Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
KAMANDA wa
Polisi wa kikosi cha usalama Barabarani Mohammed Mpinga ametoa wito kwa
madereva wote ikiwemo madereva wa Serikali na Mashirika ya Umma
kuzingatia sheria za Usalama Barabarani.
Kamanda
Mpinga ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam wakati alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa kampeni ya kitaifa
ya “Abiria paza sauti” inayotarajiwa kuzinduliwa tarehe 28 Novemba,
mwaka huu.
Kamanda
Mpinga alisema kumekuwa tabia ya baadhi ya madereva hususani wa
Serikali na mashirika ya umma ya kutofuata sheria za usalama barabarani
kwa kuendesha magari kwa mwendokasi, na kuwaonya kuwa sheria ni msumeno
na inapaswa kufuatwa na kila mtu.
“Kumekuwa
na madereva hasa wa magari madogo kusafiri kwenda maeneo mbalimbali ya
nchi huku wakiwa hawana uzoefu wa kuendesha umbali mrefu na hivyo
kupelekea uvunjifu wa sheria za barabarani kwa kuendesha kwa mwendokasi
na kusababisha ajali” alifafanua Kamanda Mpinga.
Akifafanua
zaidi Kamanda alisema uzoefu unaonyesha kuwa katika kipindi hiki cha
kuelekea mwisho wa mwaka kumekuwa na ongezeko kubwa la magari
barabarani, na hivyo kuwataka wananchi kuzingatia sheria za barabarani
ili kuweza kupunguza ajali za barabarani.
Kwa
upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Mabalozi wa Usalama
Barabarani, Jackson Kalikumtima alisema lengo la kampeni ya Paza Sauti
ni kuhamasisha ushiriki kamilifu wa wananchi katika kukabiliana na ajali
kwa kuchukua hatua stahiki bila ya uwepo wa askari.
Pia
alisema kuwa kampeni hiyo imelenga kubadili tabia na mtazamo wa
madereva kuhusu usalama barabarani ili waendeshe kwa kuzingatia sheria
bila shuruti na kubadili mtazamo wa wananchi kuhusu usalama barabarani
ili watambue kuwa usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja.
Naye Mwanasheria
wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, (ASP), Deus Sokoni alisema
mkakati wa kupunguza ajali barabarani katika kampeni hiyo umelenga
katika kutoa elimu kwa jamii ili kuona suala la usalama barabarani ni
jukumu la kila mmoja na si jukumu la Polisi pekee.
“hakuna
asiyetumia barabara duniani, hatutaki ajali tunataka kuishi salama,
hivyo kila abiria anawajibu wa kutunza na kutii sheria za barabarani “
aliongeza Mwanasheria huyo.
Mwenyekiti wa Chama
cha Kutetea Abiria Taifa (CHAKUA), Hassan Mhanjama aliwataka abiria
wote nchini hususani wanaotajaria kusafiri mwishoni mwa mwaka
kuwasiliana na Mamlaka ya Usafirishaji SUMATRA pindi watakapopandishiwa
nauli mbali na taratibu zilizopo.(P.T)
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269