Kaimu
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Julius Mbilinyi akifungua Kikao Kazi
cha Maafisa wa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa (hawapo pichani) katika cha
siku mbili kinachoanza leo katika Hotel ya Edema Mkoani Morogoro.
Katikati
ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Julius Mbilinyi akiwa katika
picha ya pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa wanaohudhuria
kikao kazi kuhusu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza
Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto katika mkutano unaofanyika Hotel ya
Edema Mkoani Morogoro.
Baadhi
ya washiriki wa kikao kazi cha Maafisa Maendelo ya Jamaii wa Mikoa
wakifuatilia maelezo ya wawezeshaji kuhusu utekelezaji wa Mpango Kazi wa
taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto katika Hotel ya
Edema, mkoani Morogoro.
………………….
Na erasto ching’oro- Msemaji: Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo imefungua
kikao cha siku mbili cha Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa kwa ajili
ya kuwajengea uwezo kuhusu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa
Kuzuia na Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017-2022).
Akifungua
kikao hicho, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Bw. Julius Mbilinyi ambaye ni
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia aliwashukuru Washirika wa
Maendeleo katika kuhakikisha kuwa tatizo la ukatili dhidi ya wanawake na
watoto linatokomezwa hapa nchini. Aliyataja mashirika haya kuwa ni
pamoja na UN-WOMEN, Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), na Shirika
la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Haki na Ustawi wa Watoto
(UNICEF).
Mgeni
Rasimi Kaimu Mkurugenzi wa Jinsia, aliwapongeza Maafisa Maendeleo ya
Jamii kwa shughuli mbalimbali ambazo wamekuwa wakizitekeleza katika
maeneo yao ya kazi, juhudi ambazo zimekuwa na mchango katika kutokomeza
ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini. Alifafanua kwamba, baada ya
mafunzo haya, maafisa hao wataendelea kutekeleza majukumu yao
kikamilifu ili kupunguza ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka
2021/20122.
Wanawake
na watoto wamekuwa wakifanyiwa ukatili kwa kisingizio cha mila na
desturi. Aidha, mfumo dume umesababisha wanawake kutoshiriki kikamilifu
katika maamuzi yanayohusu maendeleo yao, katika ngazi ya kitaifa, katika
ngazi ya jamii na hata katika familia zao. Mara nyingi tumesikia
wanawake na watoto wakipigwa, kubakwa na wakati mwingine kuuwawa na watu
wa karibu. Vitendo hivi ni ukatili wa hali ya juu na vinaleta simanzi
na madhara makubwa katika jamii yetu.
Akiongea
na Maafisa Maendeleo wa Mikoa, Bw. Mbilinyi alieleza kuwa madhara ya
vitendo vya ubaguzi, unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto
huwaathiri kiafya na kisaikolojia na kijamii ambapo uthoofisha ushiriki
wa wanawake katika shughuli za maendeleo na hivyo kurudisha nyuma
jitihada za kuiwezesha nchi yetu kuwa ya viwanda na uchumi wa kati.
Wizara kwa kuzingatia changamoto hizo, imekuwa ikifanya juhudi za
kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ikiwemo uandaaji wa
Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na
Watoto.
Katika
kuhakikisha kuwa Mpango Kazi huu unaeleweka na kutekelezwa ipasavyo
Wizara imetoa mafunzo kuhusu Mpango huu kwa wadau mbalimbali. Mafunzo
yaliyotolewa ni mwendelezo wa mafunzo yaliyotolewa kwa waratibu wa
Madawati ya Jinsia kutoka katika Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala
wa Serikali kuhusu Mpango kazi huo ili kuwezesha utekelezaji wake.
Kaimu
Mkurugenzi wa maendeleo ya Jinsia amefafanua kuwa, Tafiti mbalimbali
ikiwemo Taarifa ya Idadi ya Watu na Afya ya mwaka 2015-2016 inaonesha
kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia bado vipo. Taarifa hii inaonyesha
kuwa wanawake 4 kati ya 10 wamewahi kukumbana na ukatili wa kimwili
tangu wakiwa na umri wa miaka 15. Taarifa hiyo inaonesha kuwa wanawake 2
kati ya 10 walikumbana na ukatili wa kimwili wakati utafiti huo
ukifanyika. Ukatili wa kimwili unaongezeka kadri umri unavyoongezeka;
asilimia 22 ya wanawake wenye umri wa miaka 15-19 wamewahi kukumbana na
ukatili wa kimwili, ukilinganisha na asilimia 48% ya wanawake wenye umri
wa miaka 40-49.
Akitoa
nasaha zake Afisa Mendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Paul
Shayo alieleza kuwa mafunzo haya yatawajengea umahiri, kuweza kutekeleza
Mpango Kazi kwa ufanisi. Mbinu watakazopata zitakuwa mwongozo wa
kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii. Vile vile,
amekiri kwamba, uzoefu na weledi utakaoupata kupitia mafunzo haya
utawasaidia wahanga wa vitendo vya ukatili kupata huduma stahiki kwa
kuwaunganisha na watoa huduma katika maeneo mbalimbali.
Mikoa ambayo itajumuishwa katika awamu ya pili ya mafunzo hayo ni Kagera, Mara, Kigoma na Katavi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269