Balozi Tuvako Manongi na Rais wa ICC Jaji
Gumendi baada ya kumaliza mazungumzo yao
|
Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC) Jaji Slivia Fernandez de Gumendi ya Ijumaa wiki hii amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Matiafa, Balozi Tuvako Manongi.
Katika Mazungumzo hayo baina ya Jaji Gumendi na Balozi Manongi yaliyofanyika katika Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania, Rais wa ICC aliishukuru Tanzania kwa hotuba yake iliyotolewa na Balozi siku ya Jumatatu wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipopokea na kujadilia Ripoti ya ICC.
Kwa mujibu wa Rais wa ICC Jaji Slivia Fernandez de Gumendi hotuba ya hiyo ya Tanzania ilikuwa yenye uwiano na pia ilitoa ushauri au mapendekezo ya namna gani Mahakama hiyo inavyoweza kuboresha uhusiano na wanachama wake kwa mujibu wa Mkataba wa Roma.
“Nilikusikiliza kwa makini sana wakati ulipokuwa unatoa hotuba yako, nilinukuu kila hoja ulizokuwa unazizungumza .Hotuba ya Tanzania ilikuwa yenye uwiano (balanced) na ningependa kuitumia fursa hii kuishukuru Tanzania kwa hilo.
Rais huyo wa ICC amekiri kwamba anadhani ni wakati muafaka kwa wadau wa pande mbili kukaa na kuzungumza kama ambayo Tanzania na wanachama wengine wameshauri hasa kutokana na kile alichosema, kwamba, kila nchi imekuwa na tafsri tofauti na uelewa tofauti kuhusu baadhi ya vipengere (articles) zinazohusu Mkataba wa Roma unaounda Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai.
Kwa upande wake Balozi Manongi amesema, ushauri na mapendekezo ambayo yametolewa na Tanzania pamoja na nchi nyingine hayalengi katika kutaka kubadili Mkataba wa Roma au kuipunguzia nguvu ya kiutendaji Mahakama hiyo.
“Tungependa sana ieleweke kwamba tunaposhauri kukaa na kuzugumza kusitafsiriwe kana kwamba tunataka kupunguza nguvu ya utendaji wa chombo hiki ambacho wote tunaamini kwamba kinastahili kuwapo. Tunachosema na kusisitiza, kwamba kila upande unahoja za msingi basi tuzijadili kwa kuzungumza” akasisitiza Balozi Manongi.
Rais wa ICC na Balozi Manongi walibadilishana mawazo juu na masuala mbalimbali kuhusu utendaji kazi wa Mahakama ya ICC ikiwa ni pamoja na kuangalia ni maeneo gani ambayo Mahakama na wanachama wake wanaweza kujadiliana.
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akiwa katika mazungumzo na Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC) Jaji Slivia Fernandez de Gumendi. Katika mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ubalozi wa Tanzania, Rais wa ICC alitumia fursa hiyo kutoa shukrani zake kwa Tanzania kwa hotuba ambayo si tu ilikuwa na ushauri wa namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya Mahakama hiyo na Wanachama wa Mkataba wa Roma hususani kutoka nchi za Afrika lakini pia kwamba ilikuwa ni hotuba ya uwiano. Jumatatu wiki hii Tanzania ilikuwa kati ya nchi zilizozungumza wakati Ripoti ya utendaji kazi ya ICC ilipowasilishwa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269