Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa Siku mbili wa Kanda
unaozungumzia changamoto za ukuaji wa Miji pamoja na kushughulikia
hali ya baadaye ya Miji ya Afrika unaofanyika katika Hoteli ya Hyatt
Regency Kilimanjayo Mjini Dara es Salaamu.
Baadhi
ya washiriki wa Mkutano wa Siku mbili unaozungumzia changamoto za
ukuaji wa Miji pamoja na kushughulikia hali ya baadaye ya Miji ya Afrika.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif pamoja na Viongozi na
washiriki wa Mkutano huo wakifuatilia mada inayohusu Miji inavyoweza
kukuza uchumi iliyotolewa na Mtaalamu wa masuala ya Uchumi kutoka Sweden
Dk. David Simon.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd akiwa
pamoja na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi wa Afrika kwa Maendeleo
endelevu (Uongozi Institute), Profesa Joseph Semboja wakielekea kwenye
ukumbi wa Mikutano kwa ajili ya ufunguzi wa Mkutano unaozungumzia
changamoto za ukuaji wa Miji pamoja na kushughulikia hali ya baadaye ya
Miji ya Afrika. (Picha zote na Hassan Issa–OMPR – ZNZ)
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
19/2/2015.
MAKAMU wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba ujenzi wa
nyumba za Mkopo pamoja na bei nafuu na kulengwa kwa wananchi wenye
kipato cha kawaida katika maeneo ya Miji na vitongoji vyake ndio njia
pekee itakayosaidia mfumo mzuri katika uwekaji wa mipango Miji.
Alisema
ujenzi holela usiozingatia Mipango Miji unaoendelea kukua siku hadi
siku katika maeneo ya miji hasa ile ya Jumuyia ya Afrika Mashariki mara
nyingi huleta athari wakati yanapotokea mafuriko au majanga ya moto.
Balozi
Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiufungua Mkutano wa Siku mbili wa
kanda unaozungumzia changamoto za ukuaji wa Miji pamoja na
kushughulikia hali ya baadaye ya Miji ya Afrika unaofanyika katika
Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjayo Mjini Dara es salaamu.
Mkutano
huo uliopewa jina la Maisha ya baadaye ya Nchi za Afrika Mashariki,
jinsi gani tunataka kuishi mwaka 2050 umeandaliwa na Taasisi ya Uongozi
wa Afrika kwa Maendeleo endelevu { UONGOZI INSTITUTE }.
Alisema
asilimia kubwa ya wananchi wa kawaida huishi kwa kujenga makaazi yao
kwenye maeneo hatarishi ambayo wakati yanapotokea maafa au mafuriko
Wananchi hao wanashindwa kupata huduma muhimu za lazima kutokana na
uharibifu wa mazingira na matokeo yake hukumbwa na miripuko ya maradhi
yanayosababisha kupoteza idadi kubwa ya maisha ya watu.
Balozi
Seif alizinasihi Taasisi, wataalamu na Viongozi wanaosimamia Mipango
Miji kuelewa kwamba ili kufikia malengo ya maisha bora ya Jamii pamoja
na kukuwa kwa miji bado ipo haja ya kuimarishwa miundo mbinu ya huduma
muhimu za lazima katika Halmashauri za Mikoa, Wilaya na Vijiji ili
kupunguza kasi ya ukuaji wa miji Mikubwa.
Mapema
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi wa Afrika kwa Maendeleo endelevu {
Uongozi Institute } Profesa Joseph Semboja alisema upo uwiano mkubwa wa
ongezeko la watu Barani Afrika na Dunia kwa ujumla.
Profesa
Semboja alisema ongezeko hilo linasababisha msongamano wa shinikizo la
uhaba wa makaazi ya watu , ufinyu wa fursa za ajira hasa kwa vijana
pamoja na huduma za Kijamii.
Alisema
ukanda wa Afrika Mashariki unaendelea kukumbwa na changamoto mbali
mbali za tabia nchi, mazingira sambamba na ongezeko kubwa la idadi ya
wakaazi wake katika Miji ya Nchi hizo.
“
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi { UN
Habitat } hali ya Miji ya Afrika 2014, Afrika Mashariki inashika nafasi
ya chini katika Miji inayokuwa Duniani lakini ndio kanda inayoongoza
katika kasi ya ukuaji wa Miji yake kwa sasa “. Alisema Profesa Semboja.
Alifahamisha
kwamba ifikapo mwishoni mwa muongo huu wa sasa idadi ya wakaazi waishio
Mijini itaongezeka kwa asilimia 50% na jumla ya idadi ya wakaazi wa
mijini ifikapo mwaka 2040 inatarajiwa kuwa mara tano ya mwaka 2012.
Profesa
Semboja alieleza kwamba lengo la Mkutano huo wa kanda unaokutanisha
Viongozi na watunga sera kutoka nchi za Afrika mashariki umelenga
kujadili namna ya kutatua changamoto hizo na kufikiria miji ambayo
itatimiza matakwa yaliyokusudiwa.
Akitoa
salamu za shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi { UN Habitat }
Mwakilishi wa shirika hilo Dr. Remy Sietchiping alisema nguvu za
Viongozi wa Kisiasa zitumike katika kusaidia Taaluma ya ujenzi wa
Mipango Miji.
Dr. Remy alisema mipango hiyo lazima iende sambamba katika kukabiliana na ongezeko kubwa la idadi ya watu.
Alifahamisha
kwamba Shirika hilo la Habitat litahakikisha kwamba linatumia nguvu na
uwezo wake katika kusaidia Taaluma ya upangaji wa Miji Barani Afrika.
Washiriki
wa Mkutano huo kutoka Nchi za Burundi, Ethiopia,, Kenya, Rwanda,
Somalia, Sudani ya Kusini, Uganda na wenyeji Tanzania wengi wao ni
watendaji wa ngazi za juu Serikalini, mshirika ya Kikanda na Kimataifa,
Miji Mikubwa, wasomi, Sekta Binafsi na Taasisi za Kiraia.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269