Breaking News

Your Ad Spot

Sep 1, 2010

MAKALA MAALUM KUHUSU MAADHIMISHO YA MIAKA 46 YA JWTZ

*Zaidi ya Miongo minne limeweza kujimalisha kwa ufanisi
*Limekua msaada mkubwa kwa nchi za Darfur,Lebanon
LEO ni siku muhimu sana kwa wananchi wa Tanzania kwa kuona jeshi letu la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutimiza miaka 46 tokea kuanzishwa kwake mnamo Septemba mosi, 1964, na kuweza kufanya kazi kwa ufanisi na ubora mkubwa kwa Serikali ya awamu zote na kutimiza malengo yake ya kujenga jeshi imara na la kisasa.

Sote tu mashahidi wa Jeshi letu la JWTZ, kwa jinsi linavyotumia Taifa pamoja na mataifa mengine yaliyokumbwa na misukosuko ikiwemo ya hali kimachafuko pamoja na kujitolea kulinda amani katika nchi hizo kwa ustadi mkubwa.

Mpaka sasa ni zaidi ya miongo minne kwa JWTZ, limeweza kushirikiana na Serikali kwa karibu ili kujiimarisha na kujijenga,Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, na Amiri Jeshi Mkuu na Rais Jakaya Kikwete wameonyesha kutilia mkazo uimarishaji wa JWTZ kwa kufikia kiwango cha kimataifa kwa mafunzo na zana za kisasa.

Moja ya mambo hayo ni kwa kuanzisha Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu iliyozinduliwa na Amiri Jeshi Mkuu wa Jakaya Kikwete, hii ni kudhihirisha JWTZ kwa kuzingatia jeshi la nchi kavu likizingatia askari wake wa miguu wanayodhana kubwa ya kupambana na adui ana kwa ana katika uwanja wa vita.

Katika maadhimisho ya leo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) Dk. Hussein Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kilele hicho zitakazofanyika Kigamboni ambako kuna makao makuu ya Kamandi ya Wanamaji.

Sherehe hizo pia zitahudhuriwa na mnadhimu mkuu wa jeshi Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo pamoja na wakuu mbalimbali na wanajeshi.

Historia ya JWTZ
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilianzishwa Septemba 1, 1964 likiwa na lengo la kulinda wananchi, uhuru na mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mafunzo ya awali ya 'kuwanoa" askari wapya yalifanyika chini ya makamanda kutoka Nigeria na kuhitimu rasmi Septemba Mosi 1964 na kula kiapo cha utii na uaminifu mbele ya Amiri Jeshi Mkuu wa kwanza, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Tangu hapo JWTZ likaanza kuandika historia mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo ukombozi wa bara la Afrika, ushindi wa vita ya Kagera, nidhamu na utiifu, uokoaji wakati wa majanga, ulinzi wa amani na hivi karibuni ukombozi wa kisiwa cha Anjouan.

Ukombozi wa Afrika
Baada ya kuhitimu mafunzo hayo, jeshi hilo lilianza kazi ya ulinzi wa nchi lilikiwa pia na jukumu la kusaidia ukombozi Kusini mwa Afrika ikiwemo Msumbiji, Afrika Kusini, Angola, Namibia, Zimbabwe na nchi nyingine kwa kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wapigania uhuru wa nchi hizo.

Tanzania ilianzisha makambi katika sehemu mbalimbali nchini kwa ajili ya kuwafundishia ikiwemo Kongwa Dodoma, Mgagao Kilolo Iringa, Farm 17 Nachingwea, Masonya Tunduru, Shelala Lindi, Kidogozero Pwani, Pongwe Msungura Msata Pwani, Mkuyu Tanga, Matekwe Songea likuyu sekamaganga Namtumbo Ruvuma na nyinginezo

Aidha, Wapiganaji walifunzwa nchini waliongeza vuguvugu la ukombozi katika nchi zao kwa kuanzisha mapigano yaliyozikomboa nchi hizo kutoka katika minyororo ya ukoloni na ubaguzi wa rangi na kufanikisha nchi zote kujikomboa hadi kufikia mwaka 1975.

Kazi nyingine inayolifanya ni kutoa mafunzo ya kivita kwa maafisa na askari ili kumshinda adui, kutoa msaada unaohitajika kwa mamlaka za Serikali katika hali ya hatari na maafa yatokanayo na nguvu za asili kama vile mafuriko, kimbunga na mengineyo ambayo huharibu miundombinu na mali za watu

JWTZ pia imekuwa ikitoa msaada wa kudhibiti ghasia au vurugu ndani ya nchi iwapo majeshi mengine yameshindwa kutuliza hali hiyo, kuendesha na kusimamia mafunzo ya mgambo pamoja na kushiriki katika shughuli za kulinda amani duniani ni miongoni mwa majukumu yanayofanywa na jeshi hilo.

Mpaka sasa baadhi ya wanajeshi wa JWTZ, wapo nchini Sudan katika jimbo la Darfur nchini wakilinda amani chini ya Umoja wa Afrika(AU), na wengine wanafanya kazi hiyo nchini Lebanon.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, akisaidiana na Mnadhimu Mkuu,,Luteni Jenerali Abdulrahman shimbo wamekuwa wakisaidiana na kwa karibu na Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Kikwete ili kuliendeleza kuwa la kisasa na kutimiza malengo.

Nchi yetu kama zilivyo baadhi ya nchi za Ki-Afrika kabla ya mwaka 1884 ilikuwa haina jina kamili ambalo lilijulikana, mpaka mipaka halisi ilipowekwa ya kugawa nchi za bara la Afrika na nchi yetu kuitwa Tanganyika iliyo jumuisha Rwanda na Burundi chini ya Utawala wa Kijerumani.

Wajerumani
Wajerumani waliitawala Tanganyika kuanzia mwaka 1884 – 1918. Walianzisha jeshi lao lililojulikana kama SCHUTZTRUPPE ambalo lilikuwa na askari wapatao 3000, wengi wao walikuwa Wanubi kutoka Sudani.

Jeshi liliongozwa na Maafisa na askari wa Kijerumani wapatao 80, Vita kuu ya kwanza ya dunia ilipoanza 1914 – 1918, Jeshi hilo lilipanuka na kuongeza askari idadi yao ilifikia 12,000.

Waingereza
Baraza la udhamini la Umoja wa Mataifa liliiweka Tanganyika chini ya udhamini wa Waingereza baada ya Ujerumani kushindwa vita Kuu ya Pili. Waingereza waliunda Jeshi lao lililoitwa Kings African Rifles.

Kings African Rifles iliundwa na vikosi vya askari wa miguu, wahandisi wa medani, mawasiliano, mizinga na vikosi vya huduma. Vikosi vya Kings African Rifles vilikuwa Kenya 3rd & 5th Bn Tanganyika 1st 2nd &6th na Uganda 4th Bn.

Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar
Tanganyika ilipata Uhuru Desemba 9, 1961 na siku hiyo Kings African Rifles (KAR) ilibadilishwa na kuwa Tangayika Rifles (TR). Pamoja na kubadilika jina Tanganyika Rifles ilikuwa na muundo sawa na Kings African Rifles (KAR).

Mapinduzi ya Zanzibar yalifanyika Januari 12, 1964 kupinga utawala wa Kisultani.
Jeshi la Ukombozi wa Zanzibar Peoples Liberation Army (PLA) liliundwa baada ya Mapinduzi.

Maasi ya Tanganyika Rifles
Jeshi la Tanganyika Rifles liliasi Januari 20, 1964 na maasi hayo kuzimwa Januari 25, 1964. Maasi yalihusisha vikosi vya Dar es Salaam (DSM) na Tabora.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964 na vijana waliobaki baada ya uasi kutoka Tanganyika Rifles waliungana na vijana jeshi la Ukombozi wa Wananchi wa Zanzibar (PLA).

Mafanikio ya JWTZ
Lilishiriki kikamilifu katika kusaidia nchi za kiafrika ambazo zilikuwa bado hazijapata Uhuru kuanzia 1963 – 1994, linaendelea kushiriki katika utoaji huduma wakati wa maafa ya kitaifa, kushirikishwa katika ujenzi wa Taifa na hapa hutumika zaidi Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Kujenga uchumi-JKU (Zanzibar) na Ulinzi wa amani.

Mafanikio meingine ni ushindi wa Vita vya Kagera (Operation Chakaza) iliyoanza Oktoba 25,1978 na kumalizika Julai 25,1979 dhidi ya majeshi yaliyokuwa chini ya Idd Amin wa Uganda

Kulinda Uhuru na heshima ya nchi yetu baada ya kumfukuza Mvamizi. Makamanda na Wapiganaji kuelewa wajibu wao kwa Taifa. Mshikamano kitaifa kuanzia ngazi zote.

Vita kuu ya kwanza ya Dunia ilipiganwa kuanzia mwaka 1914-18. Sehemu kubwa ya mapigano ilikuwa Afrika hasa Afrika ya Mashariki ambako Tanganyika ilikuwa koloni la Wajerumani waliokuwa wakipigana na Waingereza waliokuwa na Makoloni ya Kenya na Uganda wakisaidiwa na Wabeligiji kutoka Congo (DRC).

Viongozi wa Majeshi ya Wajerumani na Waingereza walikuwa ni Gen Paul-Emil Von Lettow Vorbeck aliyezaliwa mwaka 1874 (Mjerumani) na Gen Jan Christan Sumut ambaye alizaliwa mwaka 1870.

Historia ya Viongozi
Hayati Julius Kambarage Nyerere ndiye alikuwa Amir Jeshi Mkuu wa kwanza kuanzia 1964 hadi Novemba 23,1985, akafuatia na Ali Hassan Mwinyi Novemba 24 1985- Novemba 1995, Benjamin William Mkapa yeye alishika wadhifa huo Novemba 24, 1995 - Desemba 2005. Kwa sasa wadhifa huo unashikiliwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania
Gen MSH Sarakikya (mstaafu) Januari 8,1964 hadi Februari 12,1977,Hayati Gen A Twalipo (mstaafu) Novemba 13,1974 hadi Novemba 8 1980.

Gen DB Musuguri (mstaafu) Novemba 9, 1980 hadi Septemba1,1988, Gen EM Kiaro (mstaafu) Septemba 1,1988 hadi Januari 27,1994,Gen RP Mboma (mstaafu) Januari 28,1994 hadi Juni 30,2001, Gen GM Waitara (mstaafu) Julai Mosi hadi Septemba 13,2007 na Gen DA Mwamunyange Septemba 13,2007 - Hadi sasa

Vituo vya Tiba JWTZ
Jeshi hili pia limekuwa na vituo vya tiba jeshini viimegawanyika katika mafungu matatu vikiwemo vya tiba kwenye vikosi (Unit Aid Station),Hospitali za Kanda na Hospitali Kuu ya Jeshi ambazo hutoa matibabu kwa wanajeshi na raia

Swala la Ndoa JWTZ
Suala la ndoa jeshini huzingatiwa ili kuboresha maisha ya jamii ndani ya jeshi ambapo kitengo cha ustawi wa jamii ndani ya jeshi hilo ndicho huifanya kazi hiyo ambapo askari haruhusiwi kuoa/kuolewa mpaka alitumikie kwa muda wa miaka sita tangu anapomaliza mafunzo ya awali.

Maombi ya kuoa/kuolewa hupelekwa kwa mkuu wa Kikosi cha mwanajeshi na mhusika kupata kibali na taarifa ya ndoa, na cheti cha ndoa kitatumwa Makao Makuu ya Jeshi . Mwanajeshi akiachana na mke/mume taarifa zake zinatakiwa zitumwe makao makuu ya jeshi.

Uandikishwaji wa askari wapya
Mtu yeyote ataandikishwa kujiunga na JWTZ kama ana ifa zifuatazo: - Awe raia wa Tanzania, aliyetimiza miaka 18 na kuendelea, elimu ya kidato cha nne na kuendelea, awe hajaoa/hajaolewa, tabia na mwenendo mzuri ,awe na akili timamu na afya nzuri

Masharti ya Utumishi
Askari atapewa nambari ya utumishi baada ya kufaulu mafunzo ya awali na atalitumikia Jeshi kwa kipindi cha mwanzo cha miaka sita, baada ya hapo atafanya kazi kwa mkataba wa miaka miwili miwili kwa kibali cha Mkuu wa Majeshi.

Maafisa ,Bodi ya Uteuzi wa Maafisa
Huwafanyia usaili askari wenye elimu ya kidato cha sita na kuendelea kutoka Vikosini na Shule za askari wapya, watakaofaulu usahili huo hupewa hadhi ya Afisa mwanafunzi, na hupelekwa Chuoni kwa mafunzo ya uafisa kwa muda wa mwaka mmoja.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
Mapema mwaka 1963 lilianzishwa Jeshi la Kujenga Taifa hapa nchini kwa lengo la kuwalea vijana kwa kuwafundisha umoja na uzalendo, kuwafundisha mbinu za uzalishaji mali na mafunzo ya ulinzi.

Kuanzia mwaka 1964 JWT ilisaidia pia kutoa mafunzo ya kijeshi kwa vijana wa JKT kazi ambayo inaendelea hadi sasa.

Mgambo
Jukumu jingine la JWTZ ilikuwa ni kuwashirikisha wananchi katika ulinzi wa taifa kwa kufundisha jeshi la mgambo. Jukumu hilo ambalo lilipata muitikio mkubwa lilifanyika katika mikoa yote na watu kwa maelfu walipata mafunzo hayo.

Matunda ya kazi hiyo yalionekana mwaka 1978 pale majeshi ya Iddi Amini wa Uganda yalipovamia na kuchukua eneo la Kaskazini la mto Kagera mwaka 1978 na jeshi la Mgambo kushirikiana na JWTZ katika kutoa "Dozi" kwa majeshi ya adui.

Kwa kuwashirikisha Mgambo, Tanzania ilionesha kwa vitendo kuwa kweli jukumu la ulinzi ni wa nchi ni la wananchi wote.

Vita vya Kagera
Kama ilivyoelezwa awali, mtihani wa kwanza wa JWTZ ulikuwa mwaka 1978 pale vikosi vya Dikteta Idd Amini vilipovamia na kuteka Kaskazini ya mto Kagera na kutangaza kuwa eneo hilo ni lao.

Kutokana na uchokozi huo, Amiri jeshi Mkuu wa kwanza Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitangaza vita dhidi ya jeshi la uvamizi na kuwahakikishia wananchi kuwa, "Tanzania kupitia JWTZ ilikuwa na nia ya kumpiga, sababu ya kumpiga na uwezo wa kumpiga Iddi Amini na vikosi vyake.

Baada ya hapo Tanzania iliingia vitani Novemba mwaka 1978 na kwa kipindi kifupi majeshi ya Amini kwanza yalitolewa katika eneo la Kagera baada ya kipigo na hatimaye kazi ya kumuondoa Amini ilifanyika ndani ya nchi yake.

Mashujaa wa vita hivyo walirejea nchini na kupokelewa rasmi na amiri Jeshi Mkuu wa kwanza Hayati Julius nyerere katika eneo la Bunazi julai 25, 1979 siku ambayo sasa ni sikukuu ya mashujaa.

Kwa kuyashinda majeshi ya Nduli Amini JWTZ iliandika historia nyingine ya kuwa makini katika ulinzi wa nchi kwa kutekeleza jukumu lake la msingi la kulinda nchi, mipaka yake, watu na mali zao.

Kusaidia Msumbiji
Pamoja na majukumu yake ya msingi ya kulinda nchi JWTZ pia ilishiriki katika kusaidia ulinzi wa nchi nyingine za Kiafrika kwa mfano kuanzia mwaka 1976 nchi ya Msumbiji ilipambana na waasi wa Renamo ambao walitishia uhuru wa taifa hilo.

Katika harakati hiyo, wanajeshi wa Tanzania zaidi ya 101 walipoteza maisha yao na kuzikwa katika majimbo mbalimbali ya Tete, Manica, Qulimani. Mabaki ya miili ya wahanga hao zilizikwa upya katika eneo la Naliendele Mtwara Septemba Mosi, 2004.

Ulinzi wa amani
Jeshi la Ulinzi laWananchi wa Tanzania (JWTZ) pia limeshiriki katika ulinzi wa amani duniani mara ya kwanza mwaka 1993-95 nchini Liberia na hatimaye nchi hiyo kufanya uchaguzi wa kidemokrasia.

Aidha kuanzia mwaka 2007 wanajeshi wa JWTZ wameshiriki kama sehemu ya majeshi ya kulinda amani nchini Lebanon. Kazi ambayo inafanyika kwa kwa ufanisi mkubwa.

Ukombozi wa Anjouan Comoro
Vilevile Tanzania iliweka historia ya pekee Machi 25, 2008 pake vikosi vya Tanzania vilipoongoza majeshi ya Afrika katika kukikomboa kisiwa cha anjouan. Katika vita hivyo vya kisayansi, majeshi ya AU yalipenya hadi ndani nya kisiwa na kuzingira maeneo yote mhimu.

Tendo hilo la kijasiri liliyaacha mataifa mengine yakiwa midomo wazi kwa mshangao kwani kwa kawaida silaha kubwa ikiwemo mizinga, ndege na hupiga kwanza kabla ya vikosi vya miguu kukamata eneo husika. Hiyo iliwezekana kwa Tanzania kutumia Makomando wake kuzingira eneo bila kutumia silaha kubwa.

Kutokana na ujasiri huo, JWTZ iliandika historia ya kupata ushindi bila kuua wala kuharibu mali za wananchi jambo ambalo ni nadra sana kutokea katika vita.

Tunapoadhimisha siku hii tutambue, kuthamini na kuenzi mchango unaotolewa na JWTZ na kuwapa moyo maafisa na wapiganaji kuendelea kulinda mafanikio yetu ambayo yanaifanya Tanzania kuwa nchi ya kujivunia kwa kuwa na amani na utulivu ukilinganisha na nchi nyingi barani Afrika na sehemu nyingine duniani.

Sikukuu ya kuanzishwa kwa JWTZ inatoa funzo kuwa amani, usalama na utulivu uliopo unapaswa kulindwa na kudumishwa kwa faida ya vizazi vijavyo ili nao waje washerehekee kama tufanyavyo sisi.

MAGWARIDE
Sherehe za kitaifa na nyingine za kijeshi huadhimishwa kwa magwaride rasmi. Magwaride hutofautiana kutokana na lengo au nia iliyokusudiwa.
Sherehe za Kitaifa ni pamoja na kuapishwa Rais wa Jamhuri na Amiri Jeshi Mkuu ambapo Gwaride hufanyika kwa kuhusisha;Jeshi la Ardhini,Jeshi la Ulinzi wa Anga,Jeshi la Majini,Bendi ya Jeshi na Kikundi cha Mizinga.

Orodha ya Vyuo vya Kijeshi
Mpaka sasa JWTZ ina vyuo; vya High Commanders Training Wing ,Command and Staff Colleage,Tanzania Military Academy, Shule ya Usalama na Utambuzi,Shule ya Mafunzo ya Infantria,Shule ya Mafunzo ya mzinga.
Shule ya Mafunzo ya Awali,Shule ya mafunzo ya Huduma,Shule ya Kijeshi ya Ulinzi wa Anga,Shule ya Kijeshi ya mawasilano, Shule ya Mafunzo ya Vifaru, Shule ya Uhandishi wa Medani, Shule, kijeshi ya Tiba, Shule ya Ufundi wa Umeme na Kituo cha Technolojia ya Habari, nyingine ni pamoja na Shule ya Anga ya kijeshi ,Shule ya kijeshi ya Ubaharia na School of Artillery.

Makaya hii imeandaliwa na Andrew Chale, kutoka vyanzo vya mtandao wa jeshi la wananchi wa Tanzania (http://www.tpdf.go.tz/)



maoni simu 0719076376

1 comment:

  1. clinical pharmacy program http://sundrugstore.net/products/proscar.htm link online pharmacy

    ReplyDelete

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages