Breaking News

Your Ad Spot

Feb 19, 2015

TACCEO KUTUMA WAANGALIZI 160 NCHINI KOTE KUANGALIA UANDIKISHAJI WAPIGAKURA

Ofisa Mratibu wa Shughuli za Uchaguzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hamis Mkinde (kushoto), akisisitiza jambo wakati akizyungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, leo, kuhusu Mtandao wa Asasi za Kiraia wa kuangalia Chaguzi Tanzania (Tacceo) kutuma waangalizi 160  nchi nzima kwa ajili ya kuangalia uandikishaji wapiga kura kwa kutumia mfumo mpya wa BVR katika wilaya zote za Tanzania Bara. Kulia ni Mwenyekiti wa mtandao huo, Martina Kabisama.

Na Dotto Mwaibale
MTANDAO wa Asasi za Kiraia wa kuangalia Chaguzi Tanzania (Tacceo) unategemea kutuma waangalizi 160  nchi nzima kwa ajili ya kuangalia uandikishaji wapiga kura kwa kutumia mfumo mpya wa BVR katika wilaya zote za Tanzania Bara.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa TACCEO Martina  Kabisama wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuhusu uangalizi wa uandikishaji wapiga kura kwa mfumo wa teknolojia ya alama (BVR), unaotarajia kuanza Februari 23, 2015 mkoani Njombe na kuendelea nchi nzima.

"Tunapenda kutamka kuwa lengo kuu la uangalizi tunaotarajia kuufanya ni kuanisha mambo chanya na mapungufu yanayoweza kujitokeza wakati wa mchakato wa uandikishaji wapiga kura unaotarajiwa kuendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kuweza kushauri namna ya kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga kura kwa ajili ya kura ya maoni na uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu na chaguzi zingine zitakazofuata" alisema Kabisama.

Alisema lengo lingine ni kuona kuwa mapungufu yote yanafanyiwa kazi na yanarekebishwa mapema ili uchaguzi ujao uwe bora na wenye tija na manufaa kwa watanzania wote.

Alisema madhumuni makubwa ya uangalizi huo ni mchakato mzima na ushirikiashwaji wa wananchi wa kujiandikisha wa upigaji kura, kushuhudia ni jinsi gani mfumo wa sheria ya uchaguzi unavyomtambua na kumpa fursa mwananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la Mpiga kura.

Alitaja madhumini mengine kuwa ni makundi mbalimbali yakiwemo ya walemavu na yale yaishio pembezo yanavyoshirikishwa katika jambo hilo ikiwemo elimu ya uraia pamoja na kutathmin utendaji kazi wa mashine za BVR na mengineyo.
Kabisama alisema mtandao huo unatumia fursa hiyo kueleza kuwa hauridhishwi jinsi mchakato wa uandikishaji wapiga unavyokwenda kwa kusuasua na kukosa uwazi jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa Taifa letu.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages