.

AJABU YA ' SITTA NA MUNGAI; ' MACHIFU' WAWILI WAAGWA NDANI YA JUMA MOJA NA KUPUMZISHWA KWENYE NYUMBA YA MILELE SIKU MOJA

Nov 10, 2016

Ndugu zangu,
Samwel Sitta ( 74) na Joseph Mungai ( 73) ni marafiki wa tangu Tabora Boys. Wawili hawa mama zao wanatoka kwenye koo kubwa za kichifu; Mama wa Samwel Sitta, Zuena Said Fundikira, ni biinti wa Chifu Fundikira ambaye babu yake ni Mtemi Isike Kiyungi.
Mama wa Joseph Mungai anatokana na ukoo wa Malangalila unatokana na Chifu Mkwawa. Hivyo, akina Malangalila na Mwamuyinga ni wajomba zake Joseph Mungai kutoka ukoo wa Kichifu wa Mkwawa.
Hivyo, wawili hawa mbali ya urafiki wao wa tangu shule uliowapelekea hadi kufanya kazi kama Mawaziri kwenye Serikali za Awamu Nne, pia ni watani wa jadi. Ni kwa vile Wahehe chini ya Chifu Mkwawa walipigana na Wanyamwezi chini ya Mtemi Isike .
Katika namna ya kusuluhisha mgogoro, Chifu Isike alimuozesha binti yake kwa Chifu Mkwawa. Kikosi kidogo cha Wakonongo kilitumwa na Isike kumsindikiza binti huyo. Walipoikaribia Iringa, Mkwawa alituma watu wake kwenda kumpokea binti huyo nje kidogo ya Iringa mahali ambapo hadi hii leo panaitwa Ikonongo.
Na Wakonongo wale waliamua kuweka makazi yao hapo. Ni nje kidogo ya Manispaa ya Iringa, na dalili za ujio wa Wakonongo hapo ni uwepo , hadi leo, wa watu wa asili ya Kikonongo na miti mingi ya miembe waliokuja nao Wakonongo kutoka Tabora, enzi hizo.
Ni huzuni kwa vile marafiki hawa wawili hawakuweza kuagana. Na kwa vile, wote wawili marafiki zao wengi ni wa wote wawili, basi, imebidi hata siku za kuwaaga Sitta na Mungai zipishane hata kwa siku moja ili marafiki wapate kuwaaga .
Chifu Mungai ameagwa leo, na mwenzake Chifu Sitta ataagwa kesho. Wote wawili watazikwa katika siku moja ya Jumamosi, mmoja Mufindi na mwingine Urambo.
Pumzikeni Kwa Amani; Chifu Sitta na Chifu Mungai
Maggid Mjengwa.(P.T)

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช