.

BARAZA LA MAWAZIRI LA ISRAEL LAIDHINISHA MPANGO WA KUPIGA MARUFUKU ADHANA HUKO QUDS

Feb 14, 2017

Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Isarel limepasisha sheria ya kupiga marufuku kusomwa adhana katika misikiti ya Quds tukufu baada ya kuifanyia marekebisho na kisha kuirejesha bungeni.

Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni Novemba 13 mwaka jana lilipasisha sheria ya kibaguzi ya kuzuia adhana katika misikiti ya mji mtukufu wa Baitul Muqaddas; hatua ambayo imekabiliwa na uipinzani kubwa kutoka kwa makundi ya Kipalestina. 

 Baraza la Mawaziri na Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel zilisitisha uchunguzi wa sheria hiyo ya kupiga marufuku kusomwa adhana katika misikiti ya Quds baada ya kuongezeka malalamiko ya wananchi na viongozi wa Palestina. Hata hivyo ikiwa imepita miezi kadhaa tangu kuchukuliwa hatua hiyo inaonekana kuwa, viongozi wa utawala hio haramu kwa mara nyingine tena wanafuatilia utekelezaji wa njama zao za kuwabana zaidi Wapalestina huko Quds na kubadili utambulisho wa Kiislamu wa mji huo kwa kudhani kuwa malalamiko na upinzani wa  wananchi wa Palestina  na fikra za waliowengi vimepungua.

Katika fremu hiyo, Bunge la Israel Jumatano ijayo limepanga kupiga kura ili kuubadilisha mpango huo wa kupiga marufuku kusomwa adhana huko Baitul Muqaddas na kuwa sheria ikiwa ni katika kuendelea sera na hatua za utawala wa Kizayuni za kubanania zaidi uhuru wa kutekeleza ibada wa raia wa Palestina. 

Kwa mujibu wa mpango huo, ni marufuku kutumia spika katika maeneo ya ibada na vilevile kusoma adhana kuanzia saa tano usiku hadi saa moja asubuhi. 

Katika miongo ya hivi karibuni utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya harakati nyingi kwa lengo la kubadili utambulisho wa Kiislamu wa mji wa Quds Tukufu na miongoni mwa harakati hizo tunaweza kuashiria sheria hiyo ya kupiga marufuku kusomwa adhana na vilevile mpango wa kuugawa msikiti wa al Aqswa kwa mujibu wa wakati na eneo.

Msikiti wa al Aqsa, Kibla cha kwanza cha Waislamu mbele ya njama za Wazayuni
Kivyovyote vile ushahidi  unaonyesha kuwa, njama zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Isarel katika maeneo ya Palestina hususan Baitul Muqaddas zimeshadidi zaidi baada ya kuingia madarakani Rais Donald Trump huko Marekani wiki kadhaa zilizopita na kutoa mkono wa baraka kwa Israel wa kuendeleza sera zake za kimabavu na kupenda kujitanua. Vitendo vya utawala huo vinakwenda sambamba na siasa na misimamo ya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Wapalestina na Waislamu na Waislamu kwa ujumla. 
Suala la kufuta utambulisho wa Kiislamu katika maeneo ya Palestina hususan  Baitul Muqaddas siku zote limekuwa katika ajenda kuu ya utawala wa Kizayuni ambao unatumia mbinu na mikakati mbalimbali  kufanikisha malengo yake ya kujitanua katika ardhi ya Palestina. Israel inachukua hatua hizo zote lengo likiwa ni kubomoa Msikiti wa al Aqswa na kupanua ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Nyumba za walowezi wa Kiyahudi zinazojengwa katika ardhi za Wapalestina 
Israel inafuta utambulisho wa Kiislamu na wa Kipalestina katika ardhi za zinazokakaliwa kwa mabavu hususan huko Baitul Muqaddas kwa kuendelea kubomoa makazi ya Wapalestina na vilevile majengo ya Kiislamu na ya kihistoria. Vitendo vyote hivyo vya kibaguzi vinafanywa na Israel katika hali ambayo Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limesisitiza kwamba, hatua za Israel huko  Baitul Muqaddas ni kinyume cha sheria na kwamba, Msikiti wa al Aqswa ni mali ya Kiislamu.  

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช