Breaking News

Your Ad Spot

Mar 1, 2017

MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KUFANYIKA MACHI 8, 2017

Dodoma, Tanzania
Machi 8, 2017, Watanzania wataungana na nchi watanachama wa Umoja wa Mataifa, katika kuadhimiasha Siku ya Wanawake Duniani.

Taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Sihaba Nkinga, imesema wakati akizungumza  na waandishi wa habari katika Ofisi ya Wizara iliyoko Chuo Kikuu cha Dodoma. 

Katibu Mkuu amesema Maadhimisho hayo kwa mwaka huu yatafanyika katika ngazi ya mkoa kufuatia uamuzi wa Serikali wa mwaka 2005 kuwa yatakuwa yanafanyika kitaifa kila baada ya miaka mitano.


"Uamuzi wa kuadhimisha siku hii kitaifa kila baada ya miaka mitano,  ulikusudia kutoa nafasi kwa Serikali yenyewe na wadau wengine kuweza kupima mafanikio ya shughuli za maendeleo ya wanawake, changamoto zilizoko na kuweka mikakati ya utatuzi wa changamoto hizo", alisema. 

Katibu Mkuu amesema, Kaulimbiu ya Siku ya Wanawake Duniani kitaifa kwa mwaka 2017 inasema  ‘Tanzania ya Viwanda; Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko ya Kiuchumi.’ Kaulimbiu hii inasisitiza kuwajengea  wanawake uwezo wa kitaaluma, kibiashara, upatikaji wa mitaji, masoko na mikopo ili waweze kushiriki kwa usawa, na kunufaika na fursa zilizopo badala ya kuwa wasindikizaji tu.
  
Dhamira ya Kaulimbiu ya ‘Tanzania ya Viwanda; Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko ya Kiuchumi’ inalenga kuhamasisha jamii na wadau wote nchini kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake ili kuwawezesha kushiriki na kunufaika na fursa za maendeleo katika kipindi hiki ambapo Tanzania inaelekea katika uchumi wa viwanda.

Kaulimbiu  hii imetoholewa kutokana na Kauli Mbiu ya Umoja wa Mataifa inayosema ‘Women Economic Empowerment in the Changing World of Work’ ambayo kwa tafsiri ya Kiswahili ni ‘Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Katika Dunia ya Mabadiliko ya Kazi.’ 

Kaulimbiu ya Umoja wa Mataifa inalenga kuzihamasisha Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuwawezesha wanawake kiuchumi ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika sekta za umma na binafsi.

Kaulimbiu ya Kitaifa ya Siku ya Wanawake Duniani  ya mwaka huu imeandaliwa kwa kuzingatia Mazingira ya Nchi yetu; vipaumbele vya kimaendeleo na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati.

Aidha, ujumbe wa Kaulimbiu ya mwaka huu imezingatia Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000), na Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu hususan lengo namba 5 kuhusu usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi.

Kupitia Kaulimbiu hii wadau wote katika ngazi zote  wanakumbushwa kuweka mikakati thabiti ya kutatua changamoto zinazokwamisha kufikiwa  kwa usawa wa jinsia na kusababisha wanawake na wasichana kushindwa kutimiza malengo na ndoto zao kimaisha.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages