Breaking News

Your Ad Spot

Dec 23, 2015

WALIMU WAASWA KUWA WAZALENDO

Baadhi ya sampuri zilizokusanywa na washiriki wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Walimu na Wanafunzi katika Ufundishaji na Ujifunzaji kwa shule za sekondari (STEP) kwa ajili ya kufundishia la Biolojia kulingana na mazingira waliopo.

(Picha na Eleuteri Mangi-MAELEZO)
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Walimu nchini wametakiwa kuwa wazalendo kwa kuhakikisha wanawafundisha wanafunzi katika muda waziada ili kuwaongezea uwezo wa ufaulu katika mitihani yao.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu Bw. Zuberi Samataba wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Walimu na wanafunzi katika ufundishaji na Ujifunzaji kwa shule za sekondari (STEP) yanayoendelea katika mikoa sita nchini.

Aidha, Bw. Samataba aliwataka walimu wasihangaike kutafuta michango kwa ajili ya uendeshaji wa shule na badala yake wajikite katika kufundisha na kuwasaidia wanafunzi kupata elimu na kufaulu masomo yao kwa kuwa Serikali ndiyo itafanyakazi ya kuhakikisha fedha za uendeshaji wa shule na vifaa vinapatikana kwenye shule zote za Serikali nchini.

Mafunzo hayo ni ya siku tano (5) ambayo yanashirikisha walimu wa shule za sekondari wapatao 2,528 yameanza kufanyika kuanzia Desemba 19, 2015 na yanatarajia kumalizika Desemba 23, 2015 

Mafunzo hayo yanayolenga kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi katika ufundishaji na ujifunzaji yanafanyika kwa awamu ambapo katika awamu ya pili yanafanyika katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Iringa, Singida na Katavi na hatimaye kufanyika katika mikoa yote nchini.

Katika awamu ya kwanza ya mafunzo ya  STEP  iliyofanyika mwezi Juni, 2015 ilishirikisha mikoa ya Mwanza, Dodoma, Geita, Mara, Simiyu, Shinyanga na Tanga ambapo walimu wa sekondari wapatao 3,880 walipatiwa mafunzo hayo.

Katika kila awamu ya mafunzo, walimu wane wa masomo ya Kiswahili, Hisabati, Biolojia na Kiingereza kutoka kwenye shule za sekondari katika Halmashauri na Mkoa husika wanashiriki katika mafunzo katika vituo mbalimbali vinavyoandaliwa na mikoa husika.

Katika mafunzo hayo, walimu wanajengewa uwezo wa kuwawezesha kuwatambua wanafunzi wenye uwezo mdogo kimasomo na walio katika hatari ya kufeli mitihani ya Taifa kwa kuwapatia mafunzo rekebishi kwa lengo la kuwawezesha kufaulu mitihani yao.

Mafunzo yanayotolewa ni sehemu ya utoaji wa mafunzo ya walimu kazini ikiwa ni utekelezaji wa Programu ya kuboresha taaluma ya Walimu na Wanafunzi wa shule za Sekondari ambayo ni mojawapo ya Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Programu ya STEP ilibuniwa na Serikali kwa lengo la kubadilisha hali ya kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi na kuboresha kiwango cha ufaulu kwa kuwawezesha walimu kujenga tabia ya kuwatambua wanafunzi wenye uwezo mdogo kimasomo na walio katika hatari ya kufeli Mtihani wa Taifa kwa kuwasaidia kufanya Mafunzo Rekebishi. 

Ili kuyafanya mafunzo ya nayotolewa kufanyika kwa ufanisi, Ofisi ya Rais,TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeandaa miongozo ya masomo husika unaotumika kuwafundishia walimu hao.

Mafunzo ya STEP yanatekeleza azma ya Serikali chini ya mpango wa BRN unaolenga kuweka mfumo thabiti wa kusimamia, kufuatilia na kutathmini mipango yake hususan Mpango wa Kupunguza na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA) na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

BRN ni mfumo ambao umejikita katika kuweka vipaumbele, kufanya ufuatiliaji makini na uwajibikaji katika kuleta matokeo tarajiwa, Elimu ni mojawapo wa sekta za kipaumbele katika utekelezaji wa BRN nchini.

Sekta ya Elimu inavipaumbele tisa (9) vilivyoainishwa ambavyo ni upangaji wa shule kwa ubora wa ufaulu katika matokeo ya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi na sekondari kidato cha nne, utaratibu wa utoaji tuzo kwa shule zinazofanya vizuri ilikuzipamotisha wa kuendelea kufanya vizuri, kuandaa kiongozi cha kuimarisha utendaji wa shule na kutoa mafunzo kwa wakuu wa shule na kufanya upimaji wa stadi za Kuandika, Kusoma na Kuhesabu (KKK) kitaifa.

Maeneo mengine ya vipaumbele katika sekta ya elimu ni pamoja na kutoa mafunzo ya Ufundishaji wa KKK kwa walimu wa darasa la kwanza na pili, kujenga uwezo wa Walimu na wanafunzi katika Ufundishaji na Ujifunzaji, Ujenzi wa Miundombinu muhimu ya shule, Utoaji wa Ruzuku ya Uendeshaji na Motisha kwa walimu.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages