Rais
Mstaafu na Mjumbe Maalum wa Kamisheni ya Kimataifa ya ELimu, Dkt.
Jakaya Kikwete akikaribishwa kwa furaha na mwenyeji wake Rais wa Benki
ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Akinwumi Adesina ofisini kwake jijini
Abidjan, Ivory Coast
Rais
Mstaafu na Mjumbe Maalum wa Kamisheni ya Kimataifa ya Elimu Dkt. Jakaya
Kikwete akiwasilisha ripoti ya Kizazi cha Elimu kwa Rais wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika, Dkt. Adesina
Rais
Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB) Dkt. Adesina katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mkutano.
Rais
Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akibadilishana mawazo na Rais wa
Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Akinwumi Adesina na Makamu wa Rais wa
Benki ya Dunia Dkt, Makthar Diop pembezoni mwa mkutano huo.
Rais
Mstaafu na Mjumbe Maalum wa Kamisheni ya Kimataifa ya Kupendekeza Namna
Bora ya Kugharamia Fursa za ELimu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekutana
na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Akinwumi Adesina
alipomtembelea katika Makao Makuu ya Benki hiyo jijini Abidjan, Ivory
Coast.
Katika
mazungumzo yao, Rais Mstaafu Kikwete amewasilisha kwa Rais Adesina
ripoti ya Kamisheni ya Elimu na kuwasilisha rai ya Kamisheni hiyo ya
kuiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika kusaidia nchi za Afrika kugharamia
miradi na mageuzi ya sekta ya elimu katika nchi zao. Rai hiyo ya
Kamisheni inatokana na ripoti kubaini kuwa misaada na mikopo inayotolewa
kwa sekta ya elimu imekuwa ikishuka ikilinganisha na zile zinazotolewa
kwa miradi ya afya na miundombinu. Kamisheni inaamini kuwa bila kuongeza
uwekezaji katika sekta ya elimu, watoto wapatao milioni 223 duniani
(takribani milioni 160 wakiwa Afrika) watakosa fursa ya kupata elimu
ifikapo mwaka 2030.
Kwa
upande wake, Rais Adesina ameupokea ujumbe huo na kusema kuwa takwimu
zilizoibuliwa na Ripoti ya Kamisheni 'zinakatisha tamaa na pia zinatoa
changamoto'. Rais Adesina ameahidi kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika
itaitizama Ripoti hiyo na mapendekezo yake na iko tayari kufanya kazi
kwa karibu na Kamisheni katika kutafuta majawabu ya changamoto zilizopo
katika elimu barani Afrika. Amesema kuwa Benki yake inatambua kuwa
kuwekeza katika vijana na nguvu kazi ya Afrika ndio jawabu la maendeleo
ya uhakika huko mbeleni.
Katika
hatua nyingine, Rais Mstaafu amekutana na Makamu wa Rais wa Benki ya
Dunia Dkt. Makhtar Diop pembezoni mwa mkutano wake na Rais wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika. Ziara ya Rais Mstaafu nchini Ivory Coast
itahitimishwa kwa kukutana na Rais wa Ivory Coast Mhe. Alassane
Ouattara.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269