Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Goodluck Ole Medeye ( Mb) akizungumza wakati wa maadhimisho ya Miaka 30 ya Mkataba wa Sheria ya Bahari, pamoja na mambo mengine, Naibu Waziri alizungumzia mchango wa Tanzania katika mchakato wote uliopelekea kuazishwa na hatimaye kuridhiwa kwa Mkataba huo., Ujumbe wa Tanzania katika mchakato wa maadalizi ya Mkataba huo, mchakato uliochukua takribani miaka 14 uliongozwa na si Mwingine, bali Mhe. Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba aliyeongoza wa watu watatu wakiwamo, Balozi Mstaafu Aterius Hyera na Jaji James Kateka, ingawa ulikuwa ni ujumbe mdogo lakini ulikuwa na nguvu na ushawishi kubwa wakati wa majadiliano ya mkutano wa Tatu wa Mkataba wa Sheri ya Habari ya Umoja wa Mataifa. Mchango wao bado unaendelewa kutambuliwa na kuthaminiwa sana ndani ya Umoja wa Mataifa.
HABARI KAMILI
Na Mwandishi Maalum, New York
Umoja wa Mataifa, mwishoni mwa wiki umeadhimisha miaka 30 ya kutiwa saini Mkataba wa Sheria ya Bahari ya Umoja wa Mataifa ( UNCLOS). Makataba ambaoTanzania ni kati ya nchi zilizotoa mchango mkubwa katika kipindi chote cha majadiliano yaliyodumu kwa takribani miaka 14.
Maadhimisho ya Mkataba huo yamefanyika sambamba na mkutano wa 22 wa Nchi Wanachama ambazo zimetia Aaini Mkataba huo. Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu unaongozwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Goodluck Ole Medeye ( Mb).
Mkataba wa Sheria ya Bahari ya Umoja wa Mataifa, uliasisiwa mwaka 1982 huko Montego Bay, nchini Jamaika ambapo nchi 119 ikiwamo Tanzania zilitia saini mkataba huo. Hadi mwaka huu nchi 162 zimekwisha uridhia mkataba huo.
Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba, ndiye aliyekuwa kiongozi na kinara wa ujumbe wa watu watatu kutoka Tanzania katika Mkutano wa Tatu wa Mkataba wa Sheria ya Bahari ( UNCLOSIII)
Ujumbe huo ingawa uliokuwa mdogo lakini ulikuwa na watu makini sana, waliokuwa chachu ya hali ya juu na ulifanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba mkutano huo ambao ulikuwa na majadiliano makali hatimaye uliibuka na Mkataba.
Wajumbe wengine wawili walioshiriki majadiliano hayo wakiongozwa na Mhe. Warioba ni Mhe.Balozi Mstaafu Asterius Hyera na Mhe. Jaji James Kateka ambaye wakati huo alikuwa Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje.
Baadaya Mhe, Jaji Joseph Sinde Warioba aliwahi kuwa Jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Sheria ya Bahari. Na Mhe. Jaji James Kateka anahudumu katika Mahakama hiyo.
Akizungumza wakati wa maadhamisho hayo, Naibu Waziri Goodluck Medeye amesema . “ miaka 30 iliyopita tarehe 10 Desemba , 1982 huko Montego bay, Jamaika, nchi 119 zilitia saini mkataba wa Sheria ya Baharí ya UM. Na Tanzania haikuishia hapo, tarehe 30 septemba 1985 kwa mara nyingine Tanzania ilitoa mchango mkubwa katika kuendesha mchakato wamajadiliano yaliandika na kupitia kifungu kwa kifungu cha mkataba huo hadi hatua ya kuridhiwa kwake na Tanzania tukawa nchi ya 24 kuuridhia mkataba huo”.
Na kwa sababu hiyo, Naibu Waziri anasema Tanzania inajivunia sana na kufurahi kwamba licha ya kwamba majadiliano ya kuanzishwa kwa mkataba huo yalikuwa makali na yenye kukatisha tamaa, lakini hatimaye leo Umoja wa Mataifa unaadhimisha miaka 30 ya chombo hicho.
Akaongeza kwa kusema. “ leo hii tunapoadhimisha mafanikio haya, ni vema pia kutambua dhamana kubwa ambayo wananchi wametukabidhi, dhamana ambayo pia inatupasa kutambua ndoto ya waliotutangulia kama ilivyoainishwa katika mkutaba huu, ambayo ni kuendeleza moyo wa maelewano na ushirikiano katika masuala yote yanayohusu sheria ya baharí”.
Na kusisitiza kwamba nchi wanachama zinatakiwa kwenda mbali zaidi ili kuhakikisha kwamba malengo yote ambayo yameainishwa katika mkataba huo yanatekelezwa ili kuchangia ujenzi wa amani na usalama wa jumuia ya kimataifa na matumizi bora ya baharí.
Naibu Waziri akabinisha pia kwamba, Tanzania inaridhishwa na kile ambacho mkataba huo umeweza kufanikisha hadi sasa . Lakini pia Tanzania inatambua kwamba bado zipo changamoto nyingi ambazo bila shaka kwa umoja wao zitaweza kupatiwa ufumbuzi.
Aidha Tanzania pia imesisitiza haja na umuhimu wa nchi wanachama zilizotia saini mkataba huo, kutambua , kuheshimu na kulinda maslahi ya nchi ambazo hazina baharí, zile ambazo haziko katika mazingira mazuri kijiografia na nchi za visiwa vidogo
Halikadhalika, Tanzania imeshauri kwamba mkazo pia uelekezwe katika kuhakisha kwamba kuna kuwa na matumizi bora na sahihi ya raslimali za baharini, kuzuia uchafuzi wa baharí, na kupambana na vitendo vya uharamia wa baharini, vitendo ambavyo havijaainishwa ndani ya Mkataba huo.
Akaongeza kwamba yalikuwa ni matumaini yake kwamba wadau wote tukiwamo sisi nchi wanachama wa mkataba huu tutaendelea kutimiza kikamilifu wajibu wetu katika utekelezaji wa mkataba huo ikiwa ni pamoja na uchangiaji wa raslimali pale inapobidi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269