Nchi za kundi la 20 zimetaka kupanuliwa ushirikiano na nchi za Kiafrika.
Kikao cha siku tatu cha Mawaziri wa Utalii wa kundi la 20 na
wawakilishi wa mataifa ya Kiafrika kilihitimisha shughuli zake Ijumaa
iliyopita mjini Johennesburg Afrika Kusini. Katika kikao hicho,
Ujerumani kama mwenyekiti wa kundi hilo ilitaka kuimarishwa ushirikiano
wa muda mrefu baina ya nchi za kundi la 20 na mataifa ya Afrika.
Mwakilishi wa Ujerumani sanjari na kusisitizia mpango wa ustawishaji
bara la Afrika unaoitwa ‘Agenda ya 2063 alisema kuwa, Afrika na nchi za
kundi la 20 zinatakiwa kufanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuinua kiwango
cha ushirikiano wa pande mbili. Kikao cha mjini Johennesburg sanjari na
kuashiria nafasi chanya ya Afrika duniani, kimesisitiza pia juu ya
ubunifu wa mipango zaidi ya kisasa kwa ajili ya nchi za bara hilo.
Kundi la 20 huandaa mijadala huru baina ya nchi za viwanda na
zinazoinukia kiuchumi, kuhusiana na uthabiti wa uchumi wa dunia. Kundi
hilo huunga mkono ukuaji wa uchumi na ustawi katika nchi mbalimbali za
dunia lengo kuu likiwa ni kuzishirikisha nchi wanachama katika
kuimarisha muundo wa masoko ya kifedha ya kimataifa na kadhalika kuandaa
mazingira ya mazungumzo kuhusu sera za fedha na ushirikiano wa
kimataifa.
Nchi wanachama za kundi hilo zinamiliki asilimia 90 ya pato jumla,
asilimia 80 ya biashara ya dunia na theluthi mbili ya idadi ya watu wote
duniani. Sisitizo la kupanuliwa ushirikiano na nchi za Kiafrika lina
maana kwamba, kutumia nguvukazi ya vijana na vyanzo vyake asilia
kutasaidia nchi hizo kuinukia kiuchumi katika medani ya kimataifa. Hii
ni kusema kuwa hivi sasa nguvukazi barani Afrika inaongezeka kwa kasi.
Hivyo ikiwa nchi za Kiafrika zitaweza kuwadhaminia vijana wao mahitaji
ya elimu na ujuzi, basi nguvukazi hiyo kubwa itasaidia katika kuinua
uchumi wa mataifa hayo. Hivi sasa uwekezaji wa kigeni umeongezeka zaidi
barani Afrika kuliko eneo lolote lile duniani.
Chunguzi zinaonyesha kwamba, matarajio ya ukuaji uchumi wa muda mrefu
kutokana na mahitaji ya kigeni na mabadiliko ya ndani barani Afrika, ni
mambo yanayopewa umuhimu mkubwa. Mbali na hayo bara la Afrika
linategemewa sana kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya dunia katika
sekta ya mafuta, gesi asilia, madini, chakula, mazao ya kilimo na
vyanzo vingine asilia. Hii ni kusema kuwa bara hilo linamiliki asilimia
10 ya akiba ya mafuta duniani, asilimia 40 ya akiba ya dhahabu na
asilimia 80 hadi 90 ya madini mbalimbali. Ni kwa msingi huo ndio maana
ikaaminiwa kuwa ukuaji uchumi barani Afrika unaweza kuandaa fursa za
kutosha za ajira kwa nchi za bara hilo. Kama ambavyo kilimo pia kinaweza
kuandaa nguvu kubwa kwa ajili ya mashirika makubwa katika sektka hiyo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269