Jeshi
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linapenda kutoa taarifa ya ufunguzi
wa mashindano ya kombe la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF CUP) ambayo
yanatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 24 Mei 2016 katika uwanja wa Uhuru
jijini Dar es salaam. Mgeni rasmi katika ufunguzi huo anatarajiwa kuwa
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe: Nape Nnauye.
Mashindano haya yalianzishwa
mwaka 2014, awali JWTZ lilikuwa likiteua wanamichezo wa kushiriki
michezo ya kimataifa kupitia timu teule za Jeshi hali iliyopelekea
kutovumbuliwa kwa vipaji vipya katika michezo, ikaonekana upo umuhimu wa
kubadili mfumo wa uteuzi. Hivyo kuanzisha mashindano ya Kombe la Mkuu
wa Majeshi (CDF CUP) ambayo huanzia ngazi za vikosi hadi kufikia ngazi
za brigedi.
lengo la mashindano haya ni
kudumisha mshikamano, kuvumbua na kukuza vipaji, pia mashindano hayo
yatatumika katika kuteua kombaini ya timu ya JWTZ itakayoliwakilisha
Jeshi na Taifa kwa ujumla katika mashindano ya michezo ya majeshi na
utamaduni kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayotarajiwa
kufanyika nchini Rwanda mwezi wa nane mwaka huu.
Kauli Mbiu ya mashindano haya ni “Michezo ni Ulinzi na Umoja Daima”
Timu zinazoshiriki mashindano
haya ni Ngome (Makao Makuu JWTZ), Kamandi ya Jeshi la nchi kavu
ikiwakilishwa na timu za Tembo, Faru, Nyuki, Mbuni na Chui, Kamandi ya
Jeshi la Anga, Kamandi ya Jeshi la Wanamaji pamoja na Jeshi la Kujenga
Taifa(JKT).
Mashindano haya yatahusisha
michezo ifuatayo, Mpira wa miguu kwa wanaume, Mpira wa kikapu kwa
wanaume, Mpira wa mikono kwa wanaume, Mpira wa pete kwa wanawake na
Mbio za nyika kwa wanaume na wanawake.Michezo hii itafanyika katika
viwanja vya Twalipo vilivyopo Mgulani pamoja na uwanja wa Uhuru jijini
Dar es salaam.
Mashindano haya yanatarajiwa
kufungwa rasmi tarehe 06 Juni 2016. Mgeni rasmi katika ufungwaji wa
mashindano haya anatarajiwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania
Jenerali Davis Mwamunyange.
Wananchi wote wanakaribishwa hakuna kiingilio.
Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
S.L.P 9203, Dar es Salaam, Tanzania.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269