Shirika la Afya Duniani, WHO limesema gharama
za matibabu ya saratani ni kubwa kuliko zile za kinga na tiba wakati wa
hatua za mwanzo za ugonjwa huo unaosababisha kifo cha mtu mmoja katika
kila watu sita duniani kote.
WHO imetolea mfano mwaka 2010 ambapo gharama za kiuchumi na
kiafya zilizotokana na saratani ilikuwa dola trilioni 1.16 duniani kote.
Ili kupunguza gharama, WHO imezindua mwongozo mpya wa kuwezesha nchi
yoyote bila kujali kipato chake iweze kuimarisha ugunduzi wa saratani
mapema.
WHO ilitoa kauli hiyo Jumamosi Februari Nne ambayo ni Siku ya
Saratani Duniani. Kwa munasaba wa siku hiyo WHO imezindua mwongozo mpya
wa kuwezesha uchunguzi wa mapema wa ugonjwa huo hatari unaosababisha
vifo vya watu milioni 8.8 kila mwaka duniani, kati ya wagonjwa milioni
14 wanaobainika kuwa nao.
WHO inasema hali si shwari kwani idadi inaongezeka mwaka hadi mwaka
na hivyo njia pekee ni kuimarisha mbinu za kubaini mapema kwani hata
visababishi vya saratani navyo vinaongezeka.
Shirika hilo linasema saratani haipaswi kusalia adhabu ya kifo wakati
huu ambapo kuna kampeni za kudhibiti visababishi kama vile matumizi ya
tumbaku, unywaji wa pombe na mlo usio bora.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269