Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu
ya Iran imekanusha vikali madai yasiyo na msingi yaliyotolewa na Rais
Ismail Omar Guelleh wa Djibouti aliyedai kuwa, Tehran inaingilia masuala
ya ndani ya nchi nyingine na kumtaka atatue matatizo ya nchi yake
kwanza na aache kutekeleza amri anazopokea kutoka kwa watu wengine.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje
ya Iran Bahram Qassemi alisema hayo jana na kuwataka viongozi wa
Djibouti watumie hekima na waache kutoa madai yasiyo na msingi.
Amesema, ni vyema kwa Rais wa Djibouti
kuacha kutoa madai ya uongo na yasiyo na msingi anayoyasikia kutoka kwa
wengine, na aangalie mambo kwa uhalisia wake kwa ajili ya kuimarisha
utulivu na manufaa ya wananchi wa eneo hili zima.
Qassemi amesisitiza kuwa, madai kama
hayo ya Rais wa Djibouti kamwe hayawezi kusaidia kuimarisha usalama na
amani ya eneo hilo, wala hayawezi kutatua migogoro ya Syria, Yemen na
Bahrain.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya
Iran pia amemtaka Rais wa Djibouti kusoma kwa makini historia na
ustaarabu wa mataifa ya dunia hususan ya eneo hili.
Siku ya Jumatano, Rais wa Djibouti
alikariri madai ya Saudi Arabia ya kwamba eti Iran inaingilia masuala ya
nchi za Kiarabu kama vile Yemen, Bahrain, Syria na Iraq na kwamba eti
nchi za Kiarabu zina haki za kukabiliana na uingiliaji huo wa Iran
katika masuala ya eneo hili.
Itakumbukwa pia kuwa, tarehe 6 Januari
mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mahmoud Ali Youssouf
alisema kuwa, nchi hiyo ndogo ya Pembe ya Afrika imeamua kukata uhusiano
wake na Iran ili kufuata siasa za Saudi Arabia.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269