Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameelezea
kusikitishwa kwake na namna Mahakama inavyoshughulikia kesi zinazohusiana na
ukwepaji wa kodi na ametoa wito kwa mahakama na wadau wake kujipanga
kukabiliana na dosari hiyo inayorudisha nyuma juhudi za maendeleo ya nchi.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 02 Februari, 2017 katika sherehe za
uzinduzi wa mwaka wa Mahakama (Siku ya
Sheria) zilizofanyika katika uwanja wa Mahakama uliopo Mtaa wa Chimala,
Kivukoni Jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa katika kipindi cha kuanzia
mwaka 2005 hadi mwaka 2016 Serikali haijalipwa kiasi cha Shilingi Trilioni 7.5
licha ya kushinda kesi za ukwepaji kodi zilizokuwa zinawakabili washitakiwa
mbalimbali.
Dkt.
Magufuli ameipongeza Mahakama na wadau wake kwa kazi kubwa inayofanywa kuleta
mabadiliko na uboreshaji wa huduma na miundombinu na ametaka kauli mbiu ya
mwaka huu isemayo “Umuhimu wa utoaji wa
haki kwa wakati kuwezesha ukuaji wa uchumi” itekelezwe vizuri kwa
kutanguliza maslai ya Taifa ikiwemo kuhakikisha wanaopatikana na hatia ya
kukwepa kodi wanalipa.
“Haiwezekani
mwekezaji anachimba madini yetu, kodi halipi, anashitakiwa mahakamani
anashindwa, halafu pesa haitolewi.
“Sasa
tujiulize, kama utoaji haki unaakisi ujenzi wa uchumi wa nchi ni kwa kiasi gani
kesi zenye thamani ya Shilingi Trilioni 7.5 zimeathiri uchumi?”
amehoji Mhe. Rais Magufuli.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli ametaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) na Mahakama wajipange kwa pamoja ili kushughulikia ipasavyo
mashauri mbalimbali na kuondokana na migongano ambayo imekuwa ikidhohofisha
ufanisi wa shughuli za kimahakama.
Pia
Dkt. Magufuli ameahidi kushughulikia tatizo la ufinyu wa bajeti na maslai ya
wafanyakazi wa Mahakama wakiwemo Majaji.
Pamoja
na kumpongeza na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa
kwa Mahakama, Kaimu Jaji Mkuu wa Mahakama Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma
amesema katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama, mwaka 2016 jumla ya
mashauri 279,331 yamesikilizwa sawa na asilimia 101 ya matarajio ya kusikiliza
mashauri 276,147, Mahakama imefanikiwa kumaliza kesi 248 kati ya kesi 249 za
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 zilizohusisha Ubunge na Udiwani na pia Mahakama Kuu
imefanikiwa kuanzisha Divisheni ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi (Mahakama ya Mafisadi)
Sherehe
hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman
Makungu, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe, Katibu Mkuu
Kiongozi Mhe. John Kijazi, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi Mhe.
Ferdinand Leons Wambali, Majaji wa Mahakama Kuu, Mawakili, Viongozi wa Dini na
Siasa na wawakilishi wa Taasisi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269