Mhe. Waziri Mahiga akiendelea kuzungumza na Waandishi wa Habari kama wanavyoonekana pichani.
=============================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba nchini Tanzania
Makamu wa Rais wa Baraza la Taifa la Jamhuri ya Cuba, Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa anatarajiwa kuwasili nchini tarehe 02 Oktoba, 2016 kwa ziara rasmi ya siku tatu. Lengo la ziara
hiyo ni kukuza na kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo baina ya
Tanzania na Cuba pamoja na kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano. Nchi
nyingine anazotarajiwa kuzitembelea ni pamoja na Uganda, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), Botswana na Zimbabwe.
Shughuli mbalimbali zitakazofanyika wakati wa ziara
Mara
baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere, Mhe. Valdes Mesa atapokelewa na mwenyeji wake Mhe. Samia Suluhu
Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tarehe
03 Oktoba, 2016 Mhe. Mesa atakutana kwa mazungumzo ya faragha na Mhe.
Samia Suluhu Ikulu yakifuatiwa na mazungumzo rasmi kati yao na wajumbe
waliofuatana nao.
Aidha, Mhe. Mesa atakutana kwa mazungumzo mafupi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli.
Baada
ya mazungumzo hayo, Mhe. Mesa na Mhe. Suluhu watakuwa na mkutano wa
pamoja na Waandishi wa Habari kuzungumzia masuala mbalimbali ya
ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba.
Katika
hatua nyingine, Mhe. Mesa atakutana kwa mazungumzo mafupi na Spika wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Y. Ndugai katika
Hoteli ya Hyatt Regency. Baadaye siku hiyo hiyo, atakutana na Ujumbe wa
Chama cha Mapinduzi (CCM) Hotelini hapo kabla ya kushiriki Chakula rasmi
cha Mchana, Ikulu kilichoandaliwa kwa heshima yake na Mwenyeji wake
Mhe. Suluhu.
Mhe.
Mesa ataondoka Dar es Salaam tarehe 03 Oktoba, 2016 alasiri kuelekea
Zanzibar kwa ajili ya kuendelea na ziara yake Visiwani humo. Akiwa
Zanzibar, Mhe. Mesa ambaye atapokelewa na Makamu wa Pili wa Rais wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi atakutana kwa
mazungumzo rasmi na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt.
Ali Mohamed Shein, Ikulu ya Zanzibar.
Tarehe
04 Oktoba, 2016 Mhe. Mesa akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba
atarejea Dar es Salaam akitokea Zanzibar kwa ajili ya kuendelea na ziara
yake ambapo atatembelea Makumbusho ya Taifa.
Uhusiano wa Tanzania na Cuba
Uhusiano
wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Cuba ulianzishwa zaidi ya miaka 50
iliyopita na Viongozi Waasisi wa mataifa haya mawili, Rais Mstaafu wa
Cuba, Mheshimiwa Fidel Castro na Baba wa Taifa, Hayati Julius K.
Nyerere. Tangu Tanzania ipate uhuru Cuba imekuwa ikitusaidia katika
maeneo mbalimbali ikiwemo afya, utamaduni, elimu, michezo, utalii,
nishati, teknolojia na kilimo.
Ushirikiano katika Sekta ya Afya
Tanzania
na Cuba zimekuwa zikishirikiana kwenye sekta ya afya ambapo hadi sasa
kuna jumla ya Madaktari 30 kutoka Cuba wanaofanya kazi kwenye Hospitali
mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar. Kati ya Madaktari hao 10 wapo Bara
na 20 wapo Zanzibar wakiwemo wanaofundisha katika Kitivo cha Tiba, Chuo
Kikuu cha Zanzibar na kutibu katika Hospitali mbalimbali Zanzibar.
Aidha,
katika jitihada za Serikali za kupambana na malaria Serikali ya Cuba na
Tanzania zilikubaliana kujenga Kiwanda cha Viuatilifu vya Kuua
Viluwiluwi vya Mbu ambacho kimejengwa kwenye eneo la Viwanda Wilayani
Kibaha, Mkoani Pwani na kuzinduliwa mwezi Julai, 2015.
Kiwanda
hicho ambacho kilijengwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Maendeleo
la Taifa (NDC) na Kampuni ya LABIOFAM ya Cuba kimekamilika na kwa sasa
kinazalisha dawa za majaribio. Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa
kuzalisha lita milioni 6 za viuatilifu kwa mwaka ambazo zinatosheleza
kwa matumizi ya Tanzania na hata kuuzwa nchi nyingine za Afrika.
Sekta ya Elimu
Katika
Sekta ya Elimu Tanzania na Cuba zimekuwa zikishirikiana kwenye programu
mbalimbali ikiwemo nafasi za ufadhili wa masomo nchini Cuba kwa
wanafunzi kutoka Tanzania. Kuanzia mwaka 2008 hadi 2014 jumla ya
Watanzania 64 walipata ufadhili wa mafunzo nchini Cuba katika fani
mbalimbali ikiwemo udaktari, uchumi, TEHAMA na Michezo.
Pia
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Cuba ilianzisha Programu ya
Elimu kwa Vijana na Watu Wazima ambayo hutolewa kwa kutumia vifaa vya
kufundishia vinavyomwezesha mwanafunzi kusikia na kuona (audiovisual).
Inatarajiwa kwamba zaidi ya vijana na watu wazima milioni 3 watakuwa
wameshiriki programu hii ifikapo mwaka 2017. Mradi wa majaribio ya
program hii ulizinduliwa mwaka 2014 katika Manispaa za Ilala, Temeke,
Kinondoni, Ilemela, Mwanga, Bagamoyo, Mkuranga na Songea.
Sekta ya Michezo
Katika
Sekta ya michezo Serikali ya Cuba wametupatia Wakufunzi wa Ngumi, Judo
na Riadha. Hivi sasa wanatoa nafasi za mafunzo nne kila mwaka kwenye
mafunzo ya michezo na utaalamu wa mazoezi ya viungo.
Hivyo,
pamoja na kutumia fursa ya ziara hiyo kuimarisha mahusiano baina ya
nchi hizi mbili Tanzania itatumia nafasi hiyo kujikita katika kuanzisha
ushirikiano kwenye maeneo mapya hususan biashara na uwekezaji.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 30 Septemba 2016
|
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269