Ofisa mwandamizi wa jeshi la Marekani
anatazamiwa kupandishwa kizimbani karibuni hivi kwa madai ya kutishia
kushambulia msikiti na kuua waumini wa Kiislamu katika jimbo la Carolina
Kaskazini.
Taarifa ya Polisi ya Kaunti ya Hoke imesema kuwa, Meja Russell
Thomas Langford, kamanda mwandamizi wa jeshi la Marekani anakabiliwa na
mashitaka ya kutishia kufanya mauaji, udini, kutishia umati mkubwa kwa
silaha, kutoa matamshi ya kibaguzi na kuvizia. Habari zinasema kuwa,
Alkhamisi iliyopita Meja Langford alitishia kuwaua kwa bastola na
kuwagonga kwa gari lake, waumini wa Kiislamu waliokuwa wakielekea katika
msikiti wa Al-Madina, katika mji wa Raeford, Kaunti ya Hoke, jimbo la
Carolina Kaskazini, kutekeleza ibada ya Swala nyakati za jioni wakati
huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Imearifiwa kuwa, mbali na kuwatishia
kwa bunduki na kuwatolea maneno makali ya kibaguzi, ofisa huyo
mwandamizi wa jeshi la Marekani alimwaga kwa makusudi na kejeli, nyama
za nguruwe katika lango la kuingia msikiti huo. Ibrahim Hooper, msemaji
wa Baraza la Mahusiano la Waislamu nchini Marekani amekosoa kitendo
hicho na kulitaka jeshi la polisi nchini humo kuwadhaminia usalama
waumini wa Kiislamu wanapotekeleza ibada zao na haswa ibada za usiku
katika mwezi huu wa Ramadhani.
Sanjari na kushika kasi kampeni za uchaguzi wa rais nchini Marekani,
suala la chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu limeongezeka mara
dufu, huku baadhi ya wanasiasa kama vile mgombea wa kiti cha rais wa
chama cha Republican, Donald Trump wakitoa wazi wazi maneno makali ya
kuudhi dhidi ya wafuasi wa dini hiyo tukufu.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269