.

JESHI LA POLISI MKOA WA KASKAZINI PEMBA LAWATOA HOFU WANANCHI

Jun 9, 2016indexNa Masanja Mabula –Pemba

JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba limewatoa hofu wananchi katika Mkoa huo wanaotekeleza ibada ya usiku wakati huu wa mfungo wa mwezi wa Ramadhan kwamba ulinzi umeirishwa .
Kamanda wa Polisi Mkoa huo kamishna msaidizi mwandamizi , Hassan Nassir Ali amesema , tayari kikosi cha usalama barabarani kimeongezwa nguvu kwa kuongezewa watendaji ili waweze kuyafikia maeneo yote.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake ja ameahidi kuimarisha ulinzi wa wananchi pamoja na mali zao kwa kipindi chote cha mfungo wa mwezi wa Ramadhan kwa kuongeza maradufu doria za kawaida .
Aidha ameeleza kuwa ulinzi umeiramishwa zaidi katika maeneo ya miji ya Wete , Konde na Micheweni na kuwatoa hofu wananchi wanaotekeleza ibada ya usiku wakati huu wa mfungo wa mwezi wa Ramadhan .
Pia Kamanda Hassan  Nassir  Ali amezidi kuwahakikishia   wananchi  kuwa jeshi la Polisi litaendelea kutunza siri wanazozitoa na kuwataka kutoa ushirikiano ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa .
“Napenda kuwahakikishia wananchi kuwa jeshi la Polisi litaendelea kutunza siri na taarifa ambazo wanazitoa , hivyo ni vyema kuendelea kutupa taarifa ambazo zitafanikisha kuwadhibiti wanaopanga njama ya kufanya hujuma ”alifahamisha.
Amesema utaratibu huo ulioandaliwa na Jeshi la Polisi umelenga kupunguza matukio ya kihalifu pamoja na yale ya ukiukwaji wa kanuni na sheria za nchi hususani za usalama  barabarani .
Akizungumzia tabia ya baadhi ya askari kuvujisha siri wanazopelekewa na raia wema , amesema kwamba ni vyema wananchi kuwasiliana moja kwa moja na wakuu wa Vituo pamoja na maofisa wengine wa jeshi kuwaripoti askari wanaotoa siri ili wachukuliwe hatua za kisheria .
“Ni vyema wananchi kuwasiliana moja kwa moja na maofisa wa Jeshi la Polisi kuwaripoti Askari ambao wanavujisha siri , kwani wanalipaka matope jeshi na kwamba tutawachukulia hatua za kisheria ”alisisitiza.
Amesema askari hao wanasababisha Jeshi kulaumiwa na wananchi , na kuwafanya wananchi wakose imani na chombo chao cha ulinzi kutokana na askari  wachache wanaokiuka maadili ya kazi zao .

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª