Utawala wa Kizayuni umemzuia Ripota wa
Masuala ya Haki za Binadamu kuingia katika ardhi za Palestina
zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Shirika la Kutetea Haki za
Binadamu la Human Rights Watch hivi karibuni lilitoa ripoti zinazokosoa
jinai za utawala huo wa Kizayuni.
Omar Shakir Ripota wa Masuala ya Haki za Binadamu wa Shirika la
Human Rights Watch (HRW) amesema kuwa utawala wa Kizayuni umekataa
kumpatia viza ya kuingia huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Utawala
huo siku kadhaa zilizopita pia uliuzuia ujumbe wa bunge la Ulaya
kuingia huko Ukanda wa Ghaza. Katika hali ambayo ukosoaji na malalamiko
dhidi ya hatua za mabavu za utawala wa Kizayuni unazidi kuongezeka,
kundi moja kwa jina la "Kundi Kazi linalojihusisha na Watoto na Mizozo
ya Silaha" limeutaka Umoja wa Mataifa kulijumuisha jina la jeshi la
Israel katika faharasa ya wakiukaji wa haki za watoto. Ombi la kutaka
kujumuishwa jina la utawala wa Kizayuni katika orodha ya wakiukaji wa
haki za watoto limetolewa huku mwaka 2015 pia kukitolewa ombi kama hilo
na taasisi za kisheria za kimataifa zilizotaka kujumuishwa jina la
utawala wa Kizayuni katika orodho hiyo. Hata hivyo ombi hilo
halikutekelezwa kutokana na mashinikizo ya Marekani na utawala wa
Kizayuni.
Taasisi za kisheria za Magharibi kwa kawaida hunyamaza kimya na
kutochukua hatua yoyote mbele ya jinai zinazofanywa na Israel; na kwa
hali yoyote ile radiamali zinazoonyeshwa na taasisi hizo kwa jinai za
utawala wa Kizayuni na ukwamishaji wake katika utendaji wa taasisi hizo
zinapaswa kuzingatiwa. Ripoti nyingi zimewasilishwa katika miaka ya hivi
karibuni zikionyesha wazi wazi miamala na vitendo visivyo vya
kibinadamu na vya utumiaji mabavu vinavyotekelezwa na utawala wa
Kizayuni dhidi ya makundi ya kutetea haki za binadamu katika ardhi za
Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Hii ni katika hali
ambayo Umoja wa Mataifa kufikia sasa haujaonyesha radiamali yoyote kali
kwa hatua za Israel za kukiuka pakubwa haki za binadamu kukiwemo
kuwavunjia heshima na kuamiliana kusikostahili na wawakilishi wa taasisi
za kisheria. Vitendo visivyoweza kuhalalishwa vya Israel mkabala na
makundi na wanaharakati wa haki za binadamu na kamati za kutafuta ukweli
za Umoja wa Mataifa vinabainisha wazi kwamba hakuna msingi wowote wa
kisheria unaoweza kuukabili utawala huo ulio dhidi ya ubinadamu. Utawala
wa Kizayuni ambao unahofia kufichuliwa zaidi jinai zake ambazo zinaweza
kufuatiliwa kimataifa, umekuwa ukikwamisha kwa njia mbalimbali utendaji
wa wajumbe wa Umoja wa Mataifa na wa taasisi nyingine za kimataifa
zinazofuatilia jinai za Israel huko Palestina; na wakati huo huo
kuzizuia tume za uchunguzi na za kutafuta ukweli za kimataifa na
maripota wa Umoja wa Mataifa kuingia katika ardhi za Palestina
zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Hii ni katika hali ambayo katika
kuendelezwa siasa za kukaa kimya Umoja wa Mataifa mbele ya jinai
zinazofanywa kila uchao na utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wa
Palestina wasio na hatia, Ban Ki-moon, katibu mkuu wa umoja huo
aliyemaliza muda wake alijizuia kuchukua hatua dhidi ya Israel kutokana
na mashinikizo ya Magharibi, licha ya kutakiwa na jamii ya kimataifa
kuliorodhesha jina la utawala wa Kizayuni katika orodha ya tawala
zinazokiuka haki za watoto. Si kwa Israel pekee, bali Umoja wa Mataifa
hata umekuwa ukitekeleza siasa za kunyamaza kimya mbele ya jinai za nchi
kama vile Saudi Arabia; na hivyo kuziandalia uwanja wa kuendeleza jinai
zao za kukiuka haki za watoto.
Itakumbukwa kuwa katibu mkuu huyo wa zamani aliliweka jina la Saudi
Arabia katika faharasa ya wakiukaji wa haki za watoto kutokana na
kutenda mauaji dhidi ya watoto wa Yemen na kisha baada ya muda mfupi
akalitoa jina la nchi hiyo katika orodha hiyo baada ya kutishwa na
Saudia kwamba ingekata misaada yake ya kifedha kwa umoja huo. Katika
mazingira kama hayo utawala wa Kizayuni na Saudi Arabia zinapata kiburi
cha kuendeleza kirahisi jinai zao dhidi ya watoto; suala ambalo
limewapelekea walimwengu kuendelea kushuhudia katika karne ya ishirini
na moja vitendo vya dhulma, ukatili na mabavu vya tawala hizo wauaji wa
watoto.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269