Chama cha Wananchi (CUF) kimetangaza Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, kuwa ni mmoja kati ya wanachama wa chama hicho, atakayewania nafasi ya Urais.
Pia
chama hicho, kimetoa rasmi ratiba ya uchukuaji fomu na utaratibu wa
kura ya maoni kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uwakilishi katika
uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu wa udiwani, ubunge,
uwakilishi na urais, na hadi ifikapo Aprili 25, chama hicho kitakuwa
kimekamilisha uteuzi wa wagombea ubunge na uwakilishi.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na
Uchaguzi wa chama hicho, Shaweji Mketo alisema kati ya wagombea
waliojitokeza mpaka sasa kuwania nafasi hiyo ya urais ni Profesa Lipumba
pekee.
“Kwa
upande wangu mie kama Mkurugenzi wa Uchaguzi nina imani na Profesa
Lipumba, kuwa hatakuwa ndiye mgombea wetu wa urais tu kwa CUF bali hata
kwa upande wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),”alisema Mketo.
Alisema
kwa mujibu wa makubaliano baina ya Ukawa, kila chama ni lazima kichague
na kuweka wagombea katika nafasi na majimbo yote ikiwemo Urais na
baadaye ndipo watakapochambua ni wagombea wangapi wabaki na akina nani
waondoke na kwa nini.
Akizungumzia
ratiba ya kuchukua fomu na kura ya maoni kwa wagombea wa chama hicho,
alisema chama hicho kimeamua kujiandaa mapema kutafuta wagombea
watakaokiwakilisha katika uchaguzi huo mkuu ambao pia watachujwa kupitia
utaratibu wa kura za maoni.
Alisema
kwa upande wa wanaotaka kuwania nafasi ya udiwani, fomu zitaanza
kutolewa Machi Mosi hadi Machi 10, mwaka huu, na fomu hizo ambazo kila
atakayezichukua atazilipia Sh 10,000 zitafikishwa kwa Katibu wa Kata
Machi 11 hadi 13 mwaka huu kwa ajili ya utaratibu wa juu zaidi.
Kwa
upande wa nafasi ya ubunge, alisema fomu hizo zitakazolipiwa Sh 50,000
zitaanza kutolewa nazo Machi Mosi hadi Machi 10, na Machi 15 hadi 30
mwaka huu, mikutano ya kata ya kura za maoni kwa nafasi ya udiwani
itaanza kufanyika.
Mketo
alisema kuanzia Machi 11 hadi 20, mwaka huu, Katibu wa kata wa chama
hicho atazifikisha fomu za wagombea nafasi ya ubunge kwa Katibu wa
wilaya na baada ya hapo maandalizi ya mikutano mikuu ya wilaya kwa ajili
ya kura za maoni itaanza kuanzia Machi 31 hadi Aprili 4, mwaka huu.
Alisema
kuanzia Aprili 5 hadi 15 mwaka huu, mikutano ya wilaya na majimbo ya
kura ya maoni itafanyika na baada ya hapo Kurugenzi itafanya uchambuzi
wa fomu za wagombea ubunge ili kuziwasilisha kwa Kamati ya Utendaji ya
Taifa kuanzia Aprili 17 hadi 19, mwaka huu.
Aidha
alisema kikao cha Kamati ya Taifa kwa ajili ya kuweka sifa za wagombea
ubunge kinatarajiwa kufanyika kuanzia Aprili 20 hadi 21, mwaka huu, na
kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kitafanyika kuanzia Aprili 22
hadi 23, mwaka huu.
Na
kuanzia Aprili 24 hadi 25, mwaka huu, chama hicho kupitia Baraza Kuu la
uongozi kitafanya uteuzi wa mwisho kwa wagombea wa ubunge na
uwakilishi.
Kuhusu
ratiba ya kuchukua fomu kwa wagombea wa urais, alisema bado wanasubiri
kikao cha pamoja cha Ukawa ambacho kitafanyika muda wowote kuanzia sasa,
kitakachoweka taratibu za kuwatafuta wagombea urais.
Pamoja
na hayo, Mketo alitupia lawama Jeshi la Polisi na kulituhumu kutumiwa
vibaya na chama cha CCM, ambapo wanachama wake takribani nane waliopo
mikoa ya Kusini wamekamatwa kwa tuhuma za ugaidi na hadi sasa
hawajafikishwa mahakamani.
“Katika
uchaguzi wa Serikali za Mitaa chama chetu kilifanya vizuri katika
maeneo yote ya kusini na kutokana na matokeo haya, tuna uhakika wa
kufanya vizuri katika uchaguzi wa wabunge, sasa CCM wameona hivyo
wanatumia polisi, kukamata viongozi wetu wanaoona ni tishio kwa
kisingizio cha ugaidi,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269