Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran amesema lengo la mazoezi ya majini ya Wilayat 95 ni
kutuma ujumbe wa amani na urafiki kwa nchi za eneo sambamba na kuinua
kiwango cha kujihami Iran.
Admeri Habibullah Sayyari Kamanda wa Jeshi la Majini la Iran
aliyasema hayo Jumamosi usiku katika mahojiano na Kanali ya Pili ya
Televisheni ya Iran. Amesema awamu ya mwisho ya mazoezi ya kijeshi
yaliyopewa jina la "Wilayat 95" yanaanza leo Jumapili na kuongeza kuwa,
upana wa eneo la mazoezi ni karibu kilomita mraba milioni mbili kuanzia
Lango Bahari la Hormoz kuelekea Bahari ya Oman hadi Kaskazini mwa
Bahari ya Hindi yapata daraja 10 kutoka mstari wa ikweta.
Admeri Sayyari amesema, kati ya malengo ya mazoezi hayo ni kuwapa
wanajeshi vijana uzoefu wa kikazi na kufanyia majaribio silaha mbali
mbali. Aidha ametaja lengo jingine la luteka hiyo kuwa ni kudumisha
amani katika eneo na kukabiliana na ugaidi pamoja na uharamia na
kuongeza kuwa: "Hadi sasa misafara ya meli za kivita za Iran imezisaidia
meli za nchi 25 duniani zikiwemo za Ufaransa, Uingereza na Marekani
katika kukabiliana na maharamia.
Admeri Sayyari amesema tokea mwaka 2008 hadi sasa, manowari za Iran
zimesindikiza meli za mafuta na za kibiashara zipatazo 3,850 katika
eneo la Bahari ya Hindi na Babul Mandab.
Admeri Sayyari amesema Iran ina uhusiano mzuri na nchi zote zenye
mipaka katika Bahari ya Hindi na Bahari ya Kaspi na kuongeza kuwa, mwaka
2018 Iran itakuwa mwenyeji wa makamanda wa majeshi ya majini ya nchi
zinazopakana na Bahari ya Hindi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269