Maelfu ya
raia wa Uturuki walijitokeza jana (16.07.2016) kumuunga mkono Rais
Recep Tayyip Erdogan baada ya jaribio la mapinduzi ya serikali
lililofanywa na jeshi Ijumaa usiku kutibuka.
Jaribio
hilo la kuipindua serikali ya Uturuki limesababisha vifo vya takriban
watu 265 na maelfu ya wengine kujeruhiwa. Serikali ya Erdogan
inamshutumu hasimu mkuu wa Rais Erdogan, Sheikh Fethullah Gulen, aliye
uhamishoni Marekani kwa kuhusika na njama hiyo ya mapinduzi, madai
ambayo Gulen ameyakanusha vikali na kulaani jaribio hilo la mapinduzi ya
serikali.
Maafisa
nchini Uturuki wamewakamata takriban watu 3,000 wanaoshukiwa kuhusika
katika njama ya kuipindua serikali na kuagiza maelfu ya majaji nchini
humo kukamatwa.
Kiasi ya
majaji na waendesha mashitaka 3,000 wameondolewa kutoka nyadhifa zao na
agizo la kukamatwa kwao limetolewa kwa kudaiwa kushirikiana na Gulen
kutaka kuipindua serikali.
Gulen alaumiwa kwa kuchochea uasi
Erdogan
anamlaumu Gulen kwa kujaribu kuchochea uasi katika jeshi, vyombo vya
habari na idara ya mahakama nchini Uturuki. Uturuki imeitaka Marekani
kumrejesha Gulen nchini humo. Marekani imesema iko tayari kuisadia
Uturuki kubaini ni kina nani walihusika na njama hiyo lakini imeweka
wazi itachukua hatua iwapo kutakuwa na ushahidi Gulen alihusika.
Akizungumza
hapo jana mjini Istanbul, Erdogan amesema waliohusika katika jaribio
hilo lililofeli wataadhibiwa vikali na kuongeza uasi huo wa baadhi ya
wanajeshi ni zawadi kutoka kwa Mungu kwasababu itakuwa ni sababu ya kile
alichokitaja 'kulitakasa jeshi'.
Miongoni
mwa waliokamatwa ni makamanda wakuu wa jeshi akiwemo mkuu wa kikosi cha
jeshi kinacholinda mipaka ya taifa hilo na Syria, Iraq na Iran.
Mamia ya
wanajeshi wanazuiwa mjini Ankara kwa kudaiwa kuhusika katika mapinduzi
hayo, na kusababisha vituo vya polisi kuwa na msongamano mkubwa wa
waliokamatwa.
Erdogan
ameitawala Uturuki, taifa lenye idadi ya watu milioni 80 tangu mwaka
2003. Rais wa Marekani Barack Obama ameeleza kuiunga mkono serikali ya
Uturuki na kuzitaka pande zote nchini humo kuepuka kuliyumbisha taifa
hilo na kuzingatia sheria.
Marekani yahusishwa na mapinduzi
Hata
hivyo waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amemuonya mwenzake
wa Uturuki Mevlut Cavusoglu dhidi ya kuihusisha Marekani na njama hiyo
ya kuipundua serikali na kuongeza madai hayo ni uwongo mtupu na huenda
ikaathiri uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Matukio
hayo ya hivi karibuni yanatarajiwa kuiathiri sekta ya utalii ya Uturuki
ambayo tayari imeathirika kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya
kigaidi nchini humo.
Kufikia
jana mchana, shirika la habari la CNN la Uturuki liliripoti maafisa wa
usalama wamekamilisha operesheni dhidi ya waliopanga mapinduzi.
Katika
nchi jirani ya Ugiriki, maafisa nchini humo waliwakamata watu wanane
waliokuwa katika ndege ya kijeshi ya Uturuki iliyotua katika mji wa
kaskazini mwa nchi hiyo wa Alexandroupolis.
Wakati huo huo, serikali ya Uturuki imetangaza kambi ya jeshi la anga ya Incirlik imefungwa kufuatia jaribio hilo la mapinduzi.
Kambi ya Incirilk yafungwa
Kambi
hiyo inatumika na muungano wa kijeshi unaongozwa na Marekani pamoja na
jeshi la Ujerumani na ni kituo maalumu cha operesheni za kijeshi dhidi
ya kundi la wanamgambo wenye itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu
IS.
Inashukiwa
kuwa kambi hiyo ilitumika na wanajeshi walioshiriki katika jaribio la
kutaka kuipindua serikali ya Uturuki hapo juzi usiku.
Mapema
mwezi huu, wabunge kadhaa wa Ujerumani walizuiwa kuitembelea kambi hiyo,
huku kukiwa na mvutano uliotokana na Ujerumani kuyatambua mauaji
yaliyofanywa na utawala wa Ottoman dhidi ya Waarmenia mwaka 1915 kuwa ni
mauaji ya halaiki.
Huku hayo
yakijiri, Marekani imewaonya raia wake dhidi ya kusafiri kuelekea
Uturuki. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeonya kuwepo ongezeko la
kitisho kutoka kwa makundi ya kigaidi kote Uturuki na kuwaonya raia wake
dhidhi ya kusafiri kuelekea hasa kusini mashariki mwa Uturuki. DW
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269