Wajumbe wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu,
Bunge la Iran, wamelaani hatua ya wajumbe wa Bunge la Marekani kurefusha
kwa muda wa miaka 10 sheria ya kuiwekea Iran vikwazo.
Wabunge wa Iran katika kikao cha wazi cha bunge Jumanne ya leo,
walitoa taarifa kulaani hatua hiyo ya Marekani na kuitaka serikali ya
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kukabiliana na uamuzi huo kwa mujibu wa
sheria iliyopitishwa na Majilisi kuhusu mapatano ya nyuklia yajulikanayo
kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA.
Itakumbukwa kuwa, Julai 14 mwaka jana, Iran na nchi zinazounda kundi
la 5+1 zilifikia mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa
Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Baada ya mapatano hayo Bunge la Iran
lilipitisha sheria maalumu ambayo inaainisha ni hatua gani
zitakazochukuliwa iwapo moja kati ya madola sita makubwa duniani
yatakiuka mapatano hayo.
Katika taarifa yao, wabunge wa Iran wamesisitiza kuhusu kulinda
mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu katika sekta ya nyuklia kwa matumizi
ya amani.
Wakati huo huo, Kamal Dehqani Firuzabadi, Naibu Mkuu wa Tume ya
Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni katika Bunge la Iran ameashiria hatua
ya Marekani kuvunja ahadi zake na kurefushwa zaidi vikwazo dhidi ya
Iran katika Bunge la Marekani, na kusema wabunge watawasilisha muswada
wa dharura kuhusu ni hatua gani zichukuliwe kukabiliana na uvunjaji
ahadi wa Marekani.
Baada ya ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais, Bunge la
Marekani ambalo linadhibitiwa na chama cha Trump cha Republican,
lilirefusha kwa muda wa miaka mingine 10 vikwazo dhidi ya Iran sambamba
na kupitisha sheria nyingine ya kuzuia Iran kuuziwa ndege.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269