Licha ya juhudi za upatanishi kwa ajili ya
kutatua mgogoro wa Burundi, serikali ya nchi hiyo imekataa pendekezo la
kufanya mazungumzo na wapinzani wake wa kisiasa.
Katika hali ambayo mazungumzo ya kujaribu kutatua tofauti
zilizopo baina ya serikali na vyama vya upinzani nchini yanatakiwa
kumalizika kufikia mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, serikali ya
Bujumbura imeweka wazi kuwa, kamwe haiwezi kuketi kwenye meza moja ya
mazungumzo na wanaharakati wa kisiasa wanaosababisha mchafuko na hali
ya mivutano nchini humo.
Msemaji wa serikali ya Burundi, Philippe Nzobonariba amesema kuwa, ni
suala lisilowezekana kufanya mazungumzo na wapinzani wenye misimamo
mikali na makundi yenye silaha ili kufikia maelewano ya kitaifa.
Nzobonariba amesisitiza pia kuwa mazungumzo kati ya serikali na
wapinzani yatafanyika kwa kuwashirikisha tu shakhsia wanaounga mkono
mapatano ya kitaifa na mazungumzo ya amani. Baadhi ya vyama vya kisiasa
nchini Burundi kati ya tarehe 21 na tarehe 24 mwezi Mei mwaka huu,
vilishiriki katika mazungumzo shirikishi ya mjini ArushaTanzania hata
hivyo baadhi ya wapinzani walisusia mazungumzo hayo. Mazungumzo ya
amani nchini Burundi chini ya upatanishi wa Rais Yoweri Museven wa
Uganda, yalimalizika mwaka jana bila kufikia natija yoyote. Rais
mstaafu wa Tanzania Benjamin William Mkapa hivi sasa ndiye mpatanishi
katika mazungumzo ya kusaka amani Burundi kati ya serikali na wapinzani.
Mgogoro wa Burundi ulianza tarehe 25 April mwaka jana, wakati Rais
Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo alipotangaza azma yake ya kugombea kiti
cha urais kwa tiketi ya chama tawala katika uchaguzi wa mwezi Julai
mwaka jana. Maandamano ya wananchi, mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli na
kuuawa watu karibu 500 ni mambo ambayo yamejiri huko Burundi katika
kipindi cha mwaka mmoja wa hivi karibuni kufuatia hatua ya rais huyo ya
kurefusha muda wake wa kusalia madarakani. Tarehe tatu ya mwezi huu,
Benjamin Mkapa ambaye alichaguliwa na Jumuiya ya nchi za Afrika
Mashariki EAC kuwa mpatanishi wa mgogoro wa Burundi, alitangaza kuwa
tarehe 15 ya mwezi huu atakutana na muungano mkuu wa vyama vya upinzani
dhidi ya serikali kwa ajili ya mazungumzo. Ahadi ya msuluhishi huyo,
ilienda sambamba na kutolewa na serikali muhula wa kuhitimisha harakati
za upinzani kwa kundi la wapinzani la eneo la Mugamba. Hii ni kusema
kuwa, Rais Pierre Nkurunziza alitoa muhula wa siku 15 kwa waasi wa eneo
hilo kuhakikisha wanaachana na harakati zao za uasi na kurejea mjini
Bujumbura haraka iwezekanavyo. Duru za usalama nchini humo zinazitaja
harakati za kundi hilo jipya kuwa ziilizo na lengo la kupinga hatua ya
kuendelea kusalia madarakani Rais Nkurunziza. Kwa mujibu wa duru hizo za
usalama, wafuasi wa kundi hilo ndio waliohusika na mashambulizi kadhaa
ya hivi karibuni katika viunga vya jiji la Bujumbura. Wakati huohuo
baadhi ya weledi wa mambo wamelihusisha kundi la vijana wa chama tawala
Imbonerakure na mauaji dhidi ya wapinzani ndani ya taifa hilo. Kwa
hakika kuendelea kusalia madarakani Rais Pierre Nkurunziza kumeibua
mgogoro mkubwa nchini Burundi, mgogoro ambao baadhi ya weledi wa mambo
wameutabiri kuwa huenda ukadumu hadi mwaka 2022. Kuendelea kung'ang'ania
madaraka ni jambo ambalo vyama vya upinzani na waungaji mkono wa
demokrasia wameliona kuwa kinyume cha sheria na kwa ajili hiyo wamemtaka
Rais Nkurunziza kuondoka madarakani. Jariobio la mapinduzi ya kijeshi
lililoongozwa na Godefroid Niyombare hapo tarehe 13 mwezi Mei mwaka
jana, linaonekana kuwa lililoutikisa utawala wa Rais Nkurunziza nchini
humo. Pamoja na yote hayo viongozi wa Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Nchi
za Afrika Mashariki walilaani jaribio hilo la mapinduzi na kusisitizia
kuwa, hatua yoyote ya kuingia madarakani inatakiwa kujiri kupitia
makubaliano ya mjini Arusha, kaskazini mwa Tanzania na kwa mujibu wa
katiba ya taifa la Burundi. Kwa mujibu wa weledi wa mambo, serikali ya
Bujumbura bado inaendelea kusisitiza kukataa pendekezo la taasisi hizo
zilizoitaka serikali hiyo kufanya mazungumzo na wapinzani.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269