.

KIWANDA CHA SUKARI MAHONDA CHAHITAJI ENEO ZAIDI LA ARDHI KUFANIKISHA UZALISHAJI

Nov 10, 2016


sukar
Na Mwashungi Tahir-Maelezo -Zanzibar
Meneja wa Biashara wa Kiwanda cha sukari Mahonda Bw Pronav Shah amekumbushia ombi lao kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar la kukipatia Kiwanda maeneo zaidi ya ardhi ili kuimarisha uzalishaji wa sukari katika kiwanda hicho.
Amesema kiwanda hulazimika kusitisha uzalishaji wa sukari kutokana na upungufu wa miwa na huku ikwalipa mishahara wafanyakazi bila ya kuzalisha na kukipelekea kiwanda kuingia katika hasara.
Ameeleza hayo Ofisini kwake Mahonda wakati Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi ilipofanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho kuangalia mafanikio na changamoto zinazowakabili .
Bw Pronav Shah ameieleza Kamati hiyo ya Baraza la Wawakilishi kuwa sehemu kubwa ya mashamba ya kiwanda imevamiwa na wananchi wa kawaida kwa shughuli zao ikiwemo ujenzi wa nyumba huku wakijua kuwa ni sehemu ya kiwanda na kupunguza ukubwa wa shamba hilo.
“Sehemu kubwa ya shamba la miwa hivi sasa limevamiwa na watu wa kawaida na inasemekana wanaungwa mkono na baadhi ya viongozi wa shehia,” amelalamika Meneja huyo.
Katika hatua nyengine Meneja huyo wa Biashara ameiomba serikali kuwapatia bima ili inapotokea ajali waweze kufidiwa gharama za ajali hiyo.
Amesema iwapo serikali itawapatia bima itawasaidia hasa kwa vile mara kwa mara mashamba ya miwa hushambuliwa na moto ambao haujulikani chanzo chake licha ya juhudi za uchunguzi zinazofanwa na jeshi la Polisi.
Bw. Pronav Shah ameshauri kuruhusiwa kupanua soko la kuuza sukari katika soko la Tanzania Bara ambalo hivi sasa bei ni tafauti na Zanzibar ama kuuza sukari yao Zanzibar kwa bei ya soko la Tanzania Bara.
Nae mwenyekiti wa Kamati ya Fedha , Biashara na Kilimo Yussuf Hassan ameutaka uongozi wa Kiwanda hicho kuendeleza uzalishaji wa sukari ili kuwasaidia vijana kupata ajira na kufikia lengo la kujitosheleza kwa bidhaa hiyo.
Ameuhakikishia uongozi wa kiwanda hicho kuwa ombi lao la kupata ardhi zaidi kwa ajili ya kuongeza mashamba ya miwa watalifikisha katika ngazi za juu ili liweze kupatiwa ufumbuzi.
Amesema Serikali inafahamu kuwa kufanikiwa kwa Kiwanda cha sukari cha Mahonda itakuwa ni kivutio kwa wawekezaji wengine kuja kuwekeza Zanzibar. (P.T)

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช