme
53. Mheshimiwa
Spika, Serikali imetenga jumla ya shilingi trilioni 1.13 sawa
na asilimia 5.3 ya bajeti yote bila kujumuisha Deni la Taifa ili kugharamia
upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa ajili ya matumizi ya majumbani na
viwandani. Baadhi ya miradi itakayotekelezwa ni pamoja na: kuongeza kasi ya
usambazaji umeme vijijini kupitia REA na kukamilisha miradi ya umeme
inayoendelea ikiwemo kuongeza mitambo mingine yenye uwezo wa kufua MW 185
katika mradi wa Kinyerezi – I na Kinyerezi II. Serikali itahakikisha kuwa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linakuwa na uwezo kifedha ili lijiendeshe
lenyewe na kuwa na ushindani katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo
nafuu ili kupunguza gharama kwa wazalishaji na walaji.
Upatikanaji duni wa huduma za afya, maji na elimu.
54. Mheshimiwa Spika, kuna changamoto nyingi katika
maeneo haya, ikiwemo kukosekana kwa upatikanaji wa uhakika wa maji safi
na salama kwa ajili ya matumizi ya majumbani na viwandani; na huduma bora za
afya. Aidha, kuna changamoto za ubora wa elimu na upatikanaji wa mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu kwa wakati. Bajeti ya mwaka 2016/17 imejielekeza katika kutatua
changamoto hizo kama ifuatavyo:
Elimu
55. Mheshimiwa Spika, sekta
ya elimu imetengewa jumla ya shilingi trilioni 4.77 sawa na asilimia 22.1
ya bajeti yote bila kujumuisha Deni la Taifa. Fedha hizi zimetengwa kwa ajili
ya kugharamia shughuli mbalimbali za elimu zikiwemo: Elimu Msingi bila malipo;
gharama za uendeshaji wa shule ikiwemo chakula, ununuzi wa vitabu, na mitihani;
mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu; na ujenzi na ukarabati wa
miundombinu ya elimu katika ngazi zote
Afya
56. Mheshimiwa
Spika, kwa kutambua umuhimu wa huduma bora za afya kwa wananchi,
Serikali imetenga jumla ya shilingi trilioni 1.99 sawa na asilimia 9.2 ya
bajeti yote bila kujumuisha Deni la Taifa kwa ajili ya sekta ya afya.
Baadhi ya maeneo yanayohusika ni pamoja na ununuzi wa dawa, vifaa tiba na
vitendanishi (reagents) ambayo yametengewa shilingi bilioni 180.5; ulipaji wa
deni la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) shilingi bilioni 71.0; na uboreshaji wa
miundombinu ya kutolea huduma za afya katika ngazi zote.
Maji
57. Mheshimiwa
Spika, Serikali imetenga kiasi cha shilingi trilioni 1.02 sawa na
asilimia 4.8 ya bajeti yote bila kujumuisha Deni la Taifa, kwa ajili ya
kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama nchini. Baadhi ya
shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na: ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya
maji mijini na vijijini; ulipaji wa madeni ya wakandarasi na utekelezaji wa
shughuli za Mfuko wa Maji.
Mazingira Wezeshi kwa Sekta Binafsi
58. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo juu,
katika bajeti ya 2016/17 Serikali imedhamiria kuboresha mazingira ya kufanya
biashara, ikiwa ni pamoja na kuwekeza kwenye miundombinu ya reli,
barabara, bandari, maji na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika ili
kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika maeneo mbalimbali. Aidha, Serikali
itaendelea kupitia kodi, tozo na ada mbalimbali ili kuzipunguza au kuziondoa
zile ambazo zinalalamikiwa na wananchi na wawekezaji wa ndani na nje. Miongoni
mwa jitihada zitakazochukuliwa na Serikali ili kuongeza ushiriki wa sekta
binafsi katika uchumi ni pamoja na kuboresha huduma za upatikanaji wa mikopo
kwa sekta binafsi, kuimarisha soko la mitaji, kukuza utaratibu wa ubia kati ya
sekta ya umma na sekta binafsi - PPP, na kuboresha mazingira ya kufanya
biashara kwa kuboresha miundombinu ya umeme, usafirishaji, maji, usambazaji wa
gesi asilia, mfumo wa kodi, kuweka vivutio mbalimbali, kuondoa urasimu
usio wa lazima na kupambana na rushwa.
Uwezeshaji kiuchumi wa Makundi Maalum
(i) Maendeleo
Vijijini
59. Mheshimiwa
Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeazimia kuwezesha wananchi
kiuchumi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka
2015 ambapo shilingi milioni 50 ziliahidiwa kwa kila kijiji ili kuwawezesha
wananchi kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji kupitia Ushirika wa
Kuweka na Kukopa (SACCOS) na vikundi vingine vya kiuchumi. Katika kutekeleza
ahadi hii, Serikali imetenga shilingi bilioni 59 kwa ajili ya utekelezaji wa
mpango huu kwa awamu. Mpango huu utaanza kutekelezwa chini ya Ofisi ya Waziri
Mkuu mara baada ya kukamilisha utaratibu wa matumizi ya fedha hizo ili
kuhakikisha kuwa fedha hizi zinatumika ipasavyo.
(ii) Vijana,
Wazee, Wenye Ulemavu, Wanawake na Watoto
60. Mheshimiwa
Spika, Bajeti ya 2016/17 imezingatia mahitaji ya makundi maalum
ya vijana, wazee, wenye ulemavu, wanawake na watoto wanaoishi katika mazingira
hatarishi. Katika mwaka 2016/17 Serikali imetenga shilingi
bilioni 2.4 kwa ajili yauboreshaji wa miundombinu ya makazi ya wazee
na mahabusu za watoto; na chakula, dawa na mahitaji mengine ya watoto walio
katika mazingira hatarishi. Katika mwaka wa fedha 2016/17, Serikali
imetenga asilimia 5.0 ya mapato ya ndani ya kila Halmashauri kwa ajili ya
vijana. Aidha, shilingi bilioni 1.0 zimetengwa chini ya Fungu 65 (Ofisi ya
Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, kifungu cha 2032 mradi namba
4945) kwa ajili ya kuendeleza vijana. Vilevile, shilingi bilioni 5.0 zimetengwa
Fungu 65, kifungu cha 2002 mradi namba 6581 kwa ajili ya kuendeleza ujuzi kwa
vijana ambao hawana ajira na walio kwenye soko la ajira.
61. Mheshimiwa
Spika, katika bajeti ya 2016/17, Serikali imetenga asilimia 5.0
ya mapato ya ndani ya kila Halmashauri kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya
maendeleo ya wanawake katika Halmashauri husika. Vilevile, Serikali imetenga
shilingi bilioni 1.95 kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi chini ya
Fungu 53 (Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kifungu
cha 3001 mradi namba 4950). Kuhusu watu wenye ulemavu, Serikali itaendelea
kuhakikisha kuwa vifaa vilivyotengenezwa mahsusi kwa ajili yao vinasamehewa
kodi ili viweze kupatikana kwa bei nafuu. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha
shule maalum za watoto wenye ulemavu na kugharamia mahitaji yao ili kuwajengea
mazingira mazuri zaidi ya kujifunzia.
(iii) Wasanii, Wabunifu
na Wanamichezo
62. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2016/17 Serikali kupitia Fungu 96 imetenga
jumla ya shilingi bilioni 3.0 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya
sanaa, ubunifu, utamaduni na michezo ikiwa ni pamoja na: kuratibu na kusimamia
uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Ubunifu; kusimamia urasimishaji
wa shughuli za Sanaa; kusimamia na kudhibiti filamu zitakazoingia
sokoni bila kufuata taratibu; na kuratibu uendeshaji wa kazi za sanaa nchini.
(iv)Wachimbaji Wadogo
wa Madini
63. Mheshimiwa
Spika, Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwezesha wachimbaji
wadogo wa madini ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli zao na hivyo
kuongeza ajira, kukuza kipato cha wachimbaji na wananchi wanaozunguka maeneo ya
uchimbaji madini. Katika mwaka 2016/17 Serikali inakusudia kutekeleza
yafuatayo: kuwapatia ruzuku; kuwapatia mafunzo; kuwatengea maeneo maalum ya
uchimbaji; kuimarisha soko; pamoja na kuziwezesha taasisi zinazohusika na
ukaguzi wa usalama wa migodi ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika. Kiasi
cha fedha kilichotengwa kwa madhumuni haya katika bajeti ya 2016/17 ni shilingi
milioni 900 kwa ajili ya ruzuku ya wachimbaji wadogo.
(v) Wafanyakazi
64. Mheshimiwa
Spika, ili kuboresha kipato cha wafanyakazi, siku ya Mei Mosi
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, aliagiza kiwango cha kodi ya mapato kwenye mishahara (PAYE)
kipunguzwe kutoka asilimia 11 hadi asilimia 9 ili kupunguza makali ya maisha
kwa wafanyakazi. Agizo hilo litaanza kutekelezwa Julai Mosi 2016. Aidha, kuanzia
mwaka ujao wa fedha Serikali itaanza kuwasilisha mchango wa mwajiri wa asilimia
0.5 ya mshahara kwenye Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi ili watumishi wa umma
wapatapo ajali mahali pa kazi waweze kulipwa na Mfuko. Kadhalika, Serikali
itaendelea kuboresha mazingira ya kuwezesha watumishi wake kujenga ama kununua
nyumba kupitia Bodi ya Mfuko wa Mikopo ya Nyumba kwa Watumishi wa Serikali,
pamoja na Watumishi Housing Company.
(vi)Vyombo vya Ulinzi
na Usalama
65. Mheshimiwa
Spika, Serikali inavipongeza vyombo vya ulinzi na
usalama kwa kujipambanua kwa nidhamu ya hali ya juu katika kazi zao. Hata
hivyo, Serikali inawaelekeza Maafisa Masuuli wa Mafungu husika kujipambanua
vivyo hivyo kwa nidhamu kama hiyo katika matumizi ya fedha na mali za umma. Aidha,
katika mwaka 2016/17, utaratibu wa kutoa misamaha ya kodi kwenye maduka ya
vyombo vya ulinzi na usalama utasitishwa na nitaeleza utaratibu mpya baadaye.
Kadhalika, Serikali itaendelea kujenga nyumba za makazi kwa askari ili
kukabiliana na uhaba wa makazi kwa askari nchini.
IV. MABORESHO YAMFUMO WA KODI, ADA, TOZO NA
HATUA NYINGINE ZA MAPATO
66. Mheshimiwa Spika, napenda
kuwasilisha sasa mapendekezo ya hatua mpya za kufanya
marekebisho ya mfumo wa kodi, ikiwemo kurekebisha baadhi ya viwango vya kodi,
tozo na ada chini ya Sheria mbalimbali na kuboresha taratibu za ukusanyaji na
usimamizi wa mapato ya Serikali. Aidha, marekebisho haya yanalenga pamoja na
mambo mengine, kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea ukuaji wa uchumi
hususan katika sekta ya viwanda, kilimo, usafirishaji na kukuza ajira.
Marekebisho hayo yanahusu Sheria zifuatazo:-
a. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA
148;
b. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
c. Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
d. Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi,
SURA 82;
e. Sheria ya Magari (Kodi ya Usajili na
Uhamisho wa Umiliki), SURA 124;
f. Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, SURA
399 (sambamba na Sheria ya kodi ya Majengo ya Mamlaka ya Miji, SURA 289; Sheria
ya Fedha za Umma ya Serikali za Mitaa, SURA 290; Sheria ya Utawala wa Kodi ya
mwaka 2015; na Sheria ya Rufani za Kodi, SURA 408);
g. Sheria ya Msajili wa Hazina (Mamlaka na
Majukumu), SURA 370;
h. Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki, ya mwaka 2004;
i. Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya
Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali; na
j. Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali
zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea;
a) Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA
148
67. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kama ifuatavyo: -
(i) Kusamehe
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye maharage ya soya baada ya kubaini kuwa,
mazao haya yalisahaulika kuingizwa kwenye orodha chini ya kifungu cha 3 cha
jedwali la misamaha linalojumuisha mifugo, mazao ya kilimo ambayo hayajasindikwa
na chakula cha binadamu;
(ii) Kusamehe
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mbogamboga zote na mazao ya mifugo yakiwahayajasindikwa kama yanavyoonekana kwenye
Ushuru wa Pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, sura ya 2 na 3 (mazao ya
mifugo yasiyosindikwa), sura ya 7 (matunda na karanga), sura ya 8 (nafaka),
sura ya 10 (unga wa nafaka) na sura ya 11 (mbegu za mazao). Hatua hii
inakusudia kutoa msamaha wa kodi ya VAT kwenye mazao ya chakula ambayo
hayajasindikwa ili kuwezesha upatikanaji wa lishe bora ya msingi kwa gharama
nafuu;
(iii) Kuongeza
vitamini na virutubishi kwenye orodha ya vifaa na madawa muhimu
yaliyoidhinishwa na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
kwa ajili ya kupata msamaha wa kodi. Vitamini na virutubishi hivyo huongezwa
kwenye vyakula ili kuboresha lishe kama njia mojawapo ya kuimarisha afya ya
jamii;
(iv) Kuongeza
madawa ya kutibu maji yanayotumiwa na binadamu kwenye orodha ya vifaa na madawa
muhimu yaliyoidhinishwa na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto kwa ajili ya kupata msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani. Madawa haya
ni muhimu kwa ajili ya kulinda afya ya msingi kwa kutumia maji salama. Waziri
wa Maji na Umwagiliaji atatakiwa kuwasilisha orodha ya madawa hayo kwa Waziri
wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili ayajumuishe kwenye orodha
hiyo;
(v) Kutoza
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma za utalii hususan kuongoza watalii,
kuendesha watalii, utalii wa majini, kuangalia wanyama na ndege wa porini,
kutembelea hifadhi na usafirishaji wa watalii ardhini. Hatua hii inachukuliwa
kama ilivyokusudiwa wakati wa kutunga Sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani, ambayo ilianza kutumika rasmi Julai 2015, lakini kwa kutambua mikataba
iliyokuwepo wakati huo kati ya watoa huduma za utalii na watalii waliokuwa
wanatarajia kuja nchini, ilikubalika kusubiri kukamilika kwa makubaliano hayo
kwa mwaka unaomalizika. Huduma hizi pia hutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani
kwenye nchi nyingine kama vile Kenya, Rwanda na Afrika ya Kusini;
(vi) Bidhaa
zinazotengezwa Tanzania Bara na kuuzwa Zanzibar zitatozwa Kodi ya Ongezeko la
Thamani upande wa Zanzibar, na bidhaa zinazotengezwa Zanzibar na kuuzwa
Tanzania Bara zitatozwa kodi hiyo upande wa Tanzania Bara. Lengo la hatua hii
ni kuondoa utaratibu uliokuwepo hapo awali wa kufanya marejesho ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani kwenda Zanzibar kwa kuwa Sheria ya Kodi hiyo inayotumika
sasa haina kifungu kinachoruhusu marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
kwenda Zanzibar kama ilivyokuwa kwenye sheria iliyofutwa. Kwa kuwa kila upande
wa Muungano una Sheria yake ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, kodi hii itatozwa
sehemu ambako bidhaa au huduma itatumika, yaani “destination principle”. Kwa
msingi huo muhimu katika utozaji Kodi ya Ongezeko la Thamani, Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar itakuwa inakusanya kodi hii kwa bidhaa zinazozalishwa
Tanzania Bara na kupelekwa Zanzibar. Vile vile, Tanzania Bara itakuwa
inakusanya kodi hii kwa bidhaa zinazozalishwa Zanzibar na kuletwa Tanzania
Bara;
(vii) Kufanya
marekebisho katika orodha ya misamaha ya bidhaa za petroli chini ya kifungu cha
15 cha Jedwali la misamaha la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka
2014 ili kujumuisha pia bidhaa za lami zenye HS Code 27.13, 27.14 na 27.15
ambazo hazikujumuishwa katika Jedwali hilo;
(viii) Kusamehe
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye bima ya vyombo vya usafiri wa anga
vinavyotambulika katika HS Code 88.01 na Hs Code 88.02. Hatua hii inapendekezwa
kwa kuzingatia kuwa sekta ya usafirishaji wa anga bado ni changa kuweza
kuhimili ulipaji wa bima kwa vyombo hivyo vya usafiri. Hivyo kuna umuhimu wa
kuhamasisha ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga na hatimaye kukuza utalii.
Aidha, hatua hii itasaidia wawekezaji katika sekta ya usafiri wa anga kutumia
bima za hapa nchini badala ya nje kwenye mikataba ya ukodishaji; na
(ix) Kutoza
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye ada za huduma za kibenki zinazotozwa na
benki hizo ili kupanua wigo wa kodi isipokuwa riba kwenye mikopo.
Hatua
hizi za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza
mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 136,140.3.
68. Mheshimiwa Spika, sambamba na marekebisho hayo kwenye
Kodi ya Ongezeko la Thamani, Serikali itachukua hatua mbalimbali za kiutawala
ndani ya Mamlaka ya Mapato ili kuboresha makusanyo ya Kodi hii, ikiwa ni pamoja
na kuanzisha programu kabambe ya ufuatiliaji wa makusanyo na hivyo kupanua wigo
wa kodi. Ili kutekeleza azma hii, Serikali itatekeleza yafuatayo:
(i) kuhakikisha
kuwa daftari la usajili wa walipakodi linahuishwa kila wakati ili kuwa na
taarifa sahihi za walipa kodi hao;
(ii) kuhakikisha
kuwa wafanyabiashara wote wakubwa na wa kati hapa nchini wanapatiwa mashine za
kielektroniki na zinatumika kikamilifu;
(iii) kuendelea
kuimarisha ukaguzi wa hesabu za walipakodi ili kuwezesha kodi stahiki kulipwa
kwa wakati; na
(iv) Kuanzisha
ofisi mpya za kusimamia mapato kwa ngazi za wilaya katika mikoa ya kikodi
kwenye Jiji la Dar es Salaam na vituo vipya vya huduma kwa walipakodi katika
maeneo mbalimbali ya majiji na miji mikubwa.
69. Mheshimiwa Spika, Napendekeza pia kufanya mapitio ya Sheria
ya Uwekezaji ili iendane na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa lengo la
kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija.
Hatua
za kiutawala kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha
shilingi milioni 268,607.1.
b) Sheria ya Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty),
SURA 147
70. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 kama ifuatavyo: -
(i) Kufanya
marekebisho ya viwango maalum vya kodi (specific duty rates) vya bidhaa zisizo
za petrol kwa kiwango cha mfumuko wa bei wa asilimia 5. Marekebisho haya ni kwa
mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa inayotaka yafanyike marekebisho ya viwango
hivyo vya ushuru kulingana na mfumuko wa bei ili kuendana na thamani halisi ya
fedha. Hata hivyo, marekebisho haya hayatafanyika kwenye maji ya kunywa
yaliyosindikwa kwenye chupa. Mabadiliko ninayopendekeza ni kama ifuatavyo:
a) Ushuru wa vinywaji baridi, kutoka shilingi
55 kwa lita hadi shilingi 58 kwa lita;
b) Ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda
(juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa hapa nchini kutoka shilingi
10 kwa lita hadi shilingi 11 kwa lita;
c) Ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi)
iliyotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini kutoka shilingi 200
kwa lita hadi shilingi 210 kwa lita;
d) Ushuru wa bia inayotengenezwa kwa nafaka ya
hapa nchini na ambayo haijaoteshwa (unmalted), mfano kibuku, kutoka shilingi
409 kwa lita hadi shilingi 430 Kwa lita;
e) Ushuru wa bia nyingine kutoka shilingi 694
kwa lita hadi shilingi 729 kwa lita;
f) Ushuru wa bia zisizo na kilevi, ikijumuisha
vinywaji vya kuongeza nguvu kutoka shilingi 508 kwa lita hadi shilingi 534 kwa
lita;
g) Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu
inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 kutoka shilingi
192 kwa lita hadi shilingi 202 kwa lita;
h) Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu
inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 kutoka shilingi
2,130 kwa lita hadi shilingi 2,237 kwa lita;
i) Ushuru wa vinywaji vikali kutoka shilingi
3,157 kwa lita hadi shilingi 3,315 kwa lita;
j) Ushuru wa bidhaa kwenye maji yanayozalishwa
viwandani hautaongezeka;
k) Sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa
kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia
75, kutoka shilingi 11,289 hadi shilingi 11,854 kwa kila sigara elfu moja;
l) Sigara zenye kichungi zinazotengenezwa
kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia
75, kutoka shilingi 26,689 hadi shilingi 28,024 kwa kila sigara elfu
moja;
m) Sigara nyingine zenye sifa tofauti na (k)
na (l) hapo juu kutoka shilingi 48,285 hadi shilingi 50,700 kwa kila sigara
elfu moja;
n) Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza
sigara (cut filler) kutoka shilingi 24,388 hadi shilingi 25,608 kwa kilo;
o) Ushuru wa “cigar” unabaki kuwa asilimia 30;
p) Ushuru wa mafuta ya kulainishia mitambo
kutoka shilingi 665.50 kwa lita hadi shilingi 699 kwa lita;
q) Ushuru wa grisi za kulainishia mitambo
kutoka senti 75 kwa kilo hadi senti 79 kwa kilo; na
r) Ushuru wa gesi asilia kutoka senti 43 kwa
futi za ujazo hadi senti 45 kwa futi za ujazo.
(ii) Kuongeza
ushuru wa bidhaa (excise duty) unaotozwa kwenye samani zinazoagizwa kutoka nje
ya nchi zinazotambulika katika HS Code 94.01 na HS Code 94.03 kutoka asilimia
15 hadi asilimia 20 kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya samani
zinazotengenezwa kwa kutumia mbao zinazozalishwa hapa nchini, kuongeza ajira na
kuongeza mapato ya Serikali;
(iii) Kutokana
na ugumu uliojitokeza katika kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na
mifuko ya plastiki, Serikali imeamua kupiga marufuku utengenezaji, uuzaji,
ununuzi na matumizi ya mifuko ya plastiki yenye kipimo cha unene chini ya
microns 50; na
(iv) Kutoza
ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye ada zinazotozwa na watoa huduma wa simu
katika kutuma na kupokea fedha badala ya ushuru huo kutozwa tu kwenye kutuma
fedha pekee. Katika utaratibu wa sasa, baadhi ya kampuni zinazotoa huduma
zimetumia mwanya kwa kuhamishia sehemu kubwa ya ada hizo kwenye kupokea fedha
na hivyo kuwa nje ya wigo wa kodi.
Hatua
hizi za ushuru wa bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali
kwa kiasi cha shilingi milioni 63,639.4.
c) Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
71. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kama ifuatavyo: -
(i) Kuondoa
msamaha wa kodi ya mapato kwenye malipo ya kiinua mgongo kinacholipwa kwa
wabunge kila mwisho wa muhula wa miaka mitano ili kujenga misingi ya usawa na
haki katika utozaji wa kodi kwa kila mtu anayestahili kulipa kodi;
(ii) Kutoza
Kodi ya Mapato kwenye mapato yote yatokanayo na hisa kwenye makampuni.
Marekebisho hayo yatafanyika kwa kufuta aya ya (d) katika kifungu cha 3 cha
Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 cha tafsiri ya maneno “Investment Asset”
(rasilimali za uwekezaji) iliyokuwa inatoa msamaha wa kodi kwa wenye hisa chini
ya asilimia 25 kwenye makampuni. Hatua hii itaongeza wigo wa kodi kwa ujumla
wake na kupunguza misamaha ya kodi;
(iii) Kupunguza
kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato yanayotokana na ajira kutoka
asilimia 11 hadi asilimia 9. Hatua hii inachukuliwa ikiwa ni sehemu ya dhamira
ya Serikali ya muda mrefu ya kuwapunguzia mzigo wa kodi wafanyakazi hatua kwa
hatua hadi kufikia kiwango cha tarakimu moja. Katika kutekeleza azma hiyo,
Serikali imekuwa ikipunguza kiwango cha kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia
18.5 mwaka 2006/07 hadi kufikia asilimia 9 inayopendekezwa sasa. Kutokana na
mabadiliko hayo, viwango vya kodi vya sasa na vinavyopendekezwa ni kama
ifuatavyo:
Viwango
vya sasa
Ngazi
|
Mapato kwa Mwezi
|
Kodi kwa mwezi
|
1.
|
Mapato ya jumla yasiyozidi Shilingi170,000/=
|
Asilimia sifuri (0%)
|
2.
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi170,000/=lakini
hayazidi shilingi 360,000/=
|
11% ya kiasi kinachozidi Shilingi 170,000/=
|
3.
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 360,000/= lakini
hayazidi shilingi540,000/=
|
Shilingi
20,900/= + 20% ya kiasi kinachozidi Shilingi 360,000/=
|
4.
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 540,000/= lakini
hayazidi shilingi720,000/=
|
Shilingi 56,900/= + 25% ya kiasi kinachozidi Shilingi
540,000/=
|
5.
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi720,000/=
|
Shilingi 101,900/= + 30% ya kiasi kinachozidi Shilingi
720,000/=
|
Viwango
vinavyopendekezwa
Ngazi
|
Mapato kwa Mwezi
|
Kodi kwa mwezi
|
1
|
Mapato ya jumla yasiyozidi Shilingi170,000/=
|
Asilimia sifuri (0%)
|
2
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi170,000/=lakini
hayazidi shilingi 360,000/=
|
9% ya kiasi kinachozidi shilingi 170,000/=
|
3
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 360,000/= lakini
hayazidi shilingi540,000/=
|
Shilingi17,100+ 20% ya kiasi kinachozidi shilingi
360,000/=
|
4
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 540,000/= lakini
hayazidi shilingi720,000/=
|
Shilingi53,100+ 25% ya kiasi kinachozidi shilingi
540,000/=
|
5
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi720,000/=
|
Shilingi98,100+ 30% ya kiasi kinachozidi shilingi
720,000/=
|
(iv) Kutoza
kodi ya zuio kwenye malipo yanayofanywa kwenye mifuko ya jamii yanayotokana na
mapato ya uwekezaji ili kuweka misingi ya usawa na haki katika utozaji kodi.
Hatua hii inalenga kuweka wajibu kwa makampuni wa kutoza kodi ya zuio kwenye
malipo yanayofanywa kwenye mifuko ya jamii kutokana na upangishaji, ukopeshaji,
n.k; na
(v) Kumpa
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mamlaka ya kukadiria mapato
yanayotokana na pango kwa kuweka kiwango cha ukomo wa chini wa thamani
kulingana na hali halisi ya soko ili kutoza kodi kwenye mapato hayo (rental
income).
Hatua
hizi za Kodi ya Mapato kwa pamoja zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa
kiasi cha shilingi milioni 71,586.9.
72. Mheshimiwa Spika, sambamba na marekebisho hayo
kwenye Kodi ya Mapato, hatua mbalimbali za kiutawala ndani ya Mamlaka ya Mapato
zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu kabambe ya ufuatiliaji wa
makusanyo na kuanzisha ofisi mpya za kusimamia mapato katika maeneo mbalimbali
kwenye ngazi za wilaya na vituo vya miji. Hatua hii itajumuisha kusajili
walipakodi wapya, na kuhakikisha kunakuwa na ufuatiliaji wa walipakodi waliopo
ili walipe kodi stahiki.
Hatua
hizi za kiutawala kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi
cha shilingi milioni 80,108.18.
d) Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi,
SURA 82
73. Mheshimiwa Spika, napendekeza kupunguza Tozo ya
kuendeleza ufundi stadi (Skills Development Levy) kutoka kiwango cha sasa cha
asilimia 5 hadi asilimia 4.5 ili kuwapatia nafuu ya mzigo wa tozo waajiri na
kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari pasipo shuruti na hivyo kuongeza mapato
ya serikali katika muda wa kati. Hatua hii itapunguza mapato ya Serikali kwa
kiasi cha shilingi milioni 28,403.4
e) Sheria ya Magari (Kodi ya Usajili na
Uhamisho wa Umiliki), SURA 124
74. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
kwenye Sheria ya Magari (Kodi ya Usajili na Uhamisho wa Umiliki), SURA 124 kama
ifuatavyo: -
(i) Kufanya
marekebisho ya viwango vya usajili wa magari na pikipiki kutoka shilingi
150,000 hadi shilingi 250,000 kwa kila gari; na kutoka shilingi 45,000 hadi
shilingi 95,000 kwa kila pikipiki; na
(ii) Kupandisha
ada ya usajili wa namba binafsi za magari kutoka shilingi 5,000,000 hadi
shilingi 10,000,000 kwa kila baada ya miaka mitatu ili kuhuisha viwango hivyo
kulingana na thamani halisi ya fedha.
Hatua
hizi kwa pamoja zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
26,915.9.
f) Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, SURA
399; Sheria ya kodi ya Majengo ya Mamlaka ya Miji, SURA 289; Sheria ya Fedha ya
Serikali za Mitaa, SURA 290; Sheria ya Utawala wa Kodi ya mwaka 2015; na Sheria
ya Rufani za Kodi, SURA 408
75. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
katika Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, SURA 399, Sheria ya Kodi ya
Majengo ya Mamlaka ya Miji, Sura 289, Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa,
Sura 290, Sheria ya Utawala wa Kodi ya mwaka 2015 na Sheria ya Rufani za Kodi,
Sura 408 ili kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kukusanya kodi ya Majengo
ambapo hivi sasa kodi hiyo inakusanywa na Halmashauri. Lengo la
marekebisho haya, pamoja na mambo mengine, ni kama ifuatavyo;
(i) Kuiwezesha
Mamlaka ya Mapato kukadiria Kodi ya Majengo na kufanya uthamini wa majengo
husika;
(ii) Mamlaka
ya Mapato Tanzania kupewa uwezo wa kukusanya Kodi ya Majengo kwa kutumia
utaratibu wake wa kawaida kupitia sheria za kodi;
(iii) Kuweka
utaratibu wa namna ya kuhifadhi na kuwasilisha Kodi ya Majengo itakayokusanywa
na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwenye Halmashauri husika;
(iv) Kuwezesha
taratibu za kutatua migogoro itakayotokana na ukusanyaji wa Kodi ya
Majengo kusimamiwa na Sheria zinazotumika hivi sasa na Mamlaka ya Mapato
Tanzania katika kusimamia migogoro ya kodi; na
(v) Kufanya
maboresho katika misamaha ya Kodi ya Majengo ili majengo mengi zaidi yaingizwe
katika mfumo wa utozwaji kodi hiyo.
g) Sheria ya Msajili wa Hazina
(Mamlaka na Majukumu), SURA 370
76. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
kwenye Sheria ya Msajili wa Hazina (Mamlaka na Majukumu) SURA 370, ili kuzitaka
wakala na taasisi zote za usimamizi na udhibiti zilizo chini ya Msajili wa
Hazina kuchangia asilimia 15 ya mapato yake ghafi katika Mfuko Mkuu wa
Serikali. Taasisi hizo zitatangazwa kwenye Gazeti la Serikali. Aidha,
napendekeza kuiondoa katika orodha hiyo taasisi ya AICC na kuwekwa katika
orodha ya taasisi zinazotakiwa kutoa gawio (dividend) kwa Serikali kwa kuwa ni
taasisi inayofanya biashara.
h) Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki, ya mwaka 2004
77. Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki walifanya kikao cha maandalizi ya Bajeti (Pre-Budget
Consultations of EAC Ministers for Finance) jijini Arusha, Tanzania, kuanzia
tarehe 2 hadi 5 Mei, 2016. Katika kikao hicho, walikubaliana kwa pamoja kufanya
marekebisho ya viwango vya ushuru wa pamoja wa forodha (EAC Common External
Tariff “CET”) na kurekebisha Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,
(EAC-Customs Management Act, 2004) kwa mwaka wa fedha 2016/17 kama ifuatavyo: -
78. Mheshimiwa Spika, marekebisho ya viwango vya ushuru
wa pamoja wa forodha (EAC Common External Tariff “CET”) yaliyokubaliwa
yalizingatia kwa sehemu kubwa katika kuendeleza uchumi wa viwanda kwenye ukanda
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama ifuatavyo:-
(i) Tanzania
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye bidhaa ya
saruji inayotambuliwa katika HS Code 2523.29.00 kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Hatua hii inalenga katika kuhamasisha na kulinda uzalishaji wa saruji hapa
nchini ambao umekuwa ukiongezeka dhidi ya ushindani wa bei ya saruji
inayoingizwa nchini kutoka nje;
(ii) Kuongeza
Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 0 hadi asilimia 10 kwenye bidhaa za chuma
(flat rolled products of iron or non-alloy steel) zinazotambuliwa kwenye HS
Codes: (HS Code 7208.54.00; HS Code 7208.90.00; HS Code 7208.52.00; and, HS
Code 7208.53.00). Hatua hii inalenga katika kulinda uzalishaji wa bidhaa hizi
hapa nchini. Utafiti uliofanywa na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
unaonesha kuwa uzalishaji wa bidhaa za chuma umekuwa ukiongezeka na uwezo upo
wa kukidhi mahitaji. Hata hivyo kuna ushindani usio wa haki kutoka kwenye
bidhaa za vyuma zinazotoka nje ambazo ni za bei ya chini na zisizo na kiwango
bora;
(iii) Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwenye bidhaa za nondo
(bars and rods of iron and steel) kwa bidhaa zinazotambulika chini ya HS Codes:
(HS Code 7213.10.00; HS Code 7213.20.00; HS Code 7213.99.00; HS Code
7227.10.00; HS Code 7227.20.00; HS Code 7227.90.00; HS Code 7308.20.00; HS Code
7308.40.00; na HS Code 9406.00.90). Lengo la hatua hii ni kulinda uzalishaji wa
bidhaa za chuma zinazozalishwa na viwanda vya ndani dhidi ya ushindani wa
bidhaa zisizo na ubora na za bei ya chini kutoka nje ya nchi;
(iv) Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwenye bidhaa za
chuma “iron and steel products” zinazotambulika chini ya HS Code 7308.10.00
ambazo ni muhimu katika ujenzi wa madaraja (bridge and bridge sections);
(v) Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 kwa mwaka mmoja badala ya asilimia 25
kwenye “automotive bolts and nuts” zinazotambulika kwenye HS Code 7318.15.00.
Aidha, ushuru huu unapunguzwa kwa kuzingatia kwamba malighafi zinazotumika
kutengeneza bidhaa hizi hazizalishwi katika Nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki;
(vi) Kutoa
msamaha wa ushuru wa forodha kwa utaratibu wa duty remission kwa wazalishaji wa
“bolts and nuts” kwenye malighafi zinazotambulika chini ya HS Code 7228.30.00
na HS Code 7228.50.00 kwa kutoza kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 10.
Lengo la hatua hii ni kuwawezesha wazalishaji kupata malighafi hizo kwa gharama
nafuu kwa kuwa hazizalishwi katika ukanda wa Afrika Mashariki;
(vii) Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya kiwango cha sasa cha asilimia 10
kwenye nyavu za samaki zinazotambulika chini ya HS Code 5608.11.00. Hatua hii
inazingatia kuwa kuna watengenezaji wengi wa nyavu za aina hii katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki;
(viii) Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya kiwango cha sasa cha asilimia 10
kwenye bidhaa za “Oil and Petrol Filters” zinazotambulika kwenye HS Code
8421.23.00, na “intake air filters” zinazotambulika kwenye HS Code 8421.31.00.
Lengo la hatua hii ni kulinda uzalishaji wa bidhaa hizi zinazozalishwa na
viwanda vya ndani dhidi ya ushindani wa bidhaa zisizo na ubora na za bei rahisi
kutoka nje ya nchi;
(ix) Kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha na kutoza asilimia 0 kwa utaratibu wa duty
remission kwenye malighafi za kutengenezea “air filters” za magari kwa
wazalishaji wa hapa nchini;
(x) Kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha na kutoza asilimia 0 kwa utaratibu wa duty remission
kwenye malighafi (splints) za kutengenezea vibiriti zinazotambulika chini ya HS
Code 4421.90.00. Hatua hii imezingatia kwamba hakuna misitu ya kutosha na yenye
mbao za kukomaa zinazokidhi mahitaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(xi) Nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki kupunguza msamaha wa Ushuru wa Forodha hatua kwa
hatua kwenye Sukari (sugar and sugar confectionery) kutoka kiwango cha sasa
ambapo waagizaji wa sukari ya viwandani hulipa asilimia 10. Kutokana na
kupunguza msamaha huo, waagizaji watalipa ushuru zaidi hatua kwa hatua.
Upunguzaji wa msamaha utakuwa kama ifuatavyo: Mwaka 2016/17 kiwango kitakuwa
asilimia 15, 2017/18 kiwango kitakuwa cha asilimia 20, 2018/19 kiwango kitakuwa
cha asilimia 25. Hatua hii inachukuliwa kwa kuwa kiwango cha sasa cha asilimia
10 kinadidimiza viwanda vyetu vya ndani na pia ni chachu ya matumizi mabaya ya
misamaha husika;
(xii) Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 10 za sasa kwa bidhaa
zinazotambulika chini ya HS Code 7612 “Aluminium Milk Cans”. Hizi ni bidhaa
zilizokamilika tayari kwa kutumika hivyo zinatakiwa kutozwa ushuru wa asilimia
25 unaostahili kwa bidhaa za namna hiyo. Lengo la hatua hii ni kulinda
wazalishaji wa ndani wenye uwezo wa kuzalisha bidhaa hizi kwenye nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(xiii) Kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha na kutoza asilimia 0 malighafi zinazoagizwa na
wazalishaji wa Aluminium cans zinazotambulika chini ya HS Codes 7606.12.00 na
HS Codes 7606.92.00. Hatua hii inalenga katika kuhamasisha uzalishaji wa
“aluminium cans” katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(xiv) Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwenye ngano (Wheat
grain) inayotambuliwa chini ya HS Code 1001.99.10 na HS Code 1001.99.90 kwa
mwaka mmoja. Hatua hii imezingatia kwamba nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
hazina uwezo wa kuzalisha ngano ya aina hii na kuweza kutosheleza mahitaji.
Aidha, itatoa unafuu kwa wazalishaji wa bidhaa na vyakula vinavyotumia ngano na
kuimarisha utulivu wa bei ya bidhaa za ngano;
(xv) Kuongeza
kiwango maalumu cha ushuru kwenye mitumba ya nguo na viatu kutoka kiwango cha
sasa cha dola za kimarekani 0.2 kwa kilo hadi dola 0.4 kwa kilo. Hatua hii
imechukuliwa ili kudhibiti hatua kwa hatua uingizaji nchini wa nguo za mitumba
ambazo zimeonekana kuwa siyo salama kwa afya za watu wetu. Aidha, Nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kuzuia kabisa uingizaji
wa bidhaa hizi baada ya miaka mitatu kuanzia sasa. Hata hivyo Nchi hizi
zimekubaliana kuweka mikakati ya kuimarisha na kuhamasisha uzalishaji wa nguo
na viatu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kukidhi mahitaji. Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji tayari imeandaa mikakati madhubuti ya kuendeleza
sekta za ngozi na nguo;
(xvi) Kuendelea
kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 25 au kiwango maalum cha dola za
kimarekani 200 – kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa kila tani moja ya ujazo
(metric ton) kwenye bidhaa za chuma (iron and iron-alloy steel) kwa mwaka
mmoja, zinazotambuliwa katika HS Codes: HS Codes 7210.41.00; HS Codes
7210.49.00; HS Codes 7210.61.00; HS Codes 7210.69.00; HS Codes 7210.70.00; HS
Codes 7210.90.00; HS Codes 7212.30.00; and HS Codes 7212.40.00. Lengo la hatua
hii ni kulinda uzalishaji wa bidhaa za chuma zinazozalishwa na viwanda vya
ndani dhidi ya ushindani wa bidhaa zisizo na ubora kutoka nje ya nchi. Utafiti
uliofanywa na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki umeonesha kuwa kumekuwa na
ongezeko kubwa la uzalishaji wa bidhaa za vyuma kupita mahitaji ya soko katika
soko la dunia. Hali hiyo imesababisha kushuka sana kwa bei na hivyo kuathiri
viwanda vyetu kutokana na ushindani wa bidhaa hizo kutoka nje. Hatua hii ya
kuweka viwango maalum vya kodi ni muhimu kulinda viwanda na bidhaa zetu
(anti-dumping measure);
(xvii) Kuendelea
kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 25 au kiwango maalum cha dola za
kimarekani 200 – kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa mwaka mmoja kwa kila
tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma (Flat-rolled products of
bars, rods, sections, angles, shapes, and related products) zinazotambuliwa
katika HS Codes: HS Codes 7214.10.00; HS Codes 7214.20.00; HS Codes 7214.30.00;
HS Codes 7214.91.00; and HS Codes 7214.99.00. Lengo la hatua hii ni kulinda
uzalishaji wa bidhaa za chuma zinazozalishwa na viwanda vya ndani dhidi ya
ushindani wa bidhaa zisizo na ubora kutoka nje ya nchi;
(xviii) Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au kiwango maalum cha dola za
kimarekani 200 – kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa mwaka
mmoja kwa kila tani moja ya ujazo “metric
ton’ kwenye bidhaa za chuma (steel reinforcement bars,
angles, sections zinazotambuliwa chini ya HS Codes: 7216.10.00; HS
Codes 7216.21.00; HS Codes 7216.22.00; and HS Codes 7216.50.00.). Lengo la hatua
hii ni kulinda uzalishaji wa bidhaa za chuma zinazozalishwa na viwanda vya
ndani dhidi ya ushindani wa bidhaa zisizo na ubora kutoka nje ya nchi;
(xix) Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye mafuta ghafi ya
kula (crude edible oil) yanayotambulika katika HS Code 1511.10.00 kwa mwaka
mmoja. Hatua hii inalenga katika kuhamasisha kilimo cha mbegu za mafuta hapa
nchini na kukuza viwanda vya kutengeneza mafuta ya kula. Aidha, Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeandaa mkakati maalum wa kuendeleza viwanda
vya kuzalisha mafuta yanayotokana na mbegu zinazozalishwa hapa nchini na
kutumia fursa soko kubwa lililopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo
Tanzania inayo nafasi ya kuweza kuongeza uzalishaji wa mbegu za mafuta;
(xx) Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwa bidhaa za karatasi
zinazotambulika kwenye HS Codes: HS Codes 4804.11.00; HS Codes 4804.19.10; HS
Codes 4804.19.90; HS Codes 4804.21.00; HS Codes 4804.29.00; HS Codes
4804.31.00; HS Codes 4804.39.00; HS Codes 4804.41.00; HS Codes 4805.59.00; HS
Codes 4805.11.00; HS Codes 4805.12.00; HS Codes 4805.19.00; HS Codes
4805.24.00; HS Codes 4805.25.00; HS Codes 4805.30.00; HS Codes 4805.91.00, na
HS Codes 4805.92.00. Hatua hii inachukuliwa ili kulinda viwanda vya hapa nchini
vinavyozalisha karatasi za aina hiyo na ajira;
(xxi) Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au kiwango maalum cha dola za
kimarekani 200 – kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa mwaka mmoja kwa kila
tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za nondo zinazotambulika kwenye
HS Codes HS Codes 7228.10.00; HS Codes 7228.20.00; HS Codes 7228.30.00; HS
Codes 7228.40.00; HS Codes 7228.50.00; HS Codes 7228.60.00; HS Codes7228.70.00; na HS Codes 7228.80.00. Lengo
ni kulinda viwanda vya ndani kutokana na ushindani wa bidhaa kama hizo
zinazoagizwa nje; na
(xxii) Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au kiwango maalum cha dola za
kimarekani 200 - kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa mwaka mmoja kwa kila tani
moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma zinazotambulika kwenye HS
Codes 7212.40.00; HS Codes 7215.10.00; HS Codes 7215.50.00; HS Codes
7215.90.00; HS Codes 7216.61.00; HS Codes 7216.69.00; HS Codes 7216.91.00; na
HS Codes 7216.99.00.
79. Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki walifanya pia marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki, (EAC-Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo: -
(i) Kufanya
marekebisho katika Jedwali la Tano (5) la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki linalotoa msamaha wa ushuru wa forodha ili kuongeza vifaa vya
majokofu yanayotumika katika kuhifadhi maiti yanayotambuliwa chini ya HS Code
8418.69.90 kwa matumizi ya hospitali na mamlaka za miji (city councils);
(ii) Kufanya
marekebisho katika Jedwali la Tano (5) la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki (Chapters 84 and 69) linalotoa msamaha wa ushuru wa forodha
ili kuongeza vifaa vinavyotumika kwenye hospitali kuteketeza na kuchoma uchafu
(incinerator’s equipments and materials used in hospitals to burn waste);
(iii) Kufanya
marekebisho katika Jedwali la Tano (5) la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki ili kuondoa msamaha wa ushuru wa forodha unaotolewa kwenye
sare za wafanyakazi wa hospitali. Msamaha huu unaondolewa kwa kuwa sare
hizi zinaweza kuzalishwa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(iv) Kusamehe
Ushuru wa Forodha kwa kutumia utaratibu wa “Duty remission” kwa wazalishaji wa
hapa nchini wa malighafi zinazotumika kutengeneza betri zinazofahamika kama
“deep cycle batteries”. Hatua hii inalenga katika kuhamasisha uzalishaji wa
viwanda vya ndani kwa kuwa deep cycle batteries zinazoagizwa kutoka nje ya nchi
zimesamehewa ushuru kupitia Jedwali la Tano (5) la Sheria ya Forodha ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki;
(v) Kufanya
marekebisho katika Jedwali la Tano (5) la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki linalotoa msamaha wa ushuru wa forodha ili kujumuisha chupa
zinazotumika kwa ajili ya kukusanya damu kwenye hospitali (blood collection
tubes); na
(vi) Kusamehe
Ushuru wa Forodha kwa kutumia utaratibu wa “Duty remission” kwa malighafi zinazotumika
kuzalisha vifaa vya nishati ya umeme wa jua (Solar equipments).
Hatua
zote za Ushuru wa Forodha kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato kwa kiasi cha
shilingi milioni 42,850.6.
i) Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya
Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali
80. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
mengine madogo madogo yasiyo ya kisera na ya kiuandishi katika Sheria
mbalimbali za kodi pamoja na sheria nyingine ili ziwe sanjari na azma ya
kurahisisha utekelezaji wake. Marekebisho hayo yataainishwa katika muswada wa
Sheria ya Fedha 2016.
81. Mheshimiwa Spika, ili kurahisisha utekelezaji wa
Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015, na kuleta uwajibikaji katika utekelezaji wa
Bajeti ya Mfuko wa Mahakama na Mfuko wa Bunge napendekeza kufanya marekebisho
yafuatayo:-
(i) Kurekebisha
kifungu cha 29 kifungu kidogo cha 3 cha Sheria ya Utawala wa Bunge, SURA 115
(The National Assembly Administration Act, CAP 115) ili kubainisha kuwa bajeti
ya Mfuko wa Bunge itawasilishwa Bungeni na Waziri mwenye dhamana na masuala ya
Bunge. Hivi sasa Sheria hii imeweka sharti kwa Waziri mwenye dhamana na masuala
ya fedha kuwasilisha Bungeni Bajeti ya Mfuko wa Bunge; na
(ii) Kurekebisha
kifungu cha 59 kifungu kidogo cha 3 cha Sheria ya Utawala wa Mahakama, SURA 237
(The Judiciary Administraion Act, CAP 237) ili Bajeti ya Mfuko wa Mahakama
iwasilishwe Bungeni na Waziri mwenye dhamana na masuala ya mahakama. Kifungu
hiki kwa sasa kimeweka sharti kwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha
kuwasilisha Bungeni Bajeti ya Mfuko wa Mahakama.
j) Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali
zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea
82. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya
viwango vya ada na tozo mbali mbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara
zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa uchumi.
Aidha, napendekeza kufuta baadhi ya ada na tozo ambazo zimeonekana kuwa kero
kwa wananchi na kikwazo katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara hapa
nchini. Tozo na ada ninazopendekeza kuzifuta ni kama ifuatavyo:
(i) Mamlaka ya Chakula na Dawa (Tanzania Foods
and Drugs Authority – TFDA):
a) Kibali cha kusafirisha chakula nje ya nchi
kwa shilingi 50,000;
b) Kushikilia dawa za binadamu na mifugo
zinazotengenezwa na viwanda vya ndani kwa shilingi 100,000;
c) Kudurufu cheti cha dawa za binadamu na
mifugo zinazotengenezwa na viwanda vya ndani kwa Dola za Kimarekani 50;
d) Kudurufu cheti cha dawa za binadamu na
mifugo zinazotengenezwa na viwanda vya nje ya nchi kwa Dola za Kimarekani 100;
e) Tathimini ya matangazo ya bidhaa
zinazotengenezwa nchini kwa Dola za Kimarekani 50;
f) Matangazo yanayofanyiwa tathimini fupi kwa
bidhaa zinazotengenezwa nchini kwa Dola za Kimarekani 25;
g) Kudurufu cheti cha usafi wa chakula, dawa
na vifaa tiba vinavyotengenezwa nje ya nchi kwa Dola za Kimarekani 100;
h) Kudurufu cheti cha vifaa tiba
vinavyotengenezwa ndani ya nchi kwa Dola za Kimarekani 30;
i) Kudurufu cheti cha dawa zinazotengenezwa
nchini kwa Dola za Kimarekani 50;
j) Kushikilia vitendanishi vinavyotengenezwa
nje ya nchi katika rejesta kwa Dola za Kimarekani 150;
k) Kushikilia vipodozi vinavyotengenezwa ndani
ya nchi katika regesta kwa shilingi 30,000;
l) Ukaguzi wa kiwanda cha dawa cha ndani ya
nchi kabla ya kusajiliwa kwa Dola za Kimarekani 250;
m) Wawakilishi wa makampuni ya dawa ya nje ya
nchi kwa Dola za Kimarekani 1,000;
n) Malighafi za vipodozi zinazoingizwa nchini
kwa shilingi 50,000,000;
o) Malighafi za dawa zinazoingizwa nchini kwa
shilingi 100,000,000;
p) Kibali cha hospitali kununua dawa zenye
madhara ya kulevya kutoka bohari kwa Dawa ya shilingi 10,000;
q) Ada ya uingizaji nchini wa dawa zenye
madhara ya kulevya ya shilingi 50,000;
r) Cheti cha kusafirisha bidhaa nje ya nchi
kwa shilingi 50,000;
s) Cheti cha utambuzi wa dawa inayosafirishwa
nje ya nchi kwa 50,000;
t) Ukaguzi wa kiwanda kidogo kipya cha
kusindika chakula kwa shilingi 100,000;
u) Cheti cha kuteketeza bidhaa;
v) Cheti cha Afya kwa ajili ya kusafirisha
bidhaa nje ya nchi kwa shilingi 50,000; na
w) Kibali cha kufanya maonyesho ya biashara ya
bidhaa inayodhibitiwa kwa shilingi 200,000.
(ii) Bodi ya Pamba:
a) Mchango wa mwenge kwa kila kiwanda cha
kuchambua pamba wa shilingi 450,000; na
b) Ada ya vikao vya Halmashauri za wilaya
wanapojadili maombi mbalimbali ya wafanyabiashara wa pamba ya shilingi 250,000.
(iii) Bodi ya Chai: Kodi ya moto na uokoaji.
(iv) Bodi ya Kahawa: Ada ya leseni ya
kusindika kahawa ya Dola za Kimarekani 250.
(v) Bodi ya Korosho:
a) Ushuru wa chama kikuu cha ushirika wa
shilingi 20 kwa kilo;
b) Ushuru wa kusafirisha korosho wa shilingi
50 kwa kilo;
c) Gharama za mtunza ghala kwa shilingi 10 kwa
kilo;
d) Kikosi kazi kwa ajili ya ufatiliaji wa
masuala mbalimbali kwa kuchangia shilingi 10 kwa kilo; na
e) Makato ya unyaufu.
83. Mheshimiwa Spika, napenda nilifahamishe Bunge lako
Tukufu pamoja na wananchi kwamba, hatua ninazopendekeza za kufuta tozo na ada
nilizozifanya ni za awali tu wakati Serikali inaendelea kufanya uchambuzi na
tathmini ya kina kuhusu tozo na ada zinazotozwa na mashirika, taasisi na wakala
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Serikali za Mitaa. Hatua hizi ni endelevu katika
kuhakikisha kuwa tunaboresha mazingira ya kufanya biashara ili nchi yetu iweze
kuwa na nafasi nzuri ya kiushindani katika biashara na kuvutia uwekezaji.
Aidha, lengo la hatua hizi ni pamoja na kuondoa kero kwa wananchi na kuwapa
unafuu katika uendeshaji wa shughuli za kiuchumi.
84. Mheshimiwa Spika, napendekeza pia kurekebisha baadhi
ya viwango vya ada na tozo mbalimbali kama zitakavyoainishwa kwenye Sheria ya
Fedha 2016 na nyingine kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali (GNs) na Mawaziri
wenye dhamana na ada na tozo hizo.
k) Kodi na Tozo Kwenye Bidhaa za Mafuta ya
Petroli
85. Mheshimiwa Spika, kwa muda sasa bei ya mafuta
(petroli, dizeli na ya taa) imekuwa ikishuka katika soko la dunia, hali ambayo
imesaidia kuleta unafuu wa gharama katika shughuli za kiuchumi hususan kwa
wananchi masikini maana bei za mafuta haya zinagusa kila mtu. Hivyo, Serikali
imeamua kuwa Ushuru wa Barabara, Ushuru wa Petroli na Ushuru wa Bidhaa kwenye
mafuta ya petroli utabaki kama ilivyo sasa. Hivyo, Mfuko wa barabara na Mamlaka
ya Usambazaji Umeme Vijijini watumie fedha hizi vizuri.
l) Misamaha ya Kodi kwa Majeshi ya Ulinzi na
Usalama
86. Mheshimiwa Spika, kwa kipindi kirefu Serikali
imekuwa ikitoa misamaha ya kodi (Ushuru wa Bidhaa, Kodi ya Ongezeko la Thamani
na Ushuru wa Forodha) kwa majeshi ya Ulinzi na Usalama kupitia kwenye migahawa
na maduka maalum ambayo yanauza bidhaa mbalimbali kwa mahitaji ya askari.
Katika kufanya hivyo, kumekuwa na changamoto ya kuwepo kwa matumizi mabaya ya
misamaha hiyo. Aidha, kutokana na hali hiyo ya upotevu wa mapato, Nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeondokana na utaratibu huu isipokuwa Rwanda na
Tanzania ambazo zinatoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwa Majeshi ya Ulinzi na
Usalama.
87. Mheshimiwa Spika, katika kikao cha Mawaziri wa Fedha
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Maandalizi ya Bajeti kwa mwaka 2015/16,
Serikali ya Tanzania ilitakiwa kuangalia njia mbadala ya kutoa unafuu wa
gharama kwa majeshi yake badala ya utaratibu wa kutoa misamaha. Ili kuendelea
kutoa huduma kwa majeshi hayo pasipo kupoteza mapato ya Serikali, napendekeza
kuwapatia posho majeshi yetu ya Ulinzi na Usalama ili kuwawezesha kununua
mahitaji yao wenyewe. Dhamira ya hatua hii ni kusitisha msamaha wa kodi kwa
majeshi ili kuondoa uvujaji mkubwa wa mapato na wakati huo huo, kuendelea
kuwapatia askari wetu mahitaji yao muhimu kwa utaratibu mzuri zaidi. Aidha,
lengo la hatua hii ni kuhakikisha kuwa motisha unaotolewa unawanufaisha
walengwa, yaani askari, badala ya wajanja wachache kuendelea kunufaika na
misamaha hiyo.
Tarehe
ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi
88. Mheshimiwa Spika, Hatua hizi za kodi
zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2016, isipokuwa pale
ilipoelezwa vinginevyo.
V. SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2016/17
89. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za uchumi jumla
pamoja na misingi na sera za bajeti kwa mwaka 2016/17, Sura ya Bajeti inaonesha
kuwa jumla ya shilingi trilioni 29.54 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika
katika kipindi hicho. Bajeti ya mwaka 2016/17 inatarajiwa kuwa na ongezeko la
jumla ya shilingi trilioni 7.04 sawa na asilimia 31.1 ikilinganishwa na Bajeti
ya mwaka 2015/16 ya shilingi trilioni 22.49.
90. Mheshimiwa Spika, Serikali inalenga kukusanya mapato ya
ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri ya jumla ya shilingi trilioni 18.46
sawa na asilimia 62.5 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, mapato ya kodi ni
shilingi trilioni 15.11 sawa na asilimia 13.8 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato
yasiyo ya kodi na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri ni shilingi trilioni
2.69 na shilingi bilioni 665.4 kwa mtiririko huo. Makisio ya mapato ya kodi na
yasiyo ya kodi yameongezeka kwa kuwa kuna viashiria vingi vinavyoonesha kwamba
TRA kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi zinazokusanya maduhuli wana uwezo wa
kukusanya kiasi hiki cha mapato. Hivyo, Serikali itasimamia kwa karibu na
kuziba mianya yote ya uvujaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ili
kuhakikisha kuwa malengo ya ukusanyaji yanafikiwa.
91. Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa
kuendelea kutupatia misaada na mikopo ya jumla ya shilingi trilioni 3.60 ambayo
ni asilimia 12 ya bajeti yote. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni
2.75 ni misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo; shilingi bilioni
372.1 ni misaada na mikopo kwa mifuko ya pamoja ya kisekta; na shilingi bilioni
483 ni misaada na mikopo ya kibajeti (GBS).
92. Mheshimiwa Spika, ili kuziba nakisi ya bajeti, katika
mwaka 2016/17 Serikali inatarajia kukopa jumla ya shilingi trilioni 7.48 kutoka
katika vyanzo vya ndani na nje. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 5.37
zinategemewa kukopwa katika soko la ndani kwa ajili ya kulipia hatifungani na
dhamana za Serikali zinazoiva pamoja na mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia
miradi ya maendeleo na kulipia malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa. Aidha, ili
kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu na kuhakikisha inatekeleza Mpango wa
Pili wa Maendeleo kikamilifu, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 2.10
kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara.
93. Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya jitihada kubwa za kuongeza
ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kugharamia, pamoja na mambo mengine, miradi
ya maendeleo. Utekelezaji wa miradi hiyo pia hutegemea mikopo ya nje ya
kibiashara ambayo upatikanaji wake hutegemea hali ya soko la fedha duniani.
Katika mwaka 2016/17, kuna miradi mikubwa hususan ujenzi wa reli ya kati kwa
kiwango cha standard gauge na uimarishaji wa bandari ambayo
matayarisho yake yanahitaji muda na umakini mkubwa hasa uhakika wa upatikanaji
wa fedha. Hivyo, utekelezaji wa miradi hii unatarajiwa kuanza katika nusu ya
pili ya mwaka wa fedha 2016/17 baada ya kutathmini hali ya upatikanaji wa fedha
zaidi na kukamilisha maandalizi ya msingi ikiwa ni pamoja na kumpata mkandarasi
na kuingia mkataba. Matarajio ya Serikali ni kuwa mkandarasi atakabidhiwa eneo
(site) ndani ya miezi tisa (9) ya kwanza ya 2016/17.
94. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi, katika mwaka
2016/17 Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 29.54 kwa matumizi
ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 17.72 zimetengwa
kwa ajili ya matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo yatakuwa shilingi
trilioni 11.82 sawa na asilimia 40 ya bajeti yote ambapo kiasi cha shilingi
trilioni 8.70 ni fedha za ndani na shilingi trilioni 3.12 ni fedha za nje.
95. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama
ulivyoelezwa hapo juu, sura ya bajeti kwa mwaka 2016/17 ni kama inavyooneshwa
katika Jedwali, ukurasa wa 92 wa kitabu cha hotuba hii.
Mfumo wa Bajeti wa Mwaka
2016/17
VI. HITIMISHO
96. Mheshimiwa
Spika, wananchi wetu wengi wamechoka na adha ya umaskini:
Watanzania wanataka kipato cha kuweza kukidhi mahitaji yao ya msingi. Wananchi
wanataka huduma bora zaidi hususan upatikanaji wa maji, elimu, afya, umeme na
makazi; akina mama wamechoka kutembea na ndoo za maji kichwani; watoto wetu
shuleni wamechoka kukaa chini na kugombania matundu machache ya vyoo; vijana
wanataka ajira; kilio cha mauaji ya kikatili ya albino ni fedheha kwa nchi
yetu; wananchi bado wananyimwa haki zao kutokana na kukithiri kwa rushwa;
Watanzania wanataka nchi yenye neema; Watanzania wanataka Serikali inayofanya
kazi kwa ufanisi; Watanzania wanataka mazingira safi na endelevu; Watanzania
wanataka miundombinu na usafiri wa kisasa na salama; Watanzania wanataka miji
na makazi yaliyopimwa na yaliyopangwa vizuri; na pia Watanzania wanapenda
amani, utulivu, utangamano na furaha. Hata hivyo, napenda nisisitize kuwa
Tanzania mpya ambayo wote tunaitamani iko mikononi mwetu!!
97. Mheshimiwa
Spika, katika kuhitimisha hotuba yangu napenda kuwaambia Watanzania
wenzangu siri ya maendeleo. Siri ya kuifikia Tanzania mpya tunayoitamani!
Kwanza, maendeleo hayaji hivi hivi! Maendeleo yanataka dhamira na utashi,
juhudi na maarifa; maendeleo yanataka vitendo, siyo maneno! Maendeleo yanataka
pawepo dira ya kutuongoza tunakotaka kwenda. Ili kufanikiwa, lazima kuyafahamu
vizuri mazingira tulipo na njia ya kupita, hususan fursa na hatari zilizo mbele
yetu. Maendeleo yanataka mwelekeo (focus), vipaumbele, malengo na viashiria vya
hatua iliyofikiwa; maendeleo yanahitaji nidhamu ya hali ya juu hususan katika
matumizi ya rasilimali (watu, fedha, muda, vitendea kazi na mali). Maendeleo
yanataka usimamizi makini wa utekelezaji. Hivyo, maendeleo yanataka hatua kali
za kumwajibisha yeyote anayekwamisha na kuhujumu juhudi zetu kwa kutotimiza
wajibu, uzembe, rushwa, ubadhirifu n.k. Maendeleo yanahitaji kujinyima au
kujitoa (sacrifice) na kwa maana hiyo yafaa Watanzania tujitafakari juu ya
kujengeka kwa utamaduni wa kuchangishana michango mingi ya sherehe za anasa na
badala yake tujielekeze kusaidiana katika masuala ya maendeleo kama ada za
shule, gharama za matibabu n.k. Aidha, maendeleo yanahitaji muendelezo wa hatua
stahiki badala ya kurukia mambo mapya kabla ya kukamilisha yaliyoanza
kutekelezwa (consistency of action); Maendeleo yanapatikana kwa
kufanya kazi kwa bidii (hard work). Hivyo, maendeleo hayatakuja kwa
kucheza pool table na kunywa viroba muda wote; maendeleo
yanapatikana kwa kuthubutu (boldness) na kujiamini (self confidence) na
hatimaye kuamua kujitegemea.
98. Mheshimiwa
Spika, niruhusu pia niseme juu ya utegemezi kwa misaada kutoka
kwa wahisani. Tangu Uhuru wafadhili wameendelea kutupatia misaada ambayo imetoa
mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu. Hata hivyo, pamoja na kuwa lengo
la misaada ni kujazia uwezo wa taifa kutekeleza miradi ya maendeleo au
kukabiliana na maafa, ni vizuri watanzania wenzangu tukaelewa kuwa kwa upande
mwingine misaada inaweza kuwa sumu ya maendeleo! Misaada inaweza kuwa uchochoro
wa sera na miradi mibovu, inapoteza kujiamini na masharti yanayoambatana na
misaada yanapunguza uhuru wa kujiamulia mambo. Misaada pia inaweza kuchochea
rushwa na kuzorotesha jitihada za ndani hususan za ukusanyaji mapato.
Mwanazuoni anayeitwa Sebastian Edwards katika kitabu chake –Toxic Aid:
Economic Collapse and Recovery in Tanzania (2014)amefichua ukweli huo kwa
maneno yafuatayo, nanukuu:-
“After analysing in great depth Tanzania’s history during its
first two decades as an independent nation, it is clear to me that the official
aid community had a major responsibility in one of the most colossal collapses
of a poor country in the history of the modern world. When one adds and
subtracts everything – the misguided policies, the blunders, the growing
corruption, and the socially worthwhile projects- the balance is hugely
negative. The inescapable conclusion of that exercise is that
during 1961-81 aid was worse than ineffective; it was toxic”! Mwisho
wa kunukuu.
Hivyo, ni muhimu sana kama taifa tutambue jambo hili na tufanye
kila linalowezekana kupunguza utegemezi kwa misaada ya wahisani kwa kulinda
utulivu wa uchumi, kujenga uwezo wetu wenyewe hususan kukuza sekta ya viwanda
ili kupanua wigo wa kukusanya zaidi mapato ya ndani na kwa ufanisi zaidi. Ni
muhimu sana tuweke msukumo zaidi wa kukuza na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje
pamoja na kuimarisha biashara katika mahusiano yetu na nchi
rafiki.
99. Mheshimiwa
Spika, jambo la mwisho na muhimu sana ni kuwa maendeleo endelevu yanapatikana
haraka katika mazingira ya amani na usalama. Hivyo ni lazima tunu ya amani
katika nchi yetu ilindwe kwa nguvu zote.
100. Mheshimiwa
Spika, Rai yangu kwa watanzania: Mungu ametujalia rasilimali nyingi;
Mama zetu walizaa na wanaendelea kuzaa watoto wenye akili timamu, wabunifu na
wenye uwezo wa kutatua changamoto kuu na vikwazo kwa maendeleo ya Tanzania
mpya. Hivyo, tukiongozwa na uzalendo, uchungu wa nchi hii na uthubutu wa Rais
wetu Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli, lazima sasa tudhamirie kuigeuza
Tanzania kuwa nguvu kuu ya kiuchumi katika kanda hii ya Afrika (economic power
house) katika kipindi cha miaka kumi ijayo. Tukiwa na nia moja, inawezekana, na
hakika Mungu yuko upande wetu.
101. Mheshimiwa
Spika, ningependa pia kuchukua nafasi hii kuwakumbusha viongozi
wenzangu na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa matumizi ya muda ambao ni
rasilimali muhimu katika maendeleo ya Taifa letu. Watanzania wengi tunatumia
muda vibaya kwa mambo yasiyokuwa na tija na hatuzingatii muda katika kutimiza
majukumu yetu. Kwa upande wa watumishi wa umma, kumekuwa na mazoea ya kutumia
muda mrefu kwenye vikao na mikutano na kuacha majukumu ya msingi ya kuwahudumia
wananchi. Vilevile, wananchi hasa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa
wamekuwa wakitumia muda mwingi wa kazi kufanya mambo yasiyokuwa na manufaa kwao
binafsi na Taifa kwa ujumla, hususan; unywaji wa pombe, kucheza pool,
uzururaji, kamari, sinema za mitaani, kukaa vijiweni na kupoteza muda mwingi
kwenye mitandao ya kijamii. Hivyo, natoa rai kwa watanzania wote kuthamini
matumizi mazuri ya muda kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuchochea maendeleo yetu
binafsi na Taifa kwa ujumla.
102. Mheshimiwa
Spika, Ninapoelekea kumalizia hotuba hii, napenda kusisitiza
mambo yafuatayo ambayo yanalenga kuimarisha ukusanyaji wa mapato na usimamizi
wa matumizi ili kuweza kutekeleza bajeti kama ilivyopangwa:
Kwanza, Serikali itaongeza msukumo katika matumizi ya
mashine za EFD ili kuhakikisha kila mfanyabiashara anatoa risiti za mashine za
EFD na wanachi wanadai risiti pale wanapofanya manunuzi ya bidhaa au huduma.
Katika kutimiza azma hii Wizara yangu itaunda Kikosi Maalum cha kufuatilia
utekelezaji wa agizo hili katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ili kuhakikisha
wale wote wataokiuka utaratibu huu wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.
Ninapenda kutoa rai kwa viongozi wote, hususan Waheshimiwa Mawaziri, Wabunge,
Madiwani na Viongozi wa Dini kuwa mfano wa kuigwa kwa wananchi wetu kwa kuhakikisha
kuwa tunadai risiti za EFD pale tunaponunua bidhaa au huduma. Aidha, viongozi
wote mnaombwa kuhamasisha wananchi kudai risiti za EFD. Kila asiyetoa risiti na
asiyedai risiti ajue anatenda kosa na anasaliti jitihada zetu za kuijenga
Tanzania mpya.
Pili, vituo vyote vya kuuzia mafuta ya petroli vinaagizwa
kukamilisha ufungaji wa mashine za EFD kwenye pampu za kuuzia mafuta hayo
ifikapo tarehe 1 Oktoba, 2016 ili kuhakisha kuwa Serikali inakusanya kodi
stahiki. Serikali itafanya ukaguzi kwenye vituo vyote vya mauzo ya mafuta hapa
nchini na kuchuka hatua za kisheria kwa wale watakaokaidi agizo hili.
Tatu, katika kudhibiti misamaha ya kodi inayotolewa kwa
wafanyabiashara, watumishi wa umma, mashirika ya dini na taasisi zisizo za
kiserikali, kuanzia mwaka ujao wa fedha watalazimika kulipa kodi kwanza kwa
bidhaa watakazoagiza. Kodi hiyo itarejeshwa kwa wanufaikaji baada ya ukaguzi
kufanyika na kujiridhisha kuwa bidhaa hizo zimetumika kwa malengo
yaliyokusudiwa. Aidha, Serikali itawataka wanufaika kuwasilisha maombi
yao Wizara ya Fedha na Mipango kabla ya kuagiza bidhaa husika ili kupata kibali
cha uagizwaji wa bidhaa hizo.
Nne, Maafisa Maasuuli wote wanaagizwa kutumia vifaa na
mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato unaofanywa na Serikali Kuu,
Mamlaka za Serikali za Mitaa, na Mashirika na Taasisi za Umma ili kuongeza
ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato. Aidha, kodi na tozo hizo
zitakazokusanywa zipelekwe benki ndani ya masaa 24.
Tano, kuanzia mwaka ujao wa fedha utaratibu wa kubakiza
sehemu ya makusanyo, yaani mfumo wa retention umefutwa.
Taasisi zote zilizokuwa zikitumia mfumo huo zitalazimika
kuwasilisha mapato yote kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Utoaji wa fedha kutoka
Hazina kwenda kwenye taasisi hizo utazingatia utaratibu wa kawaida kulingana na
bajeti iliyoidhinishwa.
Sita, Maafisa Masuuli wanaelekezwa kuzingatia agizo la
Serikali la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima katika maeneo yaliyoainishwa
ikiwa ni pamoja na: safari za nje ya nchi, mafunzo nje ya nchi, posho za vikao,
warsha na makongamano, sherehe na maadhimisho ya kitaifa, ununuzi wa samani,
ununuzi na uendeshaji wa magari, n.k. ili kupata fedha zaidi na kuzielekeza
kwenye miradi ya maendeleo na kutatua kero za wananchi.
Saba, Waajiri wanatakiwa kuwasilisha kodi ya mapato ya
wafanyakazi – PAYE pamoja na michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa
wakati. Aidha, kwa wale wenye malimbikizo ya PAYE na michango, wanaagizwa
kuwasilisha malipo hayo kabla ya tarehe 31 Desemba, 2016 vinginevyo hatua
stahiki zitachukuliwa dhidi yao. Maafisa Masuuli, Wakuu wa Taasisi, Mashirika
na Kampuni Binafsi wanaagizwa kusimamia utekelezaji wa agizo hili.
Nane, Maafisa Masuuli wanaelekezwa kutumia mfumo wa nakala
laini (soft copy) katika kusambaza nyaraka mbalimbali za Serikali zinazozidi
kurasa 50 isipokuwa kwa mafungu yanayotakiwa kusambaza nakala ngumu (hard copy)
kutokana na matakwa ya kikanuni/kisheria. Hatua hii inalenga kupunguza matumizi
makubwa ya gharama za kuchapisha na kudurufu nyaraka hizo na kulinda mazingira.
Tisa, katika mwaka wa fedha 2016/17 madai yote yanayohusu
huduma za umeme, maji na simu yatalipwa moja kwa moja (centrally)
na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kutumia bajeti za mafungu husika. Aidha,
Maafisa Masuuli wanaagizwa kulipa kwa wakati ankara za huduma za umeme, maji na
simu ili kuepuka malimbikizo ya madai mapya.
Kumi, Maafisa
Masuuli wanaagizwa kufanya ununuzi kwa kutumia Hati za Ununuzi - LPOs
zitokanazo na mfumo wa IFMS. Aidha, wazabuni na watoa huduma wanaelekezwa
kuhakikisha wanapatiwa Hati za Ununuzi - LPOs zitokanazo na mfumo wa
IFMS. Hivyo, kuanzia mwaka 2016/17 Hati za ununuzi zitakazotolewa nje ya
utaratibu huu hazitatambuliwa kama hati halali za ununuzi.
103. Mheshimiwa
Spika, mafanikio ya utekelezaji wa bajeti niliyowasilisha
yatategemea ushirikiano wa kila mmoja wetu ili kufikia malengo yanayokusudiwa.
Kama nilivyoeleza hapo awali, bajeti ya mwaka 2016/17 itategemea zaidi mapato
ya ndani katika utekelezaji wake, hivyo kila taasisi ya Serikali inahimizwa
kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kufikia lengo la
mapato linalokusudiwa na hatimaye kutoa huduma bora kwa wananchi wetu. Ninaomba
sote tushirikiane kwa pamoja na kila mmoja awajibike katika nafasi yake ili
tuijenge Tanzania ya viwanda.
104. Mheshimiwa
Spika, kwa kumalizia, niwashukuru kwa dhati wananchi wa
Tanzania, hususan wakulima, wafugaji na wavuvi, wafanyabiashara, watumishi wa
umma na walioko sekta binafsi, na Diaspora ambao wanafanya kazi kwa bidii
kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa. Ninyi ndiyo nguzo/muhimili wa
Taifa linalojitegemea. Serikali inawathamini sana. Ninawashukuru pia vijana,
Taifa la kesho. Wale waliopo shuleni na vyuoni someni kwa bidii mpate maarifa
na ujuzi wa kuijenga nchi yenu. Na wale wengine tumieni nguvu zenu na ubunifu
wenu katika kilimo cha mazao ya thamani kubwa, ufugaji, na huduma ikiwa ni
pamoja na tasnia za ubunifu, muziki, filamu, komedi, mitindo ambako bado kuna
fursa tele za kujipatia kipato halali ili kukidhi mahitaji ya maisha.
105. Mheshimiwa
Spika, mwisho kabisa naomba kuwatambua na kuwashukuru Washirika
wetu wa Maendeleo wanaotarajia kuchangia Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17
kama ifuatavyo: nchi za Canada, Jamhuri ya watu wa China, Denmark, Finland,
Hispania, India, Ireland, Italia, Japani, Korea ya Kusini, Marekani, Norway,
Poland, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, na Uswisi,
pia taasisi mbalimbali za kimataifa ikiwemo Arab Bank for Economic Development
in Africa (BADEA), Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Global Fund,
Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Organisation of the Petroleum Exporting
Countries (OPEC Fund), Saudi Fund, Kuwait Fund, na Umoja wa Ulaya. Aidha,
napenda kutambua uhusiano mzuri tulionao na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)
chini ya Mpango wa Ushauri wa Kisera unaojulikana kama Policy Support
Instrument (PSI). Rai yangu kwa marafiki zetu ni kuwa: Endeleeni kutuunga mkono
hususan katika jitihada zetu za kujenga uchumi wa viwanda kwa kuwavutia
wawekezaji kutoka katika nchi zenu na kututafutia fursa za masoko ya bidhaa
zetu. Mtimize ahadi zenu kwa wakati nasi tunawaahidi kutumia michango yenu kwa
ufanisi na uwazi.
HAPA KAZI TU!
MUNGU IBARIKI TANZANIA!
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269