Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Bodi ya
Filamu Tanzania imetoa siku saba kwa Kampuni ya Usambazaji wa Filamu
ijulikanayo kama ‘Pamoja Film Company’ kuwasilisha nyaraka za filamu
zake ili kukagua na kuhakikisha kama wamefuata sheria na kanuni
zinazosimamiwa na bodi hiyo.
Hatua
hiyo imefikiwa baada ya kampuni hiyo kubainika kukiuka baadhi ya sheria
na kanuni za usambazaji zikiwemo za kutowasilisha miswada ya filamu
(script) kabla ya kuanza kurekodi, kuzitangaza kazi hizo kwenye mitandao
ya kijamii bila ya kuzifikisha Bodi ya Filamu Tanzania Kwa ajili ya
ukaguzi pamoja na kufanya kazi za utengenezaji na usambazaji wa filamu
bila kibali.
Agizo
hilo limetolewa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce
Fissoo alipokuwa akiongea na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Lufingo Exaud
kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwake leo Jijini Dar es Salaam
ambapo amesisitiza kuwa kukiuka sheria na kanuni zinazosimamiwa na bodi
ni kosa kisheria.
“Natoa
siku saba kwa Kampuni hii kuwasilisha miswada ya filamu zake 12
alizozitangaza na kuzisambaza kinyume cha sheria pamoja na kuleta
maelezo kwa maandishi ya kujieleza sababu zilizowapelekea kufanya kazi
hizo bila kibali kutoka bodi”,alisema Fissoo.
Filamu
hizo zilizotolewa na Kampuni hiyo bila kufuata sheria na kanuni ni;
Spompompo, Tanga Raha, Buku 10, Jirani Hafugiki, Mke Sahihi, Chanzo,
Ahsante, Je Alaumiwe, Mwaka wa Tisa, Nyaraka na Kanya Boya.
Fisoo
ameongeza kuwa Bodi imefanya jitihada kubwa kutoa elimu kwa umma kupitia
njia za vipeperushi, kuandaa na kushiriki mikutano na makongamano ya
kitaifa na kimataifa, kushiriki maonesho na maadhimisho ya kisekta na
kitaifa ikiwa na lengo la kuwaelemisha wadau wa filamu kuhusu sheria,
kanuni na miongozo inayosimamia sekta hiyo nchini.
Aidha,
amewaonya wadau wote wa filamu kuacha kukiuka sheria na kanuni
zinazosimamia tasnia ya filamu nchini kwani kufanya hivyo ni kosa kubwa
kisheria, “tunawaonya wadau wote kuacha mara moja tabia hii” alimalizia.
Kwa
upande wake mkurugenzi wa kampuni hiyo, Lufingo Exaud amekiri makosa
yake na ameahidi kulipa faini za makosa yote, pia ameomba msamaha mbele
ya Bodi hiyo na kuapa kuwa hatorudia tena. Kwa kumalizia ameahidi kuwa
balozi mzuri wa Bodi ya Filamu Tanzania na yupo tayari kuwapa elimu
wadau wengine wa filamu nchini ili waweze kufuata sheria na kanuni
zinazoongoza sekta hiyo.
Mbali na
kuahidi kushirikiana na bodi hiyo, Lufingo ameusifia utaratibu wa bodi
wa kurahisisha upatikanaji wa vibali kwani kwa sasa baada ya kuwasilisha
muswada wa filamu kwa ajili ya ukaguzi utapatiwa kibali ndani ya muda
wa siku saba za kazi.(P.T)
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269