Wachezaji wa Yanga wakisherekea ubingwa wa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Azam FC kwa penati
Yanga wametwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii baada ya kuilaza timu ya Azam FC kwa mikwaju ya penati 8-7 baada ya sare ya bila kufungana kwenye mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Azam wameshindwa kufuta uteja kwenye kuwania ngao hiyo, ambapo tangu wameanza kupata fursa ya kuiwania mara zote wamejikuta wakipoteza michezo yao na kuikosa ngao hiyo ambayo inaashiria kufunguliwa rasmi kwa pazia la ligi kuu Tanzania bara.
Golikipa wa Yanga Ali Mustafa ‘Barthez’ ameibuka shujaa kwenye mchezo wa leo akifanikiwa kupangua penati mbili za wachezaji wa Azam na kuipa ubingwa timu yake.
Ushindi wa leo kwa Yanga ni sawa na wamelipa kisasi baada ya kiondolewa na Azam kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya Kagame mwezi Julai mwaka huu kwa changamoto za penati ambapo leo Azam nao wamepoteza mchezo wao kwa mikwaju ya penati.(P.T)
Kila timu
ilipata penati nne kati ya penati tano za kwanza wakati kila timu
ilipoteza penati moja kati ya tano. Baada ya kuwa sare kwa penati 4-4,
timu zote zikaanza kupigiana penati mojamoja ili kumsaka mshindi ndipo
Yanga wakapata penati nne nyingine huku Azam wao wakikosa penati moja na
Yanga akatwaa ubingwa huo.
Kipindi
cha kwanza kilimalizika huku timu zote zikiwa sare ya bila kufungana,
timu zote zilifanya mashambulizi kadhaa wakati wa kipindi cha kwanza
lakini Yanga wakiwa wamefanya mashambulizi mengi zaidi langoni mwa Azam.
Golikipa
wa Azam Aishi Manula alifanya kazi ya ziada kuokoa mipira kadhaa langoni
mwake kufuatia mashambulizi makali yaliyofanywa na Yanga.
Kipindi
cha pili kilianza kwa kasi ambapo Yanga waliliandama lango la Azam
dakika za mapema mwa kipindi hicho lakini bado washambuliaji wake
hawakuweza kufunga goli.
Mchezo wa
leo inaonekana timu zote zilikuwa zimekamia kwani mara kadhaa wachezaji
walikuwa wakifanyiana madhambi na kupelekea mwamuzi kutoa kadi za
njano.
Said Juma
alioneshwa kadi ya njano kipindi cha kwanza kwa kumchezea vibaya
mshambuliaji wa Azam John Bocco ‘Adebayo’. Nadir Haroub ‘Cannavaro’
alioneshwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Bocco kipindi cha pili
wakati Mbuyu Twite yeye alioneshwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya
Farid Mussa . Kwa upande wa Azam kadi ya njano ilitoka kwa Erasto Nyoni
baada ya kumchezea vibaya Saimon Msuva.
Katika
kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko, Yanga walimtoa Said
Juma Makapu na nafasi yake kuchukuliwa na Haruna Niyonzima, Donald Ngoma
akampisha Deus Kaseke na Andrey Coutinho akaingia baada ya Simon Msuva
kupumzishwa. Azam walimtoa Mudathir Yahya na kumuingiza Jean Mugiraneza
huku Ame Ally ‘Zungu’ akiingia kuchukua nafasi ya Frank Domayo.
Mabadiliko
hayo yalizaa matunda kwa upande wa Yanga kwani walicheza vizuri kipindi
chote cha pili wakati Azam wao wakiwa wanazuia zaidi. Kama wachezaji wa
Yanga wangekuwa makini, wangepata goli mapema kipindi cha pili lakini
walipoteza nafasi muhimu za kufunga walizozitengeneza.
Hadi
mwamuzi wa mchezo huo Martin Saanya anapuliza kipyenga cha mwisho
kuumaliza mchezo huo, timu zote zilikuwa sare ya bila kufungana na hapo
ikaidi itumike changamoto ya mikwaju ya penati ili kumpata mshindi.
Wachezaji
waliofunga penati kwa upande wa Yanga ni Haruna Niyonzima, Deus Kaseke,
Amis Tambwe, Andrey Coutinho, Godfrey Mwashiuya, Thaban Kamusoki, Mbuyu
Twite na Kelvin Yondani huku penati ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’
ikipanguliwa na mlinda mlango wa Azam Aishi Manula.
Kipre
Tchetche, John Bocco, ‘Adebayor’, Himid Mao, Agrey Morris, Jean
Mugiraneza, Erasto Nyoni na Shomari Kapombe walifunga penati zao kwa
upande wa Azam wakati Pascal Wawa na Ame Ally ‘Zungu’ wao penati zao
ziliokolewa na Ali Mustafa ‘Barthez’.
Chanzo:Shaffihdauda.com
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269