Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, SACP Justus Mamugisha, akitoa taarifa kwa waandishi wa habari.
Mwanza, Tanzania
Watu wawili wameuawa Jijini Mwanza kwa kupigwa risasi na Majambazi, huku Wengine saba wakijeruhiwa katika tukio la uvamizi wa duka lililokuwa likitoa huduma mbalimbali za kifedha.
Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza, Justus Mamugisha, amesema kuwa tukio hilo lilitokea jana msaa mbili usiku katika eneo la Bugarika Sokoni, baada ya watu watatu wanaosadikika kuwa ni majambazi waliokuwa na bunduki aina ya SMG kuvamia katika duka la mfanyabiashara na mkazi wa eneo hilo aitwae Daniel Marwa (30).
Kamanda Kamugisha amewataja waliouawa kuwa ni Julius Wankaba (30) ambae ni dereva bodaboda, pamoja na mfanyabiashara mmoja mwenye duka katika eneo hilo aliefahamika kwa jina la Mama Yuni (35).
Amewataka waliojeruhiwa kuwa ni Magesa Mungari (38), Simioni Charles (26) ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando huku wengine wakiwa ni Mwita Ryoba (30), Frank Willium (19), Saumu Said (20), Masumbuko Kanduru (38) pamoja na Emmanuel Francis ambao wanapata matibabu katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekour Toure.
Baadhi ya Mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo mmiliki wa duka lililovamiwa, wanasema majambazi hao walipofika eneo la tukio walianza kufyatua risasi ovyo ili kuwatawanya wananchi waliokuwa wamekusanyika katika eneo hilo wakiangalia taarifa ya habari na wengine wakinywa kahawa, na hivyo kusababisha wananchi kutawanyika jambo lililosababisha vifo na majeruhi hao.
Katika tukio hilo, Majambazi hao walifanikiwa kupora fedha taslimu kiasi cha Shilingi Milioni Mbili, Vocha za simu za mitandao mbalimbali zinazokadiliwa kuwa za shilingi Laki Nane pamoja na simu sita za wateja.
Kamanda Kamugisha amesema Jeshi la polisi Mkoani Mwanza limeanzisha msako mkali ili kuwakamata waliohusika na tukio hilo, huku likiahidi zawadi ya fedha kiasi cha shilingi Milioni Moja kwa yeyote atakaesaidia kufanikiwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza linaendelea kumsaka mtu aliehusika na wizi wa mtoto mwenye umri wa siku moja katika Hospitali ya Wilaya ya Magu, ambapo tukio hilo limetokea Machi 23 mwaka huu, majira ya saa nane mchana baada ya mtu mmoja asiefahamika mwenye jinsia ya kike, kufika katika wodi ya wazazi na kumuiba mtoto huyo wakati mama yake amelala.
Aidha katika katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, Jeshi hilo limepiga marufuku watoto kwenda kuogelea katika fukweni (Beach) pamoja na uwepo wa disko toto Jijini Mwanza. Chanzo BONYEZA HAPA.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269