Serikali ya Sudan imewakamata viongozi wanne mashuhuri wa upinzani nchini humo akiwemo mwanasiasa mkongwe Sadiq Youssef.
Muungano wa upinzani unaoongozwa na Youssef umesema viongozi
hao wa upinzani wamekamatwa ikiwa ni katika mwendelezo wa vyombo vya
usalama kukandamiza wapinzani na wakosoaji wa serikali ya Rais Omar
al-Bashir.
Mbali na Sadiq Youssef, wanasiasa wengine wa upinzani waliotiwa
mbaroni na vyombo vya usalama ni Mohammed Dia al-Din, msemaji wa chama
cha National Consensus Forces na makada wawili wa chama hicho cha
upinzani, Manzar Abu al-Maali na Tareq Abdul Majid.
Haya yanajiri muda mfupi baada ya mgomo wa nchi nzima wa madaktari
nchini humo kusitishwa kwa muda baada ya vyombo vya dola kuwaachilia
huru madaktari wawili waliokuwa wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kushiriki
katika mgomo wa kuipinga serikali ulioanza tarehe 6 Oktoba mwaka huu.
Mbali na mgomo huo wa madaktari, wananchi wa Sudan wanaendelea na
malalamiko yao dhidi ya kupandishwa gharama za nishati pamoja na hali ya
kisiasa na kijamii nchini mwao.
Migomo na maandamano nchini Sudan yanafuatia machafuko na maandamano
yanayoendelea katika pembe mbalimbali za nchi hiyo kupinga hali mbaya ya
kijamii na kiuchumi na sera za serikali ya Rais Omar al Bashir.
Maandamano hayo yameshika kasi zaidi baada ya serikali ya Khartoum
kufuta ruzuku ya wananchi katika sekta ya nishati, suala ambalo
limesababisha kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu na ughali mkubwa wa
maisha.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269