Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ombeni Sefue akizungumza katika mkutano huo. |
Na Mwandishi Maalum
New York
Wakati utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya kufadhili maendeleo kwa nchi maskini yakiwa yamekwama, huku washirika wa maendeleo wakijipanga kupunguza misaada yao kwa nchi zinazoendelea. Afrika kwa Upande wake imewataka washirika hao kutimizia ahadi zao za huko nyuma na kuacha kusingizia mdodoro wa uchumi.
Akizungumza kwa niaba ya nchi za Afrika ,Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue amesema, nchi zilizoendelea zinawajibu wa kutimiza ahadi zao kwa mujibu wa makubaliano ya Monterrey na Azimio la Doha. Na hasa ikitiliwa maanani kwamba nchi zinazoendelea na hususani za Afrika zimejitahidi kutimiza ahadi zake.
Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, walikutana katika mkutano wa Tano wa Kilele ambapo kwa siku mbili, walijadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu suala zima la ufadhili wa maendeleo, utekelezaji wake na mwelekeo wa baadaye. Majadiliano yaliyojikita katika taarifa za makubaliano ya mikutano ya kimataifa Monterrey na Azimio la Doha.
“ Afrika kwa upande wake imejitahidi sana kutimiza karibu mambo yote iliyoahidi katika mikutano hiyo miwili. Mambo hayo tuliyoahidi na ambayo ninapenda kuyarudia tena leo hii, ni pamoja na kumiliki ajenda zetu za maendeleo, ukusanyaji wa mapato yetu ya ndani, sera na mipango mizuri ya kukuza uchumi, utawala bora , utawala wa sheria, amani na utulivu” akasema Balozi Sefue.
Akasema matokeo ya utekelezaji wa ahadi hizo ni ya kutia moyo sana. “ tunaamani tungeweza kufanya vizuri zaidi kama tungepata misaada zaidi tuliyoahidiwa kutoka kwa washirika wetu” akasisitiza Balozi Ombeni Sefue.
Katika hotuba yake hiyo ambayo ilipokelewa vizuri na kupongezwa na baadhi wa wajumbe wa mkutano huo, akiwamo mwakilishi kutoka Ubalozi wa Marekani katika Umoja wa mataifa. Balozi aliongeza pia kwamba hata kwa upande wa ukuaji wa uchumi, Afrika imekuwa ikifanya vizuri licha ya vikwazo mbalimbali vikiwamo vya mifumo pendelevu na baguzi ya uchumi wa soko na biashara.
“Afrika tumejitahidi sana, licha ya kwamba hivi sasa dunia inakabiriwa na mdororo wa uchumi, uchumi wetu kwa baadhi ya nchi unakuwa kwa kiwango kinachoridhisha. Na ukuaji huu ingawa si mkubwa sana unatokana na mahitaji makubwa ya bidhaa kutoka nchi za afrika kwenda katika nchi zinazoinukia kiuchumi” akabainisha mwakilishi huyo wa Tanzania.
Akizungumza utekelezaji wa ahadi ambazo zimetolewa na nchi wa hisani kabla hata ya mdororo wa uchumi na ambazo hadi sasa bado hazijatekelezwa.
Balozi Sefue anasema “ wakati kiwango cha misaada kwenda Afrika kiliongezeka kwa asilimia 4 mwaka 2010, bado kuna changamoto ya kufikia utekelezaji kamili wa ahadi za maendeleo zilizotolewa katika mikutano ya kimataifa ukiwamo ule wa G8. Tunahitaji kuimarisha ubora wa kiwango wa misaada hiyo na uhakika wa upatikanaji wake” anasititiza na kuongeza
“ Mdororo wa uchumi na matatizo ya kifedha yanayozikabilia nchini zilizoendelea kisiwe kisingizio kwenu ( nchi zilizoendelea) cha kuto timiza ahadi zenu mlizoahidi kuzisaidia nchi zinazoendelea, tumetimiza ya kwetu na nyie timizeni yenu. Tunawashukuru wale wote waliotangaza nia zao za kutekeleza ahadi zao na tunawahimiza wengine kufanya hivyo”.
Aidha Balozi Sefue amewaeleza wajumbe wa mkutano huo ambao pia uliwashirikisha baadhi ya mawaziri kutoka nchi kadhaa na ulifunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro.
Anasema nchi nyingi za Afrika zinafanya jitihada kubwa ya kuimarisha uzalishaji na kuhimili ushindaji katika uuzaji wa bidhaa zake .
“ Nchi za afrika zinataka kufanya biashara miongoni mwao ili kujikomboa na umaskini. Lakini wakati misaada ikiongezeka kwa upande wa biashara katika miaka michache ilioyopita, mfumo mzima wa biashara ya kimataifa bado si mzuri. Afrika inaendelea kuumia kiuchumi kutokana na mifumo mibaya na isiyo sawa ya sheria za biashara” akabainisha.
Akasisitiza kwa kusema, kutokana na ubaguzi katika mfumo zima wa biashara ya kimataifa,mchango wa bara la Afrika katika biashara ya kimataifa kwa mwaka 2009 ulikuwa ni asilimia 3.1.
“ Tulitegema mazungumzo ya Doha, yaliyotarajiwa kukamilisha mwezi disemba mwaka 2005 na ambayo yamekwama tangu mwaka 2008 yangeweza kutoa mwelekeo na matokeo mazuri lakini imekuwa kinyume chake.
Katika hatua nyingine, Balozi Ombeni Sefue, amesema Afrika inahitaji kusaidiwa katika kuweka mikakati na mipango bora ya kuimarisha vyanzo vyake vya mapato ili kufidia kile kinachopunguzwa na wahisani.
“Mdororo wa uchumi umeiadhiri Afrika vibaya sana , na hasa katika uwezo wake wa kukusanya mapato yake ya ndani. Na kwa sababu hiyo tunaomba kusaidiwa katika kuimarisha uwezo watu wa kitaifa katika kukusanya mapato ya ndani” akasihi Balozi Sefue kwa niaba ya Afrika.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269