Breaking News

Your Ad Spot

Jun 20, 2016

MKURUGENZI WA MANISPAA YA ILEMELA MKOANI MWANZA AKABIDHI MADAWATI KWA AJILI YA SHULE ZA MSINGI

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, John Wanga, akizungumza wakati wa kukabidhi madawati katika Manispaa hiyo.
…………………………………………………………………………………………………………….
Na BMG
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, imekabidhi madawati 2,600 kwa shule zote 74 za Msingi za umma zilizopo kwenye manispaa hiyo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Dkt.John Pombe Magufuli la kutaka kila wilaya kumaliza tatizo la madawati ifikapo Juni 30 mwaka huu.
Madawati hayo ambayo yametengenezwa kwenye karakana ya shule ya sekondari ya wavulana ya Bwiru, ni sehemu ya mpango wa kutengeneza madawati 9,080 na hivyo kumaliza kabisa tatizo la uhaba wa madawati katika manispaa hiyo.
Akikabidhi madawati hayo hii leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga, amesema madawati hayo yametengenezwa kutokana na fedha zitokanazo na makusanyo ya ndani pamoja na michango ya wadau wengine ambapo katika mgawo wa awali, kata zote 19 za manispaa hiyo zimepewa madawati 139 kila moja.
Wanga amesema kila dawati moja lenye uwezo wa kukaliwa na wanafunzi watatu, limegharimu shilingi 98,000 ambapo manispaa ilinunua vifaa ikiwemo mbao, misumari na vyuma na kulipa gharama za ufundi zinazofikia shilingi 15,000 kwa kila dawati na kwamba madawati mengine yaliyobakia kukidhi mahitaji yanaendelea kutengenezwa kwenye karakana hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Manju Msambya, amepiga marufuku matumizi ya madawati hayo kwenye shughuli nyingine ikiwemo mikutano ya kisiasa huku akiwataka wazazi,walezi na jamii nzima kwa ujumla kutambua umuhimu wa kuchangia juhudi za kuboresha elimu.
Renatus Mulunga ambae ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela amesema halmashauri hiyo inafanya kila jitihada kuhakikisha kwamba inatatua tatizo la upungufu wa madawati kwa shule za msingi katika manispaa hiyo, hatua ambayo itasaidia kuboresha ari ya wanafunzi kujisomea.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages