Shirika la kutetea haki za binadamu la
Amnesty International limesema wanaharakati wapatao 150 wa vuguvugu
linaloshinikiza kujitenga jimbo la Biafra wameuawa na jeshi la Nigeria
katika kipindi cha mwaka mmoja.
Ripoti ya kurasa 60 ya Amnesty International iliyotolewa leo
Alkhamisi imebainisha kuwa, maafisa usalama nchini Nigeria walitekeleza
ukatili huo kwa lengo la kuzima maandamano ya wanaharakati wa Biafra,
kati ya Agosti mwaka jana 2015 na Agosti mwaka huu.
Makmid Kamara, Mkurugenzi wa shirika hilo nchini Nigeria amesema wana
wasi wasi kuwa yumkini idadi hiyo ikawa juu zaidi akisisitiza kuwa,
vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika vilitimia nguvu
kupita kiasi kuzima maandamano na mikusanyiko ya harakati hiyo.
Wakati huo huo, Sani Usman, msemaji wa jeshi la Nigeria amepuuzilia
mbali ripoti hiyo ya Amnesty International na kuitaja kuwa ya upande
mmoja akisisitiza kuwa, askari watano waliuawa na wanaharakati hao
wakati wa maandamano ya mwezi Mei mwaka huu mbali na kushambuliwa magari
ya jeshi na polisi.
Mwezi Aprili mwaka huu, polisi ya Nigeria ilidai kuwa harakati ya
Biafra imehusika na mauaji ya watu 55, baada ya kugundua kaburi la umati
kusini mashariki mwa nchi, madai ambayo yalikanushwa na harakati hiyo.
Kwa sasa polisi ya Nigeria inamzuilia Nnamdi Kanu, mkuu wa harakati
hiyo inayopigania kujitenga na Nigeria eneo la Biafra la kusini mwa nchi
hiyo pamoja na watuhumiwa wengine wawili wanaokabiliwa na tuhuma za
usaliti na uhaini. Mwaka 1967, Kanu alitangaza uhuru wa jimbo la Biafra
na kusema kuwa eneo hilo sio sehemu ya Nigeria.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269