Mhandisi
wa Kiwanda cha Matrekta Mbweni Haji Wa Haji Makame akimpatia Maelezo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi moja ya Mashine
zinazotumika Kiwandani hapo.
Balozi Seif akiangalia Mashine inayotumika katika uburugaji wa mashamba ya Mpunga.
Mkuu
wa Kitengo cha Ufundi katika Kiwanda cha Matrekta Mbweni Mhandisi Moh’d
Omar Moh’d (wapili kulia) akimueleza Balozi Seif juhudi za Kiwanda
hicho licha ya utengenezaji wa vyombo vya moto lakini pia hutoa mafunzo
ya Ufundi kwa vijana wanaomaliza masomo ya sekondari. Wa mwanzo kutoka Kulia ni Mhandisi mwenzake wa Kiwanda hicho Haji Wa Haji Makame. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/3/2015.
UKOSEFU
wa fungu maalum la matumizi pamoja na upungufu wa vipuri vya
utengenezaji wa vyombo vya moto katika Kiwanda cha Matrekta Mbweni ndio
changamoto ya msingi inayosababisha watendaji wa kiwanda hicho kufanya
kazi katika kiwango kisichoridhisha.
Mkuu
wa Kitengo cha ufundi katika kiwanda hicho Mhandisi Moh’d Omar Moh’d
alieleza hayo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi aliyefanya ziara ya ghafla kwenye karakana ya Kiwanda hicho
kuangalia uwajibikaji wa watendaji hao hapo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa
Zanzibar.
Mhandisi
Moh’d Omar Moh’d alisema changamoto hiyo kubwa wakati mwengine
hupelekea baadhi ya Taasisi za Umma na hata zile binafsi husita
kupelekea vyombo vyao vya moto kwa ajili ya kupata huduma za matengenezo
ya kiufundi.
Alisema
Kitengo hicho licha ya kwamba hakina kifungu cha fedha lakini watendaji
wake hulazimika kufanya kazi wakati wote kutegemea huduma
wanazozipokea kituoni hapo hasa zile za Matrekta ya Wizara ya Kilimo na
Mali Asili.
Alieleza
kwamba Kiwanda hicho hivi sasa kimepokea Matrekta kadhaa kutoka Wizara
ya Kilimo na Mali Asili ambayo yanahitaji marekebisho ya kiufundi ili
yawahi kurejea kutoa huduma za kilimo mashambani Unguja na Pemba.
Mkuu
huyo wa Kitengo cha Ufundi Kiwanda cha Matrekta Mbweni alifahamisha
kwamba Kitengo hicho hivi sasa kinaendelea na mpango wa kushirikiana na
Kampuni ya ufundi ya Mahindra ya Nchini India kwa lengo la kujiimarisha
kiufundi ili kiendelee kutoa huduma za Kimataifa.
Mhandisi
Moh’d alifafanua kuwa wataalamu wa Kiwanda hicho wako katika hatua ya
kukamilisha mapendekezo yatayopelekwa kwenye Uongozi wa Kampuni hiyo
ya Mahindra kwa hatua zaidi.
Alieleza
kwamba Mpango huo wa maombi umeainisha pia namna Kiwanda hicho
kinavyotaka kujiimarisha zaidi katika utoaji wa mafunzo ya ufundi ngazi
ya cheti kwa vijana wanaoamua kuchukuwa fani hiyo.
“
Tunaendelea kufundisha vijana wetu wanaomaliza masomo yao ya sekondari
kwa vile tayari tumeshapata idhini ya Nacte na tunafarajika zaidi kwa
vile masomo ya vijana hao huambatana na mazoezi ya vitendo hapa hapa
Kiwandani “. Alisema Mhandisi Moh’d.
Naye
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwapongeza watendaji
wa Kiwanda cha Matrekta Mbweni kwa juhudi wanazoendelea kuchukuwa katika
utekelezaji wa majukumu yao licha ya changamoto zinazowakabili kila
siku.
Balozi
Seif alielezea faraja yake kutokana kwamba vifaa na mashine nyingi
zilizopo Kiwandani hapo bado zinaendelea kutumika tokea kuanzishwa kwa
Kiwanda hicho mwaka 1967.
“
Kazi mnazozifanya mnastahiki kupongezwa hasa ikizingatiwa kwamba
mashine zenu ni zile zile mnazozitumia za mwaka 1967 “. Alisema Balozi
Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliufahamisha Uongozi wa Kiwanda hicho
pamoja na watendaji wake kwamba Serikali Kuu itaangalia namna
itakavyoweza kusaidia kukwamua changamoto zinazokikabili Kiwanda hicho.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269