Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram
la Nigeria limeshadidisha mashambulio yake katika miezi ya karibuni
nchini Cameroon ambapo kwa mujibu wa ripoti ya kundi la kimataifa la
migogoro kundi hilo limeshambulia kambi tatu za jeshi la Cameroon katika
maeneo ya Darak, Diguina na Kolofata nchini humo.
Licha ya mpasuko na mgawanyiko uliojitokeza katika miezi ya
karibuni ndani ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kutokana
na hitilafu za ndani, mashambulio ya kigaidi ya kundi hilo yangali
yanaendelea kushuhudiwa.
Mashambulio ya karibuni ya Boko Haram katika maeneo ya kaskazini mwa
Cameroon yameshadidi baada ya mamlaka za nchi hiyo kutaka kufungua tena
mpaka wa pamoja wa Cameroon na Nigeria.
Mpaka wa pamoja Cameroon na Nigeria katika maeneo ya kaskazini mwa
Cameroon ulifungwa mwaka uliopita wa 2015 kutokana na kuenea na
kushadidi machafuko na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram.
Kutokana na hali hiyo hatua kali zaidi za usalama zilichukuliwa ambapo
hivi sasa vikosi vya jeshi la Cameroon vimewekwa katika hali ya
tahadhari kwenye eneo la Ziwa Chad.
Japokuwa ngome kuu ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram iko
katika mji wa Maiduguri makao makuu ya jimbo la Borno kaskazini
mashariki mwa Nigeria, lakini tangu miaka mitatu iliyopita mashambulio
ya kundi hilo yameenea hadi katika nchi tatu jirani na Nigeria za
Cameroon, Niger na Chad.
Katika kukabiliana na kitisho cha Boko Haram cha kuhatarisha amani na
uthabiti wa eneo viongozi wa nchi hizo jirani pamoja na Nigeria yenyewe
waliamua kuunda kikosi cha pamoja cha askari 10,000 kukabiliana na
kundi hilo.
Kuanzia mwezi Februari mwaka jana operesheni za pamoja za nchi hizo
nne zilianza dhidi ya ngome za kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko
Haram ambapo idadi kadhaa ya magaidi wa kundi hilo la kitakfiri
wamejisalimisha kwa jeshi la Cameroon.
Wakati huohuo makamanda wa jeshi la Cameroon wamelitangazia na
kulionya kundi la kigaidi la Boko Haram kwamba ima lijisalimishe au
lijue kuwa mwisho wake unakaribia.
Kwa mtazamo wa wafuatiliaji wa masuala ya Afrika Magharibi viongozi
wa nchi za eneo la Ziwa Chad ambazo ni Nigeria, Niger, Chad na Cameroon
wameungana na wana dhamira ya kweli ya kuliangamiza kundi la Boko Haram.
Katika kikao cha 11 za Kiafrika kilichofanyika tarehe 23 mwezi huu
katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris, Rais Mahamadou Issoufou wa Niger
alisisitiza kwa mara nyingine tena juu ya kupambana na ugaidi katika
eneo la magharibi mwa Afrika.
Sambamba na hayo maafisa wa usalama na intelijinsia wa Nigeria
wameanzisha operesheni ya kuwasaka na kuwatokomeza watu 55 wanaoshukiwa
kuwa na uhusiano na Boko Haram. Ukweli ni kwamba hujuma na miripuko ya
mara kwa mara inayolenga mabomba ya mafuta katika eneo lenye utajiri
mkubwa wa nishati hiyo la kusini mwa Nigeria imeiweka katika hali ngumu
serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo ambayo inalazimika
kukabiliana na tatizo hilo sambamba na kupambana na kundi la kigaidi na
kitakfiri la Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa nchi.
Kwa mtazamo wa wachambuzi, operesheni zinazotekelezwa hivi sasa na
jeshi la Cameroon dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram zina umuhimu
mkubwa kwa sababu matunda yake yatakuwa ni kwa faida ya nchi zote za
eneo.
Katika miaka ya karibuni kundi la Boko Haram limekuwa tishio kubwa la
ugaidi kwa Nigeria na nchi jirani katika eneo la magharibi mwa Afrika
kama ambavyo kundi jingine la kigaidi la Al-Shabaab nalo pia
linahatarisha amani na uthabiti wa Somalia na nchi za Mashariki na Pembe
ya Afrika. Katika hali kama hiyo kuwa na msimamo na ushirikiano wa
pamoja wa kieneo kati ya nchi jirani ni wenzo muhimu wa kuyashinda
makundi ya kigaidi ambayo yamechipua taratibu katika maeneo tofauti ya
Afrika na hivi sasa yanaendelea kushamiri na kuzagaa ndani ya bara
hilo.../
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269