Breaking News

Your Ad Spot

May 15, 2017

DED MEATU: MBEGU BORA, KILIMO CHA MKATABA MKOMBOZI KWA WAKULIMA WA PAMBA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Fabian Manoza(Mwenye kofia ya njano akitoa maelezo kwa Wakuu wa Mikoa ya Kanda ya Magharibi inayolima pamba ya Simiyu, Shinyanga, Geita, Mwanza, Kagera, Kigoma, Singida na Tabora walipotembelea mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora ya pamba(UKM08) katika kata ya Mwabusalu wilayani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe.Dkt.Rehema Nchimbi (wa pili kushoto) akichangia jambo wakati wa ziara ya wakuu wa mikoa ya Kanda ya Magharibi inayolima pamba  walipotembelea mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora ya pamba(UKM08) katika kata ya Mwabusalu wilayani Meatu.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe.Aggrey Mwanri (wa pili kushoto) akichangia jambo wakati wa ziara ya wakuu wa mikoa ya Kanda ya Magharibi inayolima pamba  walipotembelea mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora ya pamba(UKM08) katika kata ya Mwabusalu wilayani Meatu.

Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba, Marco Mtunga akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali kwa wakuu wa mikoa ya Kanda ya Magharibi inayolima pamba  walipotembelea mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora ya pamba(UKM08) katika kata ya Mwabusalu wilayani Meatu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita,  Meja Jenerali Ezekiel Kyunga akiwasalimia wananchi wa Kata ya Mwabusalu wakati wa ziara ya Wakuu wa Mikoa ya Kanda ya Magharibi inayolima pamba  walipotembelea mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora ya pamba(UKM08) ya katika kata hiyo wilayani Meatu.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Salum Kijuu akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Meatu  wakati wa ziara ya Wakuu wa Mikoa ya Kanda ya Magharibi inayolima pamba  walipotembelea mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora ya pamba(UKM08) ya katika kata ya Mwabusalu  wilayani Meatu.
Bw.Charles Thobias Mkulima kutoka kata ya Mwabusalu ambaye ametumia mbegu bora ya pamba ya (UKM08) akitoa maelezo kwa Wakuu wa Mikoa ya Kanda ya Magharibi inayolima pamba ambayo ni  Simiyu, Shinyanga, Geita, Mwanza, Kagera, Kigoma, Singida na Tabora walipotembelea mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora ya pamba(UKM08) katika kata hiyo wilayani Meatu.

Na Stella Kalinga, Simiyu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Fabian Manoza amesema Matumizi ya Mbegu bora na Kilimo cha Mkataba ni suluhu ya wakulima wa pamba inayoweza kuwasaidia kuongeza uzalishaji.
Manoza ameyasema wakati akitoa taarifa ya Wilaya ya Meatu kuhusu kilimo cha Pamba kwa Wakuu wa Mikoa nane ya Kanda ya Magharibi inayolima pamba waliotembelea eneo hilo kutoka Simiyu, Shinyanga, Geita, Mwanza, Kagera, Kigoma, Singida na Tabora katika ziara yao kuona mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora ya pamba(UKM08) katika kata ya Mwabusalu wilayani Meatu.
Amesema kupitia kilimo cha mkataba wananchi watakuwa na uhakika wa kupata pembejeo bora za kilimo zikiwemo mbegu bora, mbolea na viuadudu kutoka kwa watu au makampuni yatakayoweka mikataba nao.
“Tunatarajia kuongeza uzalishaji ili kupata kata nyingi zaidi, tumewasisitiza wananchi kuwa kilimo hiki cha mbegu bora lazima kiendane na kilimo cha mikataba, wale wanaohitaji kununua pamba lazima waingie mikataba na wakulima ili wapate faida walizokuwa hawazipati; baadhi yao wamekuwa wakihangaika hawana uwezo wa kununua mbegu, viuadudu na kuhudumia mashamba, lakini wakiingia mikataba hao watakaonunua pamba watatoa huduma zote hizo kwa wakulima” alisema.
Ameongeza kuwa pamoja na kilimo cha mkataba na matumizi ya mbegu bora ili kuboresha uzalishaji wa pamba Wataalam wa Kilimo wanapaswa kuwapa wakulima huduma zote muhimu za ugani ili wazingatie taratibu
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Meja Jenerali Ezekiel Kyunga ameitaka Bodi ya Pamba nchini kuboresha utaratibu wa kilimo cha mkataba ili kiweze kuwanufaisha wakulima badala ya kuwakatisha tamaa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe.Aggrey Mwanri amesema ni vema Bodi ya Pamba ikaweka  utaratibu utakaowawezesha wakulima kupata mbolea na zana bora za kilimo kwa mkopo ambao watarejesha baada ya mavuno.
Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba, Marco Mtunga amesema wakulima wa pamba kwa miaka ya nyuma wamekuwa wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo  ukosefu wa mbegu bora na kutopanda kwa kuzingatia mistari, hivyo katika msimu wa mwaka 2017 jumla ya tani 8000 za mbegu bora zitazalishwa kwa ajili ya kusambaza kwa wakulima na jitihada zinaendelea kufanywa kupitia kilimo cha mkataba kuhamasisisha wakulima kulima kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu.
Aidha, Mtunga amesema ili kuongeza uzalishaji wa pamba wakulima wahamasishwe kulima kilimo cha mkataba na ili kilimo cha mkataba kiwe na tija kwao Bodi hiyo inaendelea kutimiza wajibu wake kusimamia masharti yaliyowekwa katika utekelezaji wa mikataba hiyo kati ya wachambuzi  na wakulima wa pamba.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe.Dkt.Rehema Nchimbi amesisitiza kuwepo kwa mikakati ya kilimo cha umwagiliaji katika zao la pamba ikiwepo uchimbaji wa mabwawa makubwa yatakayowasaidia wakulima wakati wote badala ya kutegemea mvua tu.
Naye  Bw.Charles Thobias Mkulima wa kata ya Mwabusalu ambaye ametumia mbegu bora ya pamba ya (UKM08) amesema mbegu hiyo imekuwa mkombozi kwa wakulima kwa kuwa kulingana na mazao yalivyo sasa shambani, mavuno yataongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na msimu uliopita.
Utekelezaji wa Mpango wa uzalishaji wa Mbegu bora katika kata ya Mwabusalu Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu umehusisha jumla ya wakulima 1,709 katika vijiji vinne ambao kwa pamoja wameweza kulima jumla ya ekari 6,506 na unafadhiliwa na Programu ya Kuendeleza Kilimo cha Pamba chini ya usimamizi wa Bodi ya Pamba.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages