Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
Dar
es Salaam. Matukio ya wasafiri kukamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere (JNIA) wakiwa na nyara za Serikali na dawa za kulevya,
yanazidi kuchukua sura mpya baada ya raia mmoja wa Ubelgiji kukamatwa
akiwa na fuvu la binadamu.
Raia
huyo, Balcjan Christine Weejktgns (49), alikamatwa Jumatatu saa 2.30
usiku wakati akiwa katika taratibu za kuingia uwanjani hapo tayari kwa
safari ya kuelekea Ubelgiji kupitia Zurich, Uswisi.
Tukio
la kukamatwa kwa Mbelgiji huyo ni mwendelezo wa matukio ya aina yake
uwanjani hapo baada ya watu wengine wawili kukamatwa kwa nyakati tofauti
kwenye uwanja huo wakiwa na kucha za simba na kenge walio hai.
Kamanda
wa Polisi Viwanja vya Ndege, Hamisi Selemani alisema mtu huyo alikutwa
ameficha fuvu hilo la binadamu kwenye mfuko wa plastiki.
“Alivyopita
kwenye mashine za ukaguzi tulimtilia shaka na tulipompekua tulimkuta
amebeba fuvu la kichwa cha binadamu kikiwa kimewekwa kwenye mfuko wa
plastiki ndani ya sanduku alimokuwa ameweka nguo zake na vitu
mbalimbali,” alisema Selemani.
Raia
huyo anadaiwa kuwa ni mkazi wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) mkoani
Morogoro na inadaiwa kuwa alikuwa nchini kwa ajili ya kufanya utafiti.
Kamanda
Selemani alisema baada ya askari wa kikosi cha polisi cha JNIA kumhoji
kwa undani madhumuni ya kubeba fuvu, alisema ni mali yake na kuwa
alikuja nalo nchini kutoka Ubelgiji.
“Kwa
maelezo yake alidai kuwa fuvu hilo analimiliki muda mrefu tangu
alipoingia nchini mwaka 2000 akitokea Ubelgiji akidai kuwa yeye ni
mtafiti,” alisema.
Pamoja
na raia huyo wa Ubelgiji kujitetea kuwa ni mtafiti, Kamanda Selemani
alisema sheria za nchi haziruhusu mtu kumiliki viungo vya binadamu hivyo
anayekiuka lazima akamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Jeshi
la polisi haliwezi kuona taratibu za nchi zikivunjwa hata kama ni raia
wa kutoka nje ya nchi ambaye amekuja kufanya utafiti nchini. Lazima
afuate sheria,” alisema na kuongeza:
“Wito
wangu ni kwamba watu wote wanatakiwa kufuata taratibu za nchi. Huyu
raia ameona kitu cha kawaida kuishi na fuvu la kichwa, lakini hapa ni
tofauti na nchini kwao,” alisema.
Alisema
polisi inaendelea na upelelezi ili kujua sababu ya Mbelgiji huyo
kusafirisha fuvu hilo na kuahidi kuwa uchunguzi ukikamilika, atafikishwa
mahakamani.
Pamoja
na kuwa tukio hilo ni la aina yake, si geni kwenye uwanja huo ambao una
historia ya upitishaji wa vitu mbalimbali kinyume cha sheria.
Januari
7, Polisi wa JNIA walimkamata raia wa Kuwait akiwa na viumbe hai aina
ya kenge 149 wenye thamani ya Sh6.3 milioni ambao walikuwa
wakisafirishwa kwenda Kuwait.
Agosti
mwaka jana, Raia wa Vietnam, Dong Van (47), alikamatwa uwanjani hapo
akiwa na meno 65 na kucha 447 za simba zenye thamani ya Sh189.4 milioni.
Van alikamatwa akijiandaa kwa safari ya kuelekea Vietnam kwa kutumia ndege ya Shirika la Qatar kupitia Doha.
Raia
huyo alikamatwa na nyara hizo akiwa amepakia katika begi lake la nguo
huku zikiwa zimefungwa vizuri katika pakiti za mchele na kahawa. Baada
ya kupita kwenye mashine za ukaguzi ilibainika kuwa begi hilo lilikuwa
na pakiti 22, kati ya hizo saba zilikuwa na meno pamoja na kucha za
simba.
Chanzo:-Mwananchi
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269