.

NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI ZAUNGANISHA NGUVU KUTOKOMEZA UVUVI HARAMU KATIKA ZIWA VICTORIA

Mar 11, 2018

Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Tanzania, Luhaga Mpina mwenye miwani akimkabidhi uenyekiti  wa Baraza  la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi na Utunzaji wa Viumbe Kwenye Maji katika nchi za Afrika Mashariki(FASCoM)  Ssempija Vicente Bamulangaki ambaye ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Uganda hivi karibuni

Na Mwandishi Maalum, Entebbe 
NCHI za Tanzania, Kenya na Uganda zimeridhia kufanya operesheni ya pamoja kupambana na uvuvi haramu katika Ziwa Victoria ili kuokoa samaki aina ya sangara walioko katika hatari kubwa ya kutoweka.

Uamuzi huo umefikiwa na Baraza la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria  ( LVFO) na kuidhinisha Dola 1,800,000 za Marekani, sawa na sh. Bilioni 4.1  za Tanzania kwa ajili ya kufanya operesheni hiyo, hivyo nchi za Kenya, Uganda na Tanzania kila moja itapata Dola 600,000 za Marekani sawa na Sh. Bilioni 1.3 za Tanzania ili kufanikisha operesheni hiyo,

Katika siku za karibuni kumekuwa na malalamiko kuwa operesheni hiyo inafanyika upande mmoja tu wa ziwa hilo kwa Tanzania huku shughuli za uvuvi haramu zikidaiwa kufanyika katika nchi za Kenya na Uganda hivyo uamuzi huo utasaidia kumaliza tatizo hilo lililodumu kwa miaka mingi sasa.

Akizungumza katika kikao kukabidhi madaraka kwa nchi ya Uganda mjini Entebbe juzi, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa Baraza hilo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Tanzania, Luhaga Mpina alisema fedha hizo zitasaidia kuongeza kasi ya kupambana na uvuvi haramu ambapo kwa Tanzania ilishaanza operesheni hiyo mwanzoni mwa mwaka huu na kuleta mafanikio makubwa.

Mpina pia aliwaomba viongozi wa nchi wanachama wanaozunguka Ziwa Victoria kutekeleza kwa vitendo mapendekezo yaliyotolewa na Taasisi za Utafiti za  KMFRI, TAFIRI na NaFIRRI ikiwemo kanuni ya urefu wa samaki aina ya sangara wanaoruhusiwa kuvuliwa (slot size regulations) kati ya sentimita 50 hadi 85, Kanuni hii licha ya kuagizwa na Kikao cha Baraza la Mawaziri 2016  kutumika kwa nchi zote lakini baadhi ya nchi hazijatekeleza sharti hili kikamilifu.

Aidha Waziri Mpina pia  aliwakumbusha viongozi wa nchi zinazotumia Ziwa Victoria kuwaeleza ukweli wananchi wao wanaojishughulisha na biashara ya uvuvi kuhusu Sheria za Uvuvi za nchi zingine ili kujiepusha na adha watakazokumbana nazo pindi nchi husika inapochukua hatua  kwa mujibu wa sheria zake na kwamba  Tanzania itaendelea kuheshimu sheria za nchi nyingine ili kulinda rasimali za ziwa hilo.

“Ni imani yangu kuwa itakuwa hivyo hivyo Kenya na  itakuwa hivyo hivyo Uganda kwani rasilimali hii ni mali yetu sote hivyo tunajukumu kubwa la kuilinda kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho”alisema.

Hivyo Waziri Mpina alisisitiza kuwa biashara ya uvuvi haramu itabaki historia katika nchi za Afrika Mashariki kama viongozi watakuwa na dhamira safi na kujitoa kwa moyo wote kulinda rasilimali hizo na kwamba vita hiyo haiwezi kufanikiwa kama viongozi hawatajitoa mhanga kufanikisha kazi hiyo.

Hata hivyo chini ya uenyekiti wake, Waziri Mpina alijivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana ikiwemo kuanzishwa vya vikosi kazi mtambuka vilivyoweza kongoza mapambano ya uvuvi haramu ikiwemo Inter-Agency Unit ya Kenya, Multi-Agency Task Team(MATT) ya Tanzania na Fisheries Protection Force(FPF) ya Uganda.

Alisema  Tanzania imepata mafanikio makubwa baada ya kuendeshwa kwa operesheni Sangara 2018 ambayo ililenga kupambana na uvuvi haramu kwa kuondoa zana zote haramu ndani ya ziwa, kudhibiti wazalishaji zana haramu pamoja na wachakataji wa samaki wasioruhusiwa.

Aidha Waziri Mpina alimweleza Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Uganda, Ssempijja Vicent Bamulaki kutambua kuwa kupewa fursa ya kuongoza watu ni kupewa  fursa ya kuleta  mageuzi na kwamba uongozi ni vitendo sio nafasi.

Waziri Mpina alieleza kuwa hali ya upatikanaji wa samaki aina ya sangara ni mbaya katika Ziwa Victoria kwani kwa mujibu wa taarifa kutoka Taasisi za Utafiti za Afrika Mashariki zinaonyesha kuwa sangara wenye urefu wa sentimita 50 na kuendelea wamepungua na kubakia asilimia 5 tu, hivyo juhudi za haraka zisipochukuliwa samaki hao watatoweka na shughuli za uvuvi katika ziwa hilo zitakoma .

Aidha, Waziri alisema  katika kipindi cha uongozi wake kumekuwepo na changamoto mbalimbali zikiwemo uvuvi haramu,utoroshaji wa mazao ya uvuvi,usimamizi dhaifu wa sheria, uvunaji holela,nguvu kubwa ya uvuvi,ukwepaji wa mapato ya Serikali, nchi wanachama na nchi za nje kuingia katika mipaka ya nchi nyingine na kufanya biashara ya uvuvi bila vibali wala leseni.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa LVFO anayemaliza muda wake, Godfrey Monor alisema nafasi ya Katibu Mtendaji kwa kipindi hiki ni ya Tanzania na nafasi na Katibu Mtendaji Msaidizi ni ya nchi ya Uganda baada ya Sekretarieti iliyopo kumaliza muda wake Agosti mwaka huu kwa mujibu wa mkataba wa LVFO kifungu cha X hivyo nchi husika zifanye mchakato wa kujaza nafasi hizo kwa muda muafaka.

Monor alisema miongoni mwa maazimio ya kikao hicho ni pamoja na kuundwa kwa chombo kipya kitakachosimamia rasilimali za uvuvi katika nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (East Africa Fisheries Organizatin – EAFO) ili kusimamia shughuli zote za uvuvi katika mito,maziwa na bahari badala ilivyokuwa awali kwa LVFO kusimamia Ziwa Victoria pekee.

Waziri Mpina alisema  miongoni  mwa ajenda za  kikao hicho cha Baraza la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria ( LVFO) ilikuwa ni kujadili utekelezaji wa  maagizo ya  kikao cha awali cha tisa cha Baraza hilo kilichofanyika Nairobi nchini Kenya Januari 29 mwaka 2016. 

Baadhi maagizo yaliyowasilishwa ni pamoja  na kuwasilisha taarifa za tafiti za kisayansi kutoka katika taasisi zenye dhamana ya kufanya tafiti za uvuvi kwenye nchi wanachama ili kusaidia usimamizi wa pamoja wa  Ziwa Victoria ambapo  taasisi hizo kwa upande wa Tanzania ni TAFIRI, Kenya ni KMFRI na  NaFIRRI kwa upande wa Uganda.

Mpina alisema kikao hiki kimekuwa ni kikao cha kwanza baada ya mabadiliko  makubwa yaliyofanywa katika kikao cha tisa cha Baraza la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria  ( LVFO) kilichofanyika Nairobi nchini Kenya Januari 29 mwaka 2016 ambacho kilifanya mabadiliko ambayo yanalifanya baraza hilo kuwa Baraza  la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi na Utunzaji wa Viumbe Kwenye Maji katika nchi za Afrika Mashariki(FASCoM)  badala ya (LVFO)
Baraza  la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi na Utunzaji wa Viumbe Kwenye Maji katika nchi za Afrika Mashariki(FASCoM) linaliwajumuisha  Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi wa Tanzania, Uganda na Kenya, Makatibu Wakuu na Wakurugenzi katika picha ya pamoja  baada ya kikao cha kwanza cha Baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni Entebbe nchini Uganda

Picha ya pamoja ya ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina(mwenye miwani) baada ya kikao cha kwanza cha Baraza  la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi na Utunzaji wa Viumbe Kwenye Maji katika nchi za Afrika Mashariki(FASCoM) kilichofanyika hivi karibuni Entebbe nchini Uganda.Kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Uvuvi, Dkt Yohana Budeba.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª