Na Mwandishi Maalum, New York
Katika hali ambayo haikutarajiwa , hasa pale linapokuja suala la kumchagua Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ( GA), mwishoni mwa wiki - ijumaa, wajumbe wa Baraza hilo ambalo ni nchi 193 walilazimika kupiga kura ya siri ili kumpata Rais wa Baraza la 67.
Hatua ya kupiga kura hiyo ya siri ilisababishwa na kushindwa kukubaliana kwa nchi mbili ambazo zote zilikuwa zikiwania kiti hicho. Nchi hizo ambazo zinatoka Ulaya ya Mashariki ni Serbia na Lithuania. Kanda ya Ulaya ya Mshariki ndiyo ilikuwa na Zamu ya kutoa Rais ajaye wa Baraza la 67.
Kwa kawaida na kwa utaratibu wa Baraza Kuu, rais hupatikana kwa utaratibu wa mzunguko miongoni mwa mabara. Na mara kwa mara pale inapotokea kwamba bara husika kutoa wagombea wawili, basi hutakiwa kuyamaliza wenyewe ndani ya kundi lao na hivyo kupitisha mgombea mmoja ambaye baadaye kupitishwa kwa kauli moja ndani ya baraza hilo.
Hata hivyo hali ilikuwa tofauti kwa nchi hizo mbili, ambazo licha ya kushauriwa wayamalize ndani ya kundi lao, hakuna kati yao aliyekubali kumwachia mwenzie kijiti.
Wagombea wote wawili, walifanya kampeni za hali ya juu wakipitia kwa nchi wanachama kumwaga será zao na kuomba afiriwe kuchaguliwa.
Serbia ilimsimamisha waziri wake wa Mambo ya Nje, Bw. Vuk Jeremic huku Lithuania ikimsimamisha Balozi wake katika Umoja wa Mataifa, Bw. Dalius Cekuolis.
Baada ya wajumbe kupiga kura ya siri, mgombea wa Serbia aliibuka kidedea kwa kupata kura 93 dhidi ya 85 za Lithuania. Na hivyo kuifanya Serbia kuwa Rais wa Baraza Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa na atakalia kiti hicho kwa mwaka mmoja kuanzia mwezi septemba mwaka huu.
Inaelezwa kwamba hii ilikuwa ni mara ya kwanza Baraza kuu kupiga kura ya siri kumpata rais wake,tangu kumalizika wa vita baridi.
Wakati wote wa mchakato wa kupatika kwa rais wa 67 wa Baraza kuu, duru za kidiplomasia zilikuwa zikiashiria kwamba Serbia alikuwa na nafasi ndogo kushinda kiti hicho. Huku ikitabiriwa kwamba Nchi zisizofungamana na upande wowote ( NAM) zingekuwa mstari wa mbele kuingua mkono Serbia, wakati Lithuania ambayo ilikuwa ikitabiriwa ushindi kwamba ingeungwa mkono na Jumuia ya Ulaya na baadhi ya nchi za Ulaya Magharibi.
Hata hivyo mvutano kati ya nchi hizo mbili unaelezwa kwamba unatokana na tofauti za kisiasa na kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili, na kubwa zaidi likiwa ni suala Kosovo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269