Breaking News

Your Ad Spot

Feb 20, 2015

THBUB YALAANI MAUAJI YA MTOTO YOHANA BAHATI

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa na mauaji ya kikatili ya mtoto Yohana Bahati aliyetekwa nyara hivi karibuni katika kijiji cha Ilelema, Chato Mkoani Geita.
Pia Tume inalaani kuumizwa kwa mama yake, Ester Jonas wakati anatetea uhai wa mwanae wakati wa tukio lililotokea Februari 15, 2015.
Tume inapenda kuwakumbusha wananchi kwa ujumla kuwa vitendo vya ukatili wanaofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi, ni matukio ya ukiukwaji wa Sheria na haki za kibinadamu. Matukio haya yanaonesha yamekuwa yakichagizwa na imani za kishirikina hivyo Tume inakemea matendo haya na kutaka yapigwe vita.
Chini ya Katiba na Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu Serikali inao wajibu wa kulinda raia wake. Tume inaiomba Serikali kuwatafuta wale wote wanaohusika na vitendo hivi na kuwafikisha mbele ya vyombo vya Sheria.
Aidha, Tume inaungana na wananchi, wadau mbalimbali na Serikali kulaani vikali mauaji ya mtoto Yohana Bahati na kujeruhiwa vibaya mama yake wakati akitetea haki ya mwanae kuishi katika jamii huru, na inakemea vikali vitendo hivyo vya kikatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa ujumla.
Tume inaikumbusha Serikali kuwa wakati umefika wa kufanyia marekebisho makubwa Sheria ya Uchawi (Sura ya 18 ya 1928) au kutunga Sheria mpya ili kupiga marufuku vitendo vyote vinavyoendeleza imani za uchawi na ushirikina.
Tume inashauri pia Serikali kupitia upya Sheria inayowatambua waganga wa jadi (Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala).
Tume inatoa wito kwa wananchi na jamii yote kwa ujumla kuachana na imani potofu zenye mtizamo hasi kwamba mafanikio yoyote yanaweza kupatikana kwa njia za kishirikina.  Tume inakumbusha wananchi kuwa mafanikio yoyote yatapatikana kwa kufanya kazi zote halali kwa bidii, na siyo kwa njia za kishirikina ikiwemo kutumia viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Tume inaungana na wananchi na Serikali kupiga vita vitendo hivi vya kikatili.
Pia Tume inatoa pole kwa mama aliyeumizwa akitetea uhai wa marehemu mwanae.
Mwisho Tume iko mbioni kwa kushirikiana na wadau wengine kutekeleza mpango wa kitaifa wa kuelimisha wananchi ili kuepusha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini. Tume inaomba wananchi wote kushirikiana katika jukumu hili.
Imetolewa na:
Mhe. Bahame Tom Nyanduga (Pichani Juu)
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Februari 19, 2015:

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages