Breaking News

Your Ad Spot

Feb 16, 2015

Dawa Zilizopigwa MARUFUKU Zazagaa Mitaani....Wananchi Wataka TFDA Ichue hatua za Haraka kuwanusuru


Licha ya Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi (TFDA) kufuta usajili na kupiga marufuku uuzaji wa dawa duni, zenye madhara na zisizofaa kwa matumizi ya binadamu, dawa hizo zimegundulika kuuzwa holela na baadhi ya wamiliki wa maduka ya dawa  katika kata ya Kisesa wilayani Magu mkoani Mwanza.

Hayo yameelezwa na wakazi wa Kisesa wilayani hapa, wakati wa semina ya siku moja iliyojadili visababishi vya  ulemavu katika jamii, ambapo walisema madhara ya ulemavu yanatokana na watu kutumia dawa zilizopita muda wake.
 
Semina hiyo ilihudhuriwa na washiriki zaidi ya 50 kutoka katika makundi ya walemavu wa kutoona, viungo, kutosikia, uono hafifu, ngozi na watendaji wa vijiji na vitongoji, iliyoandaliwa na asasi ya watu wenye ulemavu ya SANJO na kufadhiliwa na Shirika la the Foundation for Civil Society. 
 
Wananchi hao waliiomba Serikali kupitia TFDA, kuwachukulia hatua wamiliki hao wa maduka wanaoendelea kuuza dawa hizo zilizofutiwa usajili kwa madai kuwa zinaweza kuwasababishia madhara na pengine vifo. 
 
Dawa zilizofutiwa usajili na TFDA ni dawa ya kutibu fungus (ya vidonge na kapsuli) aina ya Ketoconazole, dawa za kutibu mafua na kikohozi za maji, vidonge na kapsuli zenye kiambato hai aina ya phenylpropanol amine na dawa ya kuua bakteria ya sindano, aina ya Chloramphenicol Sodium Succinate.
 
Zingine ni dawa ya kuua bakteria ya maji na kapsuli aina ya cloxacillin, malaria ya vidonge yenye mchanganyiko wa Sulphadoxine na Pyrimethamine(SP) na  dawa aina ya Amikacin, Levofloxacin.
 
Watoa huduma pia waliagizwa kusimamia mabadiliko ya matumizi ya dawa aina ya SP ili ziweze kutumika kwa wajawazito tu na dawa aina ya kanamycin, amikacin na Levofloxacin zitumike kwa wagonjwa wa kifua kikuu tu kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati. 
 
Akizungumza katika semina hiyo, mkazi wa Kisesa, Romanus Kalista alisema licha ya Serikali kupitia TFDA kubaini kuwepo kwa dawa duni kwa watumiaji na kufuta usajili wake kwa matumizi ya binadamu, anaona hali hiyo imewachanganya wananchi kutokana na ukweli wananchi wengi kabla ya kufutiwa usajili, walikuwa wakizitumia.
 
“Dawa hizi hizi zimetumiwa na wananchi kwa muda mrefu, je wananchi waliokuwa wakizitumia endapo watagundulika kupata madhara nani atawahudumia, na ukweli ni kuwa kama zilikuwa na madhara wananchi nao watakuwa wameathirika”, alihoji.
 
Aliongeza,  “Hata hivyo dawa hizo zilizopigwa marufuku bado zinatumika hapa Kisesa na TFDA bado haijatoa elimu ya kutosha kwa wananchi, na kibaya ni kwamba dawa hizi bado zinauzwa kwenye maduka ya dawa.”
 
Alisema yeye binafsi anashangaa kusikia serikali imetangaza kufuta usajili wa baadhi ya dawa zilizoharibika, ambazo vijijini zilikuwa zinatumiwa na wananchi na kuhoji kuwa kama dawa hizo hazina ubora ni kwanini zisipigwe marufuku zinakotengenezwa hususan viwandani. 
 
Kwa upande wake, Agnes Mathias ambaye ni mkazi wa Kisesa na ambaye alikiri kuwa aliwahi kufanya kazi ya kuuza dawa katika duka la dawa, aliitaka Serikali itoe elimu zaidi kwa umma.
 
“Bado dawa zilizopigwa marufuku zinauzwa huku kwetu, mimi nilikuwa muuzaji najua mbinu zinazotumika kuuza dawa, wauzaji wanauza kwa kufungua mlango kidogo, ningeomba serikali ingetuma wataalam waje kufanya ukaguzi vinginevyo madhara yatakuwa makubwa”, alionya.
 
Kwa upande wake, mkazi wa Kisesa John Alphonce licha ya kuitaka Serikali kupambana na mila potofu juu ya watu wenye ulemavu, alisema kuwa baadhi ya dawa wanazotumia akinamama wajawazito husababisha ulemavu kwa mtoto anayezaliwa. 
 
“Na kwa sababu hiyo mimi sikubaliani na hoja kuwa ulemavu ni mpango wa Mungu, inawezekana mama anaweza akawa amemeza dawa au kuchomwa sindano wakati wa ujauzito na baadae mtoto anayezaliwa hupata ulemavu”, alisema.
 
Mwezeshaji wa semina hiyo, Mwanasheria wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Mwanza (CHAWATA), Revocatus Almasi  aliitaka jamii kushiriki kamilifu katika kukabiliana na changamoto zinazowapata watu wenye ulemavu nchini na waachane na mila potofu. 
 
“Kutokana na mila zilizopitwa na wakati, jamii inaamini kuwa watu wenye ulemavu ni tegemezi, wasio na uwezo,wanastahili kusaidiwa na watu wasio na ulemavu ili waweze kumudu maisha yao”, alisema.
 
Mkurugenzi wa SANJO, Joseph Msuka alisema lengo la semina hiyo ilikuwa ni kuelimisha jamii kupitia kwa watu wenye  ulemavu na watendaji wa vijiji na kata wajue madhara yakuteketeza watoto wanaozaliwa na ulemavu kunakofanywa na baadhi ya watu katika jamii, hasa wanaume na baadhi ya akinamama kutumia dawa zilizopita muda wake wa matumizi.
 
Akizungumza na Mpekuzi kwa njia ya simu kutoka mkoani Iringa, Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Ziwa, Moses Mbamba alisema wamiliki wa dawa wanaouza dawa hizo zilizofutiwa usajili, wanajali zaidi kutafuta pesa kwa gharama ya maisha ya watu kuliko kujali uhai wa binadamu. Alisema ofisi yake itafanya ukaguzi wa haraka katika eneo hilo. 
 
“Kesho nitamuagiza msaidizi wangu aende huko mara moja kufanya ukaguzi na watakaobainika tutawafikisha mahakamani mara moja, hatutakubali wao kuendelea kuuza dawa zilizofutiwa usajili,” aliahidi.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages